25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

MANISPAA YAZUIA NDESAMBURO KUAGWA MASHUJAA

 

 

Na Upendo Mosha – Moshi

SIKU chache baada ya familia na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutangaza kufanya shughuli ya kuuaga mwili wa kiongozi wa chama hicho, marehemu Philemon Ndesamburo katika viwanja vya Mashujaa mjini hapa, Halmashauri ya Manispaa ya Moshi imezuia.

Badala yake, halmashauri hiyo imeelekeza Chadema kufanya shughuli hiyo katika Uwanja wa Majengo.

Hoja za kuzuia uwanja huo ni pamoja na udogo, ikilinganishwa na idadi ya watu kutoka ndani na nje ya mji huo wanaotarajia kuhudhuria.

Lakini pia kwa kuwa shughuli itafanyika siku ya kazi itasababisha usumbufu katika taasisi zilizo karibu na viwanja hivyo kama shule na mahakama.

Zuio hilo limezua mtafaruku mkubwa kwa baadhi ya makada wa Chadema na wananchi waliokuwa katika eneo hilo kwa lengo la kufanya maandalizi ya kuaga mwili wa Ndesamburo ikiwamo kufanya usafi.

Katika barua yake yenye kumbukumbu namba MMC/A.20/1/VOL.XV11/107 ya Mei 2, mwaka huu iliyosainiwa na Kaimu Mkurugenzi, Patric Leyana, Halmashauri ya Manispaa ya Moshi imeeleza kuwa Chadema hawatakuwa na kibali cha kutumia uwanja huo kati ya Julai 5 hadi 6 kama walivyoomba “Inaonekana ni vema mkatumia Uwanja wa Majengo kufanya shughuli ya kumuaga marehemu kwa kuwa ni mkubwa zaidi na upo karibu na nyumbani kwa marehemu na uwanja una milango ya kutokea na kuingilia, hivyo itakuwa rahisi kuegesha magari,” ilieleza barua hiyo.

Barua hiyo ya zuio iliwasilishwa na Kaimu Kamanda wa Polisi Wilaya ya Moshi, (OCD) Pankras Mdimi, ambaye aliisoma mbele ya wafuasi wa Chadema waliokuwa wakiendelea na usafi katika viwanja vya Mashujaa na kisha kuwataka kuondoka mara moja katika eneo hilo.

Akizungumzia zuio hilo, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alisema lina sura ya kisiasa.

Alisema shughuli ya umma ya kumuaga Ndesamburo hapo awali ilitangazwa kufanyika katika viwanja vya Mashujaa, ambavyo mara nyingi vimekuwa vikitumika katika shughuli mbalimbali za kijamii na kiserikali, ikiwamo kampeni za ugombea wa urais.

 “Eneo hili la Uwanja wa Mashujaa ni eneo lililopo katikati ya mji wa Moshi, sasa katika mazingira ya kushangaza kidogo wakati maandalizi yakiendelea, tulipata barua kutoka kwa mkurugenzi akielekeza kwamba kiwanja hicho hakitatolewa tena kwa ajili ya shughuli yetu,” alisema.

Alisema Chadema haijashangazwa na kitendo cha kuhamishiwa Uwanja wa Majengo ila kinachowashangaza ni sababu za kipuuzi zilizotolewa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi.

 “Sababu zilizotolewa na Mkurugenzi ni sababu za kitoto na kijinga sana, eti wanadai siku ya shughuli yetu ni siku ya kazi na mahakama itakuwa inaendelea  pamoja na shule, naziita ni za kijinga kwa sababu mahakama imekuwemo eneo hilo hata kabla ya uhuru na mikutano mbalimbali imekuwa ikiendelea pale na mahakama imekuwa ikiendelea na kazi yake na sababu ya shule ni ya kijinga kwani shule zimefungwa,” alisema Mbowe.

Aidha alisema eneo la Majengo walilohamishiwa pia kumekuwa na shughuli mbalimbali ambazo zimekuwa zikiendelea na kwamba kuna hospitali, shule na makazi ya watu.

 “Uwanja wa Majengo umepakana na Shule ya Sekondari Majengo na msingi pamoja na Hospitali ya Majengo. Swali je, hizo hazitasumbuliwa? Hivyo tunaona sababu hizo hazina mashiko,” alisema.

 Alisema Chadema walitegemea kuwa viongozi wa Serikali wangetumia busara katika kushauriana suala hilo na si kufanya ubabe kama walivyofanya jambo ambalo alidai ni dhahiri lilikuwa halina nia njema na ni la kisiasa zaidi.

“Polisi walianza kuzunguka uwanja na kuwataka watu waondoke, sasa jambo hili lilikuwa halina nia njema na limekaa kisiasa na ni dhahiri kwamba Serikali inatia doa zoezi la kumuaga mzee wetu na shujaa wetu Ndesamburo,” alisema Mbowe.

 Alisema mbali na hayo, viongozi wa Chadema na familia ya Ndesamburo wamekaa na kujadiliana kwa kina ni wapi mahala sahihi pa kufanyia shughuli na kufikia uamuzi na kukubali kuhamia Uwanja wa Majengo.

Awali wakizungumza na gazeti hili, baadhi ya makada wa Chadema walionekana kuwa tayari kutokubali kuhamisha shughuli katika uwanja huo.

Mbunge wa Moshi Vijijini, Anthony Komu, alisema wakiwa katika maandalizi ya kufanya usafi katika Uwanja wa Mashujaa, alifika OCD ambaye alidai kuwa ana maelekezo ya kuzuia maandalizi hayo.

 “Yeye OCD amekuwa hapa akidai kuwa ana maelekezo kwamba tuondoke hapa na kwamba Mkurugenzi wa Manispaa anafanya utaratibu mwingine wa kutuhamishia Uwanja wa Majengo,” alisema.

 Komu alishangaa zuio hilo kufanywa kwa Ndesamburo ilihali uwanja huo wa Mashujaa umekuwa ukitumika kufanya shughuli mbalimbali, ikiwamo mikutano ya dini hata katika siku za kazi.

 “Huu ni msiba na msiba ni jambo ambalo halina itikadi na sioni sababu kubwa hasa ya kutuzuia na jambo hili, huu ni utamaduni mpya kabisa hapa kwetu, jambo hili halikubaliki,” alisema Komu.

Alisema polisi ni vema wakafahamu kazi yao kubwa ni kulinda amani na kulinda shughuli hiyo iende kwa amani kwani Ndesamburo alikuwa ni kongozi aliyewahi kuendesha halmashaui hiyo kwa miaka zaidi ya 15 kwa amani.

Aliba Bananga ambaye ni Diwani wa Kata ya Sombetini katika Jiji Arusha, alisema wao hawapo tayari kuondoka katika eneo hilo na kwamba ni vyema Serikali na Jeshi la Polisi wakaacha shughuli hiyo ifanyike kwa amani pasipo umwagaji wa damu.

 Naye Elga Mchovu ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha) Mkoa wa Kilimanjaro, alisema wametumia gharama kubwa kusafisha uwanja huo, lakini anashangazwa na hatua ya Serikali ya kuwazuia licha ya taratibu nyingine kufuatwa.

RPC AZUNGUMZA

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamisi Isah, alikiri polisi kuzuia shughuli hiyo kwa madai kuwa Chadema tayari walikwisha elekezwa kufanya shughuli hiyo Uwanja wa Majengo kwa kuwa kuna nafasi kubwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles