Maisha ya Rugemalira Segerea

0
1577

Kulwa Mzee -Dar es salaam

BAADHI ya vijana waliokuwa mahabusu katika Gereza la Segerea, wamemtaja Mkurugenzi wa Kampuni ya VIP Engineering and Marketing Ltd na mmiliki mwenza wa zamani wa Kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), James Rugemalira, kuwa ni mahabusu mwenye nidhamu, huruma anayesaidia wenzake wenye kesi.

Hayo yalibainishwa jana Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakati vijana hao walipofika kufuatilia kesi hiyo iliyokuwa ikitajwa mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Vicky Mwaikambo kwa sababu Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi anayesikiliza kesi hiyo yuko likizo.

Wakiwa nje ya mahakama baada ya kesi hiyo kuahirishwa vijana hao ambao hawataki majina yao yaandikwe, walizungumzia maisha ya Rugemalira akiwa gerezani.

Mmoja alidai; “mzee ni msikivu na ana huruma sana, anasoma sana vitabu, aliniambia nikitoka gerezani nikasome kwa sababu mimi bado mdogo, sio mimi peke yangu, anahurumia watu wengi sana.

“Mzee Rugemalira anaishi gerezani akiwa mwenye nidhamu ya hali ya juu, habishi jambo akiambiwa, ana huruma na afya yake iko vizuri.”

 Alidai kila asubuhi Rugemalira lazima afanye mazoezi.

 Mkuu wa Gereza la Segerea, SSP George Wambura, alipopigiwa simu kuzungumzia taarifa hizo, alisema mahabusu wote wanapoingia gerezani wanakuwa wenye nidhamu na wanatakiwa kufuata taratibu na sheria za magereza.

“Sisi hatuwezi kusema yupi mahabusu bora kuliko mwingine, mahabusu wote wanafuata taratibu za magereza,” alisema Wambura.

Oktoba 10 mwaka jana, Rugemalira aliandika barua kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) akiomba kuachiwa huru ili washirikiane kupata Sh trilioni 37 za Serikali.

Rugemalira aliandika barua Oktoba 4, mwaka jana kwenda kwa DPP na kupokewa Oktoba 5, mwaka huo akiomba aachiwe huru ili aweze kushirikiana na Serikali kupata Sh trilioni 37 kutoka Benki ya Standard Chartered na washirika wake.

Mshtakiwa huyo ameainisha vielelezo kadhaa vinavyoonyesha Benki ya Standard Chartered ilivyohusika katika sakata la IPTL.

Miongoni mwa vielelezo hivyo, ni gharama zilizokuwa zinatozwa na IPTL Dola za Marekani 1.06/ kWh ni za chini kuliko zilizokuwa zinatozwa na Kampuni ya Songas Dola za Marekani 4.31/kWh.

Kielelezo kingine ni barua ya Rugemalira aliyomwandikia Gavana wa Benki Kuu Januari 17 mwaka jana akiomba majina ya watu waliolipa Sh 144,947,669,844.2 zilizokuwa katika Akaunti ya Tegeta Escrow kati ya Julai 5, 2006 na Machi 19 mwaka 2014.

Anadai katika kielelezo hicho kwamba kipindi hicho PAC ililipa Benki Kuu Sh 164,513,630,314.15 na Dola za Marekani 22,198,544.60 na si Sh 309,461,300,158.27 na Dola za Marekani 22,198,544.60 kama ilivyokuwa katika hati ya mashtaka kwenye kesi ya uhujumu uchumi namba 27/2017.

Rugemalira amebainisha kwamba yeye hana ugomvi na Serikali pamoja na kukaa mahabusu kwa kipindi chote kwa sababu anaamini upande wa mashtaka ulidanganywa na Benki ya Standard Chartered pamoja na washirika wake.

“Iwapo nitaondolewa mashtaka yanayonikabili, itaniwezesha kuendelea na kesi nilizozifungua dhidi ya Standard Chartered na washirika wake ambapo nadai kiasi cha Sh trilioni 20 kiasi ambacho kitaiwezesha TRA kukusanya kodi kutoka kwenye hiyo fedha Sh trilioni 6,” alisema.

Rugemalira na mwenzake, mmiliki mwenza wa zamani wa IPTL, Habinder Sethi ambaye ni Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Pan Africa Power Solutions Tanzania Limited (PAP), walifikishwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Juni 19, 2017, wakikabiliwa na mashtaka 12 yakiwamo ya utakatishaji fedha.

Wanadaiwa kutenda makosa hayo katika Jiji la Dar es Salaam na nchi za Afrika Kusini, Kenya na India.

Miongoni mwa mashtaka yanayowakabili ni kula njama, kujihusisha na mtandao wa uhalifu, kughushi na kutoa nyaraka za kughushi.

Pia wanadaiwa kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, kutakatisha fedha na kusababisha hasara ya Dola za Marekani 22,198,544.60 na Sh bilioni 309.

Washtakiwa hao wanadaiwa kati ya Oktoba 18, 2011 na Machi 19, 2014 wakiwa Dar es Salaam walikula njama ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu katika nchi za Afrika Kusini, Kenya na India.

Katika shtaka la kujihusisha na mtandao, washtakiwa hao wanadaiwa kati ya Oktoba 18, 2011 na Machi 19, 2014 jijini Dar es Salaam, wakiwa si watumishi wa umma  walitekeleza mtandao wa uhalifu kwa lengo la kujipatia faida.

 Sethi anadaiwa Oktoba 10, 2011 katika Mtaa wa Ohio jijini Dar es Salaam, akiwa na nia ya ulaghai alighushi fomu namba 14 ya usajili wa kampuni na kuonyesha yeye ni Mtanzania anayeishi kiwanja namba 887 Mtaa wa Mrikau Masaki wakati akijua ni uongo.

Kesi hiyo ilitajwa jana, upelelezi haujakamilika na hakuna maelezo yoyote kutoka upande wa mashtaka kuhusiana na barua walizoandika kwa DPP, kesi itatajwa tena Januari 30.

Hata hivyo mshtakiwa Rugemalira hakuweza kufika mahakamani kwa kuwa anaumwa, aliyefika ni Sethi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here