27.5 C
Dar es Salaam
Tuesday, February 7, 2023

Contact us: [email protected]

MOTO WA KLABU YA USIKU UNAICHOMA SERIKALI ROMANIA

NA RAS INNO,

USINGETARAJIA kwamba tukio la ajali ya moto katika klabu ya usiku lililoua watu 64 lisababishe moto mkubwa kisiasa ulioizidi nguvu Serikali, baada ya maandamano mfululizo ya kuishinikiza isipitishe muswada wa sheria unaodhamiria kufunika kombe mwanaharamu apite.

Lakini ndivyo ilivyotokea Romania, hatimaye Serikali imenywea kwa waandamanaji na kusitisha mikakati ya kupitisha mabadiliko ya muswada tata wa sheria ili kuepusha nchi kugawanyika na kusababisha maafa zaidi kuliko moto ulioanzisha figisu hilo. Waziri Mkuu Sorin Grindeanu amelazimika kutangaza kusitisha mchakato huo baada ya waandamanaji wanaompinga kuandamana hadi ofisini kwake. Chanzo cha mzozo huo ni kuungua moto Klabu ya Usiku ya Colectiv katika mji mkuu wa taifa hilo Oktoba 30, 2015 ulioua watu kadhaa na kujeruhi wengi, uliotokana na mbwembwe zilizopitiliza za bendi maarufu ya muziki ya Metalcore iliyokuwa ikizindua albamu yake ya ‘Mantras Of War’ yenye kawaida ya kuwasha fashifashi.

Ilizidisha kiwango na kusababisha kulipuka mapambo ya plastiki yaliyoshika moto na kusababisha wengi wazimie kwa kukosa pumzi kwa moshi uliojaa sumu ghafi zilizotengenezewa mapambo hayo. Ilikuwa ajali mbaya ya kihistoria iliyoilazimu Serikali kuwasafirisha baadhi ya majeruhi wakatibiwe katika nchi za Israel, Uholanzi, Ubelgiji, Austria, Uingereza, Norway, Ujerumani na Ufaransa.  Moto huo umewasha moto wa kisiasa unaoichoma Serikali ya Romania iliyoingia madarakani mwezi uliopita kupitia chama cha Kisoshalisti cha ‘Partidul Social Democrat’ (PSD) kutokana na wizara inayosimamia sheria kupendekeza muswada unaosamehe baadhi ya makosa yakiwamo yanayohusisha matumizi mabaya ya madaraka, yaliyosababisha rushwa kufumbia macho tahadhari za usalama katika kumbi za starehe hivyo kusababisha janga lililotokea.

Muswada huo ungepita wahusika kadhaa wakiwamo viongozi waandamizi wa chama hicho wanaotumikia nyadhifa serikalini, wasingechukuliwa hatua zozote na wachache waliohukumiwa vifungo wangeachiwa kwa kisingizio kilichotolewa na Serikali kwamba inataka kukabiliana na mlundikano wa wafungwa magerezani. Unaweza kuwashangaa Waromania kwa kuishikia bango Serikali kutokana na moto uliosababisha maafa kwenye ukumbi wa burudani, lakini mfupa kamili wa sakata zima ni jinsi Serikali ilivyotumia njia za kinyemela kukiuka taratibu ili iwaokoe baadhi ya watendaji wake.

Baada ya kuandaa muswada uliopingwa na wanasheria wakiwamo wa Serikali yenyewe, ikaufanyia marekebisho kwa siri wapinzani wakagundua siri hiyo na kupaza sauti kwamba Serikali inataka kuhalalisha ufisadi na rushwa, ndipo maandamano yaliyoanza kwa idadi ya watu 25,000 yakarindima na mahudhurio kuongezeka kufikia watu laki tatu waliopinga hatua za Serikali mpya kujiosha kinyemela siku chache baada ya kukabidhiwa madaraka. Mbaya zaidi katika kufanyia marekebisho sheria hiyo kwenye kikao cha baraza la mawaziri mapendekezo hayo yanayoelekea kuungwa mkono na Bunge lenye wanachama wengi wa PSD, ajenda hazikuwekwa hadharani kama taratibu zinavyoelekeza hivyo kumlazimu Rais Klaus Iohannis kuhudhuria kikao hicho na kukiendesha kwa mujibu wa kifungu cha 87 cha Katiba ya nchi hiyo.

Waziri Mkuu alizuia vyombo vya habari kuhudhuria na kuripoti kuhusu kikao hicho lakini baada ya kikao Rais alizungumza  na vyombo vya habari, akabainisha kuwa kulikuwa na miswada miwili tofauti kuhusu marekebisho hayo akaanika mbinu zilizotaka kufanyika ili muswada halali ubadilishwe na wenye utata kuwasilishwa bungeni kupitishwa ili kuwaokoa wanasiasa wa PSD. Licha ya Waziri Mkuu kumhakikishia Rais na umma kuwa taratibu zitafuatwa katika kupitisha marekebisho hayo ya sheria, lakini mahakama zote na wananchi walihamanika baada ya Rais kuweka bayana kilichokuwa kinafichwa na kuwasha moto wa maandamano.

Serikali imejirudi kwa muda lakini hilo halitarajiwi kuwaridhisha waandamanaji wanaotaka hatua zaidi zichukuliwe,si kupeleka mapendekezo bungeni bali marekebisho hayo yafutwe kabisa. Lakini Bunge lenye wabunge wengi wa PSD nalo linakanganya mambo zaidi kwani linataka kuitetea Serikali yake kwani Mwenyekiti wao Liviu Dragnea, anashtakiwa kwa ufisadi wa pauni 24,000 wakati Mahakama ya Katiba ikijiandaa kutoa uamuzi kama ilichofanya Serikali ni sahihi au batili, lakini Umoja wa Ulaya nao umeionya vikali Romania kutobinya demokrasia.

Maandamano yaliyozidi kuvutia wengi yalipata taswira mpya Rais alipoungana na waandamanaji Januari 22 na kudai genge la wahuni wachache wanataka kupindisha sheria ili wajilinde, lakini Mwenyekiti wa PSD, Dragnea, alimshutumu Rais na waandamanaji kuwa wanataka kuipindua Serikali ya chama chake wakitumiwa na wapinzani wa vyama vya ‘Uniunea Salvați România’ (USR) yaani ‘Save Romanian Union’ na ‘Partidul Național Liberal’ (PNL) inayomaanisha ‘The National Liberal Party’ kwani viongozi wa vyama hivyo, Nicusor Dan na Raluca Turcan nao walihudhuria maandamano hayo.

Inavyoelekea Serikali ya ‘Social Democratic Party’ PSD imekalia kuti kavu katika mkanganyiko huo kwani tayari mataifa ya Ubelgiji, Canada, Ufaransa, Ujerumani, Uholanzi na Marekani yametoa onyo kali kwa Serikali kuacha mchezo wake mchafu wa kinyemela unaohatarisha si tu mustakabali wa utangamano wa taifa hilo, lakini pia uhusiano wake na Jumuiya ya NATO wakati Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Marekani wanaoiingizia Romania tija ya asilimia 25 kwenye jumla ya pato lake la ndani (GDP) wakitahadharisha kuwa itaathiri uchumi na biashara kwa ujumla.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,885FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles