29.7 C
Dar es Salaam
Friday, October 4, 2024

Contact us: [email protected]

UTAFITI WA TWAWEZA WAIBUA MAZITO


Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM   |

UTAFITI uliofanywa na Taasisi ya Twaweza, umebaini zaidi ya nusu ya Watanzania hawajisikii huru kumkosoa Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu.

Katika utafiti huo ambao unawakilisha Tanzania Bara peke yake, nusu ya wananchi ambao ni sawa na asilimia 47, hawajisikii huru kuwakosoa mawaziri na asilimia 46, wakuu wa mikoa na asilimia 43, wakuu wa wilaya.

Hayo yalisemwa jana Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze, wakati anatoa matokeo ya Twaweza yaliyotokana na utafiti huo.

Eyakuze alisema takwimu za muhtasari huo wa utafiti zinatokana na utafiti wa Sauti za Wananchi ambao huratibiwa na taasisi yao.

Alisema Sauti za Wananchi ni utafiti wenye uwakilishi wa kitaifa unaotumia simu za mikononi.

Eyakuze alisema wananchi wanaendelea kuunga mkono kwa kiwango kikubwa upatikanaji wa taarifa.

“Wananchi 7 kati ya 10 wanasema taarifa zinazomilikiwa na mamlaka za umma ni mali ya umma, ni asilimia 70 juu zaidi kutoka asilimia 60 mwaka 2015.

“Na wananchi 9 kati ya 10 wanasema wananchi wa kawaida wapate taarifa zinazomilikiwa na mamlaka za umma kwa asilimia 86 juu zaidi kutoka asilimia 77 mwaka 2015 na kwa kuwapa wananchi uwezo wa kupata taarifa kunaweza kupunguza rushwa asilimia 86, juu zaidi kutoka asilimia 80 mwaka 2015.

“Pamoja na kuunga mkono kwa kiwango kikubwa upatikanaji wa taarifa, wananchi 9 kati ya 10 hawajawahi kuomba taarifa kutoka katika ofisi za Serikali kwa asilimia 95, mamlaka za maji asilimia 93 , au vituo vya afya asilimia 93,” alisema.

Alisema utafiti unaonyesha wananchi wameendelea kutumia vyanzo vile vile vya habari bila kuwa na mabadiliko makubwa isipokuwa kwa upande wa runinga.

Eyakuze alisema mwaka 2013 runinga ilikuwa ni chanzo kikuu cha taarifa kwa asilimia 7 ya wananchi na mwaka 2017 ni asilimia 23 ya wananchi.

Hata hivyo, alisema imani kwa aina mbalimbali za vyanzo vya habari inashuka; radio kutoka asilimia 80 mwaka 2016 hadi asilimia 64 mwaka 2017, runinga kutoka asilimia 73 mwaka 2016 hadi asilimia 69 mwaka 2017 na maneno ya kuambiwa kutoka asilimia 27 mwaka 2016 hadi asilimia 13 mwaka 2017.

“Idadi kubwa ya wananchi pia wanasema Serikali ipate ridhaa ya mahakama katika kufanya maamuzi yoyote ya kuliadhibu gazeti kwa kutoa taarifa zenye maudhui yasiyofaa kwa asilimia 54.

“Japokuwa wananchi wana mtazamo thabiti kuhusu upatikanaji wa taarifa na uhuru wa kuzungumza, ni wananchi wachache sana wanaofahamu sheria zinazohusiana na masuala ya habari,” alisema.

Kuhusu sheria inayofahamika zaidi katika suala hilo ni Sheria ya Makosa ya Mtandao (2015), ambayo inafahamika na asilimia 10 ya wananchi huku asilimia 4 pekee ya wananchi wakifahamu Sheria ya Huduma za Habari (2016).

Akifafanua kuhusu utafiti huo, alisema ni uwakilishi wa Tanzania Bara pekee, Zanzibar haihusiki.

Takwimu za muhtasari huo zilikusanywa kutoka kwa wahojiwa 1,519 kutoka awamu ya 25 ya kundi la pili la Sauti za Wananchi, na zilikusanywa kati ya Novemba 7 na Novemba 27 mwaka 2017.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles