23.2 C
Dar es Salaam
Monday, February 6, 2023

Contact us: [email protected]

KUFELI WATOTO: JAWABU NI KUWAFUKUZA KAZI WALIMU?

NA CHARLES KAYOKA,

SASA Habari ni walimu kufukwa kazi, kushushwa vyeo, au kupewa nafasi ya kujieleza. Kwa nini watoto wamefeli, kwa nini shule zao zimekuwa za mwisho? Kwa nini… kwa nini.. ili mradi sasa lawama zinakwenda kwa walimu wakuu na walimu wanaowasaidia.

Tatizo la kufeli si la leo, si la jana, limekuwa la muda mrefu, likikua siku hadi siku na sasa limekuwa sugu, walimu sasa tumekuwa ndo wasingiziwa na kama inavyoonekana, ndio visababishi vikuu. Majibu rahisi kwa tatizo gumu linalotokana na uzembe wetu!

Nilitaka nianze kwa kuwauliza wakaguzi wa shule za msingi na sekondari! Ratiba za ukaguzi kwa mwaka zikoje? Je, mmezitekeleza zote? Mmekuwa na rasilimali fedha za kutosha kuwawezesha kuzifikia shule zote? Mliandika ripoti nzuri na kuwapatia mrejesho walimu wakuu? Je, vitendea kazi vipo?

Aidha nilitaka mtueleze kutoka kwenye mtima wa nafsi zenu, mlizikuta shule zikiwa na vifaa? Mlikuta uwiano kati ya walimu na wanafunzi wa kiwango sahihi cha wizara? Mlikuta vitabu na vifaa vya kujifunzia na kufundishia vya kutosha? Mlikuta walimu wakiwa na morali  ya juu katika kazi zao?

Waliwaambia kila walicholalamikia kilitekelezwa na Serikali au halmashauri? Je, mishahara yao inatosha kuwafikisha mwisho wa mwezi? Je, madarasa yalikuwa ya kutosha katika kila shule? Madarasa yalikuwa na vifaa vya kumsaidia mwanafunzi na Mwalimu? Kulikuwa na maktaba shuleni? Viwanja vya michezo vilikuwapo?  Mliona walimu wakifundisha kwa mtindo gani (student centred) mwanafunzi kwanza,  ufundishaji shirikishi,  au teacher centred (Mwalimu kwanza)

Maswali yangu ni mengi, likiwapo la kama shule ziliwaambia zilikuwa na fedha za kutosha na Je, Bajeti ilikuwa ikitosha kuwawezesha kujiendesha bila kuwa na sababu ya kulalamika? Na nilitaka kujua kama uwekezaji wa Serikali katika elimu unafanana na mahitaji halisi au kama uwekezaji unakwenda sambamba na malengo tuliyojiwekea katika sera yetu ya elimu? Kama maswali haya na mengine hayana majibu yoyote ya kuridhisha, tunaanzaje kuwalaumu walimu.

Serikali yetu imekuwa ya kwanza kujitoa katika lawama kuhusiana na kushindwa kusimamia elimu vizuri na kuanza kuwalaumu walimu kama vile wao ndio waanzilishi wa matatizo. Nilishaandika mara nyingi kuhusu umuhimu wa kuisimamia elimu kikamilifu. Serikali hii inataka kusifiwa hata isipofaa kusifiwa na ikishindwa kuonyesha matokeo mazuri katika kile walichosifiwa wanaanza kutafuta mchawi na wakati ule wa kusifiana wachache wakijitokeza na kusema jamani huu mwelekeo sio mzuri, wanatishiwa, wanachukiwa, wanafukuzwa kazi, wanaonekana wapinzani.

Nilishaandika kwa JPM kuwa kama ukiwa kiongozi na ukiona wasaidizi wako wanabaki kukushangilia tu, ujue wanafanya hivyo kukufumba macho usione makosa yao katika utendaji. Hayo yalitolewa kama maonyo na Mwanafalsafa mmoja wa Uyunani Ugiriki, Diogenes Laertius.  Na sasa baada ya kushindwa kufanya vizuri katika usimamizi wa elimu walimu wakuu ndio wanaoshinikizwa kukubali kuwa wao ndio chanzo cha kufeli wanafunzi.

Nilishawahi kuandika pia kuwa kunahitajika kufanyika kwa utafiti wa kutosha kuhusu umri wa wanafunzi, matini tunayowapatia na mfumo wa ufundishaji. Umri wa wanafunzi, nikimaanisha (mental age na chronological age), una athari sana katika uwezo wake wa kujifunza. Kama kilichochopo kwenye matini hakifanani na umri kuna uwezekano wa kuwafanya wanafunzi  kushindwa kuelewa, ndio maana nashauri tufanye utafiti wa kisaikolojia juu ya uwezo wa wanafunzi wetu kiakili na hatimaye tuone kama kuna umuhimu wa kurekebisha maudhui ya mitaala yetu na namna ya ufundishaji.

Sisi tulioko hapa Chuo Kikuu tunaona wazi juu ya uwezo mdogo wa wanafunzi katika kufikiri kidhahania (abstract thinking), aidha kwa sababu ya umri mdogo au kwa sababu ya mtindo duni wa ufundishaji katika madaraja ya chini ya elimu ambapo wanafunzi wanalishwa na walimu wao zaidi ya kupewa fursa ya kujifundisha. Lakini tuliposema tunataka kuongeza idadi ya wanafunzi shuleni tulikuwa pia tunajishughulisha na kutambua uwezo wa walimu na shule kumudu ongezeko hilo.

Nasikia kuwa huko serikalini idadi ni muhimu kuliko mafanikio ya ubora, tunapenda takwimu zaidi, tumesajili  wangapi, wamemaliza wangapi, tuna walimu wangapi, tuna vyuo vingapi, tuna shule ngapi…. Lakini hatutaki kujua ubora wa hicho cha kitakwimu…

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,471FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles