23.4 C
Dar es Salaam
Friday, May 10, 2024

Contact us: [email protected]

Usajili vyama vipya kusubiri uhakiki

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini imesema usajili wa vyama vipya 18 utafanyika baada ya kumalizika zoezi la uhakiki wa vyama vilivyopo unaotarajiwa kuanza Julai 20,2023.

Naibu Katibu Mkuu CCM Bara, Anamringi Macha, akizungumza wakati wa kikao kazi kilichoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 17,2023 wakati wa kikao kazi na viongozi wa vyama vya siasa, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, amesema lengo ni kubaini iwapo vyama vilivyopo vinakidhi matakwa ya kisheria.

“Hili zoezi (uhakiki) tumeona tulifanye kwanza kabla hatujaingia kwenye usajili wa vyama vipya, ingekuwa kichekesho kwamba tunakimbilia kusajili vipya pengine vipo ambavyo havistahili kupewa tena usajili.

“Kama chama kimepoteza sifa kabisa tunakifutia usajili…tukishamaliza litaunganishwa na zoezi la usajili wa vyama vipya. Tutavitangaza kuruhusu mwenye pingamizi awasilishe mapema,” amesema Jaji Mutungi.

Kuhusu kikao hicho amesema kina lengo la kuvisaidia vyama kujiandaa na zoezi la uhakiki ambalo linawasaidia kujua mapungufu waliyonayo.

“Ofisi ya msajili hatutaki kuwa kama mapolisi kwa vyama vya siasa, tunataka kuchukua jukumu la kuwa walezi wa vyama vya siasa,” amesema.

Aidha amesema wameamua kulipa kipaumbele suala la hesabu za vyama kwa sababu hati chafu zimekuwa zikijirudia mara kwa mara kwenye ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Wakichangia mada zilizowasilishwa na Wakala wa Ufilisi na Udhamini (Rita) na ofisi ya CAG, baadhi ya viongozi wamependekeza taratibu za ukaguzi hesabu za vyama na ulipaji tozo mbalimbali uangaliwe upya.

Mwenyekiti wa Chama cha AFP, Rashid Sudi, amependekeza vyama ambavyo havina ruzuku viwe vinalipa tozo za Rita kila baada ya miaka mitano.

“Shilingi elfu moja kila mwezi kwa mjumbe wa bodi ya wadhamini naomba muiondoe kupunguza mzigo kwa sababu vyama vyetu havina ruzuku…kuwe na utaratibu mtu akifanya vizuri (hati safi) apewe motisha,” amesema Mwenyekiti wa Chama Cha Kijamii (CCK), David Mwaijojele.

Naibu Katibu Mkuu CCM Bara, Anamringi Macha, amesema msajili amefanya vizuri kuandaa mafunzo hayo kwani yanalenga kuhakikisha vyama vinakidhi matakwa ya kisheria ya kuvianzisha.

Meneja Kitengo Cha Ufilisi na Udhamini Rita, Edna Msuya, amesema kila chama kina wajibu wa kusajili bodi za wadhamini na kusisitiza ada zote ni lazima zilipwe.

Mkaguzi Mkuu wa Nje kutoka ofisi ya CAG, Sylivester Kibona, amesema mwaka huu kuna mabadiliko makubwa katika hesabu za vyama na kuviomba vijitahidi zaidi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles