24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

UTAJUAJE AMEPOTEZA UPENDO WA AWALI?

INAWEZEKANA upo katika uhusiano na mpenzi ambaye hukumwelewa vizuri mwanzoni, lakini sasa unagundua kwamba amepoteza uwezo wa kupenda kama ilivyokuwa awali.

Ni vigumu sana kugundua hili mapema, lakini ukimchunguza na kuwa mkweli kwake, ni rahisi kukueleza ukweli huu uliojificha moyoni mwake.

Pengine wakati unakutana naye, alikukatalia akisema muda wa kuwa na mpenzi bado, lakini ukaendelea kumsumbua na kukukubalia, mwisho wa siku ukagundua hafurahii uhusiano wenu.

Hili huwa tatizo kubwa sana kwa walio wengi. Wakati mwingine yawezekana ukawa unafanya bidii ya kumshawishi mpenzi mpya lakini akawa katika tatizo hili.

Kila siku anakuzungusha, lakini siku moja akaamua kukueleza ukweli, kwamba anashidwa kukupenda! Hiyo ni hatua nzuri kwako, maana yamkini sasa unaweza kusuka mbinu mpya za kurejesha ule upendo wake wa awali uliotoweka ili muweze kuanzisha uhusiano ulio na nguvu.

Katika vipengele vifuatavyo, vitakusaidia kwanza kung’amua mpenzi ambaye amepoteza upendo wake wa awali au patna ambaye una mpango wa kuanzisha uhusiano naye lakini hana uwezo wa kupenda tena kutokana na sababu mbalimbali.

Sasa hebu twende  katika vipengele vifuatavyo, bila shaka kuna kitu kipya utakijenga kichwani mwako.

 

KWANINI HILI HUTOKEA?

Ni muhimu kwanza kujua sababu za kupoteza ule uwezo wa kupenda uliokuwa mwanzo. Angalau kwa kujua, itakusaidia kusogea kwenye ukweli na kuifuata hatua nyingine muhimu zaidi.

Tatizo la kutokuwa na uwezo wa kupenda, limekuwa likiwasumbua wengi sana siku hizi (hasa wanawake). Sababu kubwa zaidi ni kuwa na uhusiano wenye historia mbaya katika kipindi kilichopita.

Mwanamke aliyeachwa na wanaume watatu kwa kipindi cha miezi miwili, hawezi kuwa na uwezo wa kupenda kwa asilimia 100 kama yule ambaye ndiyo kwanza anaanza uhusiano.

Mwanamke aliyeachwa na mwanaume wake aliyedumu naye kwa miaka minne, anaweza kuwa bora zaidi katika uhusiano mpya akitaka kuokoa maisha yake ya kimapenzi kuliko yule ambaye ametoswa mara nyingi zaidi.

Yapo mengi yanayosababisha hilo, lakini kwa uchache ni pamoja na vifuatavyo;

 

(i) Anahisi havutii

Mara nyingi wasichana wakiachwa, hukuchukulia kwamba huenda hawana mvuto sana. Kwahiyo anahisi hata kama atakupenda, akitokea mwenye mvuto zaidi yake, utamtosa kama alivyofanya aliyepita!

 

(ii) Ugonjwa wa moyo

Inawezekana ameshaumizwa sana huko nyuma na kila anapokuangalia anahisi kuteswa tena na hivyo anaogopa tena kupata ugonjwa wa moyo! Ana mashaka, hana amani na mapenzi tena, sababu kubwa ni historia iliyopita.

 

(iii) Walewale!

Lakini kubwa zaidi ni kwamba, mtu akiwa katika athari hii, akili yake yote inamwambia kwamba wote wanaweza kuwa sawa na waliopita.

…uking’atwa na nyoka, hata unyasi ukikugusa unashtuka rafiki zangu! Hisia hizo zinaweza kumfanya akaogopa kuwekeza moyo wake tena kwako.

 

UTAMTAMBUAJE BASI?

Ni afadhali uwe katika hatua za kumfuatilia, kabla hujajua chochote ukagundua wazi kwamba huyu ana tatizo la kupenda, lakini ukishaingia katika uhusiano naye, ni vigumu sana kujua, maana unaweza kuhisi anakudharau kumbe mwenzio ni mgonjwa!

Lakini hapa, zipo njia za kitaalam kabisa ambazo zinaweza kukufanya ugundue mpenzi wako ana tatizo la ugonjwa wa kupenda! Hebu tuone…

 

(i) Siyo muwazi

Sifa ya kwanza kabisa ni kwamba, hataki kukupa nafasi ya kumjua vizuri, anakuogopa, maana ukijua udhaifu wake unaweza kumtenda na kumfanya aishi mpweke kwa mara nyingine. Ni msiri sana, hataki ujue ratiba zake na mambo yake mengi anafanya kwa kushtukiza.

 

(ii) Anachelewa kupokea simu

Hayupo katika penzi la msisimko, kwahiyo hata akiona simu yako anashtuka na kuogopa kupokea haraka. Hana amani ya moyo. Hapendi kukusikia ukisema; “I love you baby!” maana anahisi kama unamuumiza tu. Vinginevyo basi anakuona kama unamzingua tu.

 

(iii) Mgumu kukuambia anakupenda

Ukiwa naye katika mahaba au mtoko, ukimwambia: “Nakupenda sana mpenzi wangu,” yeye anaona shida sana kukujibu anakupenda pia.

Sababu kubwa hapa ni majeraha ya moyo. Huwa anahisi kama atakuwa anakudanganya, maana moyo wake una bandeji kila kona. Upo na mgonjwa!

Jiandae kupata kitabu changu kipya cha SIRI ZA NDOA YENYE FURAHA kitakachokuwa mitaani hivi karibuni.

 

Wiki ijayo tutaendelea na mada hii, USIKOSE!

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles