27.5 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

KOZI YA UUGUZI, UKUNGA SI YA ‘VILAZA’- BARAZA


Na VERONICA ROMWALD-DAR ES SALAAM    |

SERIKALI imehuisha mtalaa wa kozi ya uuguzi na ukunga nchini kuanzia mwaka ujao wa masomo utakaoanza Septemba mwaka huu, lengo ikiwa ni kuwapata wakunga na wauguzi walio bora katika utaaluma.

Hayo yalielezwa Dar es Salaam jana na Msajili wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania, Lena Mfalila, kwenye semina ya siku moja ya kuwajengea uwelewa waandishi wa habari kuhusu Kongamano la Sayansi la Wauguzi na Wakunga linalotarajiwa kufanyika April 4 hadi 7, mwaka huu mkoani Dodoma.

“Kuanzia mwaka ujao wa masomo mtu anayetaka kujiunga chuo chochote nchini kusoma fani hizi anatakiwa awe na ufaulu wa daraja C katika masomo ya msingi ya biolojia, fizikia na kemia,” alisema.

Alisema serikali kwa kushirikiana na baraza hilo imeona vema kuhuisha mtaala wa fani hiyo kuwapata watumishi watakaotoa huduma bora.

“Jamii ilijenga mtazamo kwamba fani hii inastahili watu walioshindwa kusoma fani nyingine, nikiri wazi kwamba soko huria lilitupeleka kwenye matatizo makubwa.

“Ndiyo maana tumeona vema mtaala uhuishwe tuwapate watu ambao kweli wana sifa na wana nia ya kufanya kazi tofauti na ilivyokuwa awali,” alisema.

Alisema kwa kuwa fani hiyo inajumuisha sayansi na sanaa hivyo pamoja na ufaulu wa masomo hayo ya msingi, ufaulu wa masomo mengine hususan kiingereza itakuwa nyongeza.

Awali alisema baraza hilo linatekeleza majukumu yake katika sheria ikiwamo kusimamia suala la maadili na kwamba wamekuwa wakichukua hatua kila wanapokuwa wanafikishiwa malalamiko.

“Tayari kuna wauguzi saba ambao wanatumikia adhabu ya vifungo jela katika mahakama mbalimbali nchini baada ya kuthibitika kughushi vyeti vya taaluma.

“Mwaka 2016 tulipokea malalamiko dhidi ya muuguzi mmoja wa Temeke, tulifuatiliwa na tulipomkuta na hatia tulimfungia leseni yake na alikaa mwaka mzima bila kufanya kazi, tulishikilia na vyeti vyake, baada ya kumaliza adhabu yake, tulimrejeshea,” alisema.

Awali, Mkurugenzi wa Idara ya Uuguzi na Ukunga wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Gustav Moyo alisema kazi ya uuguzi na ukunga ni ngumu hata hivyo wahusika wanapaswa kuendelea kutoa huduma kwa kuzingatia maadili ya taaluma.

Alisema pamoja na hayo, bado kuna changamoto ya uhaba wa watumishi wa kada hizo nchini.

“Kazi ya uuguzi na ukunga ni ngumu, kulingana na uwiano wa watanzania milioni 54 tunahitaji kuwa na watumishi wapatao 15,000, hivi sasa wapo 35,000 – 40,000,” alisema.

Kuhusu kongamano hilo, alisema watajadiliana kwa kina jinsi ya kuboresha huduma za uuguzi na ukunga hasa kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi.

Katibu Mkuu wa Chama cha Wauguzi na Wakunga Tanzania, Dk. Sebalda Leshabari alisema vifo vinavyotokana na uzazi vinaepukika kwa wauguzi na wakunga kupata ujuzi wa kutosha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles