27.5 C
Dar es Salaam
Tuesday, February 7, 2023

Contact us: [email protected]

USIMWINGIZE MWANAO KWENYE MIGOGORO YA UHUSIANO

Na CHRISTIAN BWAYA,

KUTOKUELEWANA katika uhusiano wa ndoa ni jambo lisiloepukika. Watu wawili, tena waliokutana ukubwani, wanaweza kutofautiana kwa sababu za msingi.

Hatua madhubuti zisipochukuliwa mapema kuondoa tofauti hizi, ndoa inaweza kukumbwa na mgogoro. Inapofikia hatua hiyo, wanandoa wanaweza kujikuta wakilazimika kuwahusisha watu wengine katika matatizo yao.

Watu hawa wasiohusika hualikwa kwenye mgogoro kwa malengo tofauti. Mosi ni kuwasaidia kutatua mgogoro uliopo. Mmoja wapo anapoomba msaada wa ndugu na jamaa wengine, kwa mfano, analenga kupata msaada wa mawazo yatakayochangia kutatua changamoto zilizojitokeza.

Hata hivyo, si mara zote mwaliko huo wa watu wengine hulenga kutatua matatizo. Wakati mwingine, nia ya kuwaambia wengine huwa ni kutafuta huruma yao. Kwamba anapowaambia watu hali halisi, kimsingi halengi kupata suluhu ya mgogoro unaoendelea ndani ya ndoa bali kutafuta faraja ya kisaikolojia kuwa anaonewa.

Katika mazingira ambayo ndoa iko kwenye mgogoro kwa sababu yoyote ile, ni rahisi kwa wazazi kufikia hatua ya kuwahusisha watoto wao kwenye matatizo yao. Katika makala haya tunaangazia hatari ya kuwaingiza watoto kwenye migogoro ya ndoa.

Awali ya yote, ni vizuri kutambua kuwa changamoto yoyote mnayokumbana nayo kama wanandoa, ni yenu wenyewe. Ni kukosa ukomavu kujaribu kuwaingiza watoto kwenye mgogoro huo kwa namna yoyote. Katika mipaka ya makala haya, mtoto ni mtu anayeendelea kukua kiufahamu na kimwili na anayetegemea msaada wa wazazi akiishi chini ya mamlaka yao.

Kuwaingiza watoto kwenye mgogoro kunaweza kutafsiriwa kama kuwapa watoto taarifa zisizo za lazima kuhusu mgogoro wenu kwa lengo la kuwafanya wajue nani ni mkosaji na yupi hana hatia.

Mfano, baba anapowajulisha watoto kuwa anaachana na mama yao, hiyo haimaanishi kuwa anawaingiza watoto kwenye mgogoro. Lakini anapowapa watoto maelezo ya kina ya kiini na historia ya mgogoro ili kuwafanya waelewe nani amefanya nini kumwonea nani, hapo tunasema, anawaangiza watoto kwenye mgogoro usiowahusu.

Unaweza kuwapa taarifa hizi kwa lengo jema la kuwaelewesha kwa nini mnaachana, lakini akili ya mtoto ikajenga msimamo dhidi ya mzazi mmoja wapo. Hatari kubwa ya kufanya hivi ni kuwafanya watoto wachukue upande.

Hali hii inaweza kuonekana kuwa jambo dogo lakini ikawa na athari kwa maisha ya mtoto.  Kwa mfano, kwa kugundua kosa la mmoja wenu, mtoto anaweza kujenga chuki na kisasi kitakachoathiri uamuzi wake wa ndoa.

Kama tulivyotangulia kusema, wazazi huwaingiza watoto watoto kwenye migogoro yao kwa nia ya kupata uungwaji mkono. Ni namna fulani ya kutafuta faraja kuwa ‘hata kama mwenzangu hanielewi, angalau mwanangu yuko na mimi!’ Unapofanya hivyo unambebesha mtoto mambo mazito yatakayosumbua nafsi yake kwa muda mrefu.

Inashauriwa kuwatenganisha watoto na matatizo yenu ya ndoa. Hakuna sababu ya kuwapa watoto taarifa zitakazowafanya wamlaumu mmoja wenu hata kama ni kweli. Hata katika mazingira ambayo mgogoro hauwezi kufichika tena, mathalani kulazimika kuachana, jitahidi kuwa kama dodoki linalonyonya hasira, chuki, kukata tamaa, kisasi na hisia hasi zinazotokana na mgogoro.

Mstahi mwenzako hata kama ndiye aliyesababisha hayo yote. Ikiwa unahitaji mtu wa kukusikiliza, kukuelewa, kukutetea, mtafute. Lia, kasirika, omboleza ukiwa faraghani. Lakini unapokuwa na mwanao, jitahidi kuwa mtu mwenye uwezo wa kumstahi mwenzako. Utamsaidia mwanao.

Mwandishi ni Mhadhiri wa Saikolojia Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge. Blogu: http://bwaya.blogspot.com, 0754870815.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,885FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles