23.2 C
Dar es Salaam
Monday, February 6, 2023

Contact us: [email protected]

UTAFUTWE MWAFAKA WA PROF. LIPUMBA NA MAALIM SEIF

Na THOMAS MONGI,

CHAMA Cha Wananchi (CUF), kilichong’aa na kubeba taswira halisi ya Chama chenye wapenzi tosha kwa pande zote za Muungano yaani, Bara na visiwani hivyo kujinasibu kuwa chama chenye uwakilishi wenye nguvu wa Muungano hasa katika miaka ya 2000 hadi 2010, ni chama kilichokuwa kimebeba hadhi na heshima ya kipekee hapa nchini na hasa kwa jinsi kilivyoweza kushajihisha wanachama na wapenzi wake huku kikisimama kidete kutetea maslahi ya Watanzania kiuchumi na kidemokrasia  nchini.

 Kilionekana kuwa chama makini na mbadala wa chama cha Mapinduzi ( CCM), kwa kuwa viongozi wake walionesha umakini na umahiri wa hali ya juu katika kukiongoza chama hicho kilichokuwa ni chama kikuu cha upinzani wakati huo.

Msimamo thabiti, busara na weledi wa viongozi wa hao Prof. Ibrahim Lipumba na Maalim Seif Sharif Hamad, katika medani ya siasa hapa na nchini, umahiri na hoja zao ziliweza  kuvutia hata jumuiya za kimataifa na zenye kuheshimika sana kuwasilikiza; kwa mfano mnamo mwaka 1996, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Chifu Emeka Anyaoku, alikuja Tanzania katika kuleta maridhiano ya mwafaka wa Zanzibar baina ya CUF  na CCM baada ya kutokea mgogoro wa Kisiasa Zanzibar.

Chifu Anyaoku hakuja kwa sababu zingine ila alikuja kwa kuwa aliweza kushawishika na hoja zilizowasilishwa na CUF, wakiongozwa na na viongozi wao   Mwenyekiti  Prof. Lipumba na Katibu Mkuu wao Maalim Seif Sharif Hamad..

Hakuwa Chifu Anyaouku tu kukutana na CUF, bali Mabalozi wa nchi mbalimbali na taasisi tofauti za ndani na nje ya nchi   walikuwa wanapishana katika ofisi kuu ya CUF iliyopo Buguruni Dar es Salaam, na makao makuu  yaliyopo Mtendeni Zanzibar, kwa kifupi ni kwamba wanadiplomasia na viongozi tofauti waliona kuna sababu  na hoja   nzito toka kwa viongozi hawa.

Hata hivyo mambo si shwari kwa sasa ndani ya chama hiki kilichojizolea sifa kwa ubora wake, umoja na mshimano wa wanachama na wapenzi wake.

Imefika  miezi tisa sasa chama hiki kimekumbwa na mgogoro wa uongozi  baada ya Mwenyekiti wa chama hicho Prof. Lipumba, kuandika barua ya kutengua kung’atuka kwake Uenyekiti wa CUF Taifa ambayo aliiandika Juni 25, 2016, ambapo kabla ya barua hiyo hapo Agosti 5, 2015, Prof. Lipumba alimuandikia barua Katibu Mkuu wake Maalim Seif kuwa amejiuzulu nafasi yake ya uenyekiti wa Taifa wa CUF, kwa madai kwamba hakuwa  tayari kumuunga  mkono aliyekuwa mgombea wa Chadema kwa tiketi ya Ukawa, Edward Lowasa, kipindi alipochukua uamuzi huo ilikuwa zimebaki miezi miwili kabla ya kuanza kwa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Hadi sasa jitihada kadhaa zimefanywa na zinazoendelea kufanywa ili kurudisha amani na umoja ndani ya chama hicho lakini hali  imeendelea kuwa mbaya zaidi kila kukicha. Baadhi ya jitihada hizo ni pamoja na msajili wa vyama vya siasa, ambaye ndiye mlezi wa vyama vya siasa nchini, Jaji Mutungi kuingilia kati mgogoro huo ili kujaribu kuleta suluhu.

Baada ya vikao vya kuleta suluhu na makundi hasimu katika mgogoro huo yaani kundi la Prof. Lipumba na kundi la Maalim Seif,  hali ikawa mbaya zaidi “kama amewasha moto katika nyasi kavu”,  kwani kitendo  chake cha kumtambua Prof. Lipumba, kuwa bado ni Mwenyekiti halali wa CUF Taifa, kwa mujibu wa  kifungu namba 117 cha Katiba ya CUF, kilizidisha mshikemshike ndani ya chama hicho kiasi kwamba sasa mgogoro huo umepelekwa  mahakamani katika kutafuta suluhu au haki kwa kundi la Maalim linaloamini kuwa haki haikutendeka kwa kitendo cha msajili wa vyama kumtambua  Prof. Lipumba kuwa   bado ndiye Mwenyekiti halali wa CUF .

Katika mgogoro huu makundi hasimu ni mawili moja likiwa limejikita upande wa Tanzania Bara ambapo Mwenyekiti Prof. Lipumba, ndiyo anauongoza upande ambapo  anaungwa mkono na wapenzi na wanachama wengi toka Bara, kundi  linaongozwa na Katibu Mkuu Maalim Seif Sharif Hamad, lipo upande wa pili wa Muungano, Tanzania visiwani (Zanzibar),a mbapo naye anaungwa mkono zaidi na Wazanzibar.

Huu ni mpasuko ndani ya chama hiki, mpasuko ambao umewaweka katika mahusiano yasiyo mazuri kati ya viongozi wawili wakuu wa chama hiki ambapo kwa sasa wanapishana kimtazamo na msimamo juu ya mgogoro huo.

Hali ya mgogoro ilivyo

Kimsingi hali ya mgogoro huu ni mbaya, makundi haya mawili yamekuwa yakishambuliana kupitia mitandao ya kijamii na kiasi hata kuwadhalilisha viongozi wao, hali hii haifurahishi wala kuleta afya ndani ya chama hiki. Ushabiki uliokosa hekima na busara katika mgogoro huu umechangia kuendeleza uhasama baina ya wanachama na wapenzi wa chama hiki na kujikuta wakijiona kama maadui wao kwa wao,wengi wao hawazungumzii suluhu bali wanazungumzia kupambana au kuushinda upande hasimu!

Simu 0713-690637

Itaendelea wiki ijayo

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,471FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles