26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

UMUHIMU WA MAZOEZI YA KUNYOOSHA, KULAINISHA VIUNGO

Dk. Fredirick L Mashili, MD,PhD.

KUNA aina kuu tatu za mazoezi. Mojawapo kati ya hizo ni mazoezi ya kunyoosha na kulainisha viungo au kwa lugha ya Kiingereza flexibility exercises. Mazoezi ya kunyoosha na kulainisha viungo yanahusisha mazoezi ya yoga na yale ya kunyoosha viungo na misuli au stretch ups. Kutokana na mabadiliko ya mitindo ya maisha, mazoezi ya aina hii yamekuwa muhimu kiasi cha kutakiwa kufanyika kila siku, na wakati mwingine zaidi ya mara moja kwa siku.

Zifuatazo ni sababu kubwa nne zinazofanya aina hii ya mazoezi kuhitajika mara kwa mara.

Kuzuia na kutibu maumivu sugu ya mgongo

Ziko sababu nyingi zinazoweza kusababisha maumivu sugu ya mgongo. Licha ya uzito uliokithiri kuchangia katika tatizo hili, tafiti zinaonyesha kwamba kuketi kwa muda mrefu kunaweza kusababisha tatizo la maumivu sugu ya mgongo. Watu wanaoketi zaidi ya saa nne mfululizo wanauwezekano mkubwa wa kupata tatizo hili.

Maumivu ya mgongo yanayosababishwa na kuketi kwa muda mrefu husababishwa na kukakamaa kwa misuli ya mgongo kutokana na kuwa katika mkao mmoja kwa muda mrefu. Wakati mwingine husababishwa na pingili za mgongo kutoka kidogo katika nafasi zinapotakiwa kuwapo.

Kuzuia tatizo hili, simama na ujinyooshe (stretching) kila baada ya kukaa kwa takribani saa moja. Unaweza pia kusimama na kutembea kidogo kasha ukarudi tena kuendelea na kazi. Kujinyoosha ni mfano mzuri wa flexibility exercise.

Mazoezi maalumu ya kunyoosha na kulainisha misuli ya mgongo hutumika pia kutibu tatizo hili. Wakati mwingine ni muhimu kufanya mazoezi haya kila siku baada ya kazi.

Kuzuia na kutibu maumivu ya viungo kama magoti

Maumivu na matatizo ya viungo/maungio kama vile magoti, nyonga, mabega na kiwiko au arthritis kwa lugha ya kitaalamu, mara nyingi huweza kuzuiwa au kutibiwa kwa kufanya mazoezi ya kunyoosha na kulanisha viungo hivyo (flexibility exercises). Yako mazoezi tofauti kutokana na aina ya kiungo/kiungio na lengo kuu la zoezi hilo. Mazoezi haya pia husaidia kulainisha misuli iliyokakamaa, ambayo pia huchangia katika maumivu ya viungio.

Onana na mtaalamu akupe maelekezo ya nini kinatakiwa kufanyika ili kuzuia tatizo hili.

Kuzuia na kutibu maumivu sugu ya shingo

Kulala vibaya au kutumia mto usio kuwa na ubora kunaweza kusababisha maumivu sugu ya shingo au mgongo. Mara nyingi maumivu yanayotokana na tatizo hili huongezeka wakati wa asubuhi.

Jenga tabia ya kujinyoosha angalau kwa dakika tano mara tu unapoamka. Kufanya hivi husaidia kuondoa kukakamaa kwa misuli ya shingo na mgongo, pamoja na kulainisha maungio ya pingili za uti wa mgongo. Kukakamaa huku kunaweza kusababishwa na kulala vibaya, kutumia mto na godoro lisilo na ubora au hata kulala katika mlalo wa aina moja kwa muda mrefu.

Kuzuia matatizo ya viungo yatokanayo na umri mkubwa

Kadri umri unavyoongezeka ulaini wa viungo/maungio na misuli katika miili yetu hupungua. Hii husababisha kupungua kwa wigo wa kujongea (range of motion) kitu ambacho huweza kusababisha kuanguka na kuumia mara kwa mara. Kwa kufanya mazoezi ya kunyoosha na kulainisha viungo/maungio tunakuwa tunazuia tatizo hili kutokea au kulichelewesha.

Dk. Mashili ni Mtaalamu wa Fisiolojia ya Mazoezi na Homoni. Pia ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba Muhimbili (MUHAS). Kwa maelezo zaidi unaweza kuwasiliana naye kwa namba 0752255949, baruapepe, [email protected]. Unaweza pia kujifunza zaidi kwa kutembelea mojawapo ya tovuti zake: www.jamiihealthtz.com au www.jamiiactive.org

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles