27.4 C
Dar es Salaam
Wednesday, August 17, 2022

Usajili Nida usiwe mateso kwa Watanzania

DESEMBA 31 mwaka jana, ilikuwa ni mwisho wa kusajili laini za simu kwa mfumo wa alama za vidole kwa Watanzania.

Lakini Desemba 27, mwaka jana mkuu wa nchi, Rais Dk. John Magufuli aliongeza siku 20 za usajili huo hadi Januari 20, mwaka huu iwe mwisho na wale ambao watashindwa kusajili simu zao zitazimwa.

Hata hivyo zikiwa zimesalia siku tatu ili kufikia tamati ya usajili huo, kwa mujibu wa takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) hadi sasa laini milioni 22.4 hazijasajiliwa na kufanya kuwa kwenye hatari ya kuzimwa.

Hatua ya kuongezwa kwa muda ilikuwa kutoa nafasi kwa watu walioshindwa kusajili namba zao kwa sababu ya kuugua na wasiokuwa na namba ama vitambulisho vya taifa, waweze kumalizia mchakato huo.

Pamoja na hali hiyo, bado zimekuwa zikiibuliwa changamoto kadhaa kutokana na usajili wa vitambulisho vya taifa, ikiwamo kwa baadhi ya maeneo kama wilayani Arumeru mkoani Arusha mashine kuibwa na wananchi kubaki kukosa huduma kwa wakati hadi sasa.

MTANZANIA tumekuwa tukiripoti mara kwa mara kuhusu msongamano na changamoto zinazojitokeza kwenye usajili wa vitambulisho, kiasi kwamba kuna shaka huenda lengo la usajili likakumbwa na dosari kutokana na changamoto hizo.

Kwa mujibu wa TCRA, hadi kufikia Januari 12 mwaka huu, laini zilizosajiliwa ni 26,170,137 sawa na asilimia 53.8 ya laini 48,648,864 zinazotumika nchini.

Takwimu zinaonyesha hadi Desemba 10 mwaka jana, laini zilizokuwa zinatumika zilikuwa 47,063,603 ambazo zinamilikiwa na watu milioni 21.1.

Licha ya TCRA kutoa tumaini kwa kazi hiyo ya usajili wa simu kuendelea kwa watakaositishiwa huduma, ila bado kuna juhudi za makusudi zinahitajika kuchukuliwa hasa kwa upande wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida).

Hilo nalo linakwenda kudhihirika katika ziara iliyofanywa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola mkoani Ruvuma ambako alipigwa na butwaa na kulazimika kumwondoa madarakani Ofisa wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) Mkoa wa Ruvuma, Seif Mgonja kwa kosa la kutogawa kwa wananchi mamba za utambulisho wa taifa (NIN) 14,493 tangu Desemba 31, 2019, licha ya kuzalishwa na Makao Makuu na kuletewa ofisini kwake mjini Songea.

Pia Lugola alimwondoa madarakani Ofisa wa Nida Wilaya ya Namtumbo, Thobias Nangalaba kwa uzembe wa kutofika katika kikao chake cha viongozi wa mkoa na wilaya, licha ya kupewa taarifa ya kuhudhuria.

Hizi ni sehemu ya changamoto ambazo alikutana nazo Waziri Lugola kuhusu watendaji wa Nida ambao wamekuwa kikwazo kwenye baadhi ya maeneo nchini.

MTANZANIA tunaamini usajili wa laini za simu una lengo jema kwa masilahi ya nchi yetu, lakini bado watendaji wa Nida wanatakiwa kutambua wajibu wao ikiwamo kutoa huduma kwa wakati sambamba na utoaji wa namba za  NIN.

Ni vema mamlaka zote zinazohusika na kuratibu suala zima la usajili zijipange ili kuwe na mfumo ambao hautokuwa na kero na mateso kwa wananchi ambao wengine sasa hulazimika kuamka usiku mkubwa kuwahi foleni na mwisho hujikuta wakikwama kwa kuambiwa Nida ina idadi maalumu ya kuhudumia watu kwa siku.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,903FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles