25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Upepo mkali wazamisha kivuko Kilombero

kivuko*40 wahofiwa kufariki dunia

Na Ramadhan Libenanga, Morogoro

ZAIDI ya watu 40 wanahofiwa kufa maji katika Mto  Kilombero baada ya kivuko walichokuwa wamepanda kuzama maji juzi saa mbili usiku.

Akizungumza na MTANZANIA jana, mmoja wa  wahanga wa ajali hiyo aliyejitambulisha kwa jina la  Shahib Msinduka, alisema kivuko hicho kilizama baada  ya kuzidiwa nguvu na maji yaliyokuwa yakitoka upande  wa kushoto kwao na hivyo kukizidi nguvu.

Hata hivyo mmoja wa mashuhuda wa ajali hiyo, Yahaya Masele ambaye alikuwa upande wa pili wa Wilaya ya Kilombero akisubiri kivuko hicho, alidai kuwa kilikuwa na watu takribani 50 au 60 pamoja na magari matatu.

“Kwenye kivuko hicho kulikuwa na gari tatu ambazo ni Isuzu Fuso lililobeba mpunga ,Toyota Land Cruiser pick  up mali ya Kampuni ya Mitiki na Land Cruiser Station Wagon mali ya Benki ya CRDB ambazo zote zimezama katika mto huo,“ alisema shuhuda huyo.

Mashuhuda wengine walidai kuwa watu 15 waliokolewa na wengine sita walijiokoa wenyewe.

Walisema kuwa idadi kamili ya watu waliokuwamo  kwenye kivuko hicho bado haijajulikana rasmi licha ya watu wengine kudai kuwa walikuwa zaidi ya watu 50.

Mkuu wa Wilaya ya Kilombero ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya hiyo, Reff Gembe, alisema hadi sasa ni watu watatu waliofariki dunia ambao ni wale waliokuwa kwenye magari.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, waliothibitika kufariki dunia hadi sasa ni Meneja mikopo wa benki ya CRDB  Tawi la Kilombero pamoja na vijana wawili waliokuwa  kwenye Fuso ambao ndugu zao walifika na kuulizia  kukosekana kwao.

Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa Kamati ya Ulinzi  na Usalama ya Wilaya kwa kushirikiana na kampuni ya  Wachina wanaojenga daraja katika mto huo, wanajaribu kutafuta njia ya kuyaopoa magari hayo  matatu yaliyozama ili kuona kama kutakuwa na miili  ya  watu wengine.

“Kwa  mujibu wa wafanyakazi, nimeambiwa  kuwa  kivuko hicho kilikuwa na watu kama 30 -35, lakini  mpaka sasa kwa mujibu wa taarifa tumeambiwa kuna  tofauti ya watu watatu ambao hawajaonekana,“ alisema mkuu huyo wa wilaya.

Aidha mkuu huyo alisema  kuwa anaomba wananchi  kuwa watulivu wakati juhudi mbalimbali zinafanyika kutoa magari yaliyozama ili kupata jibu sahihi la idadi ya watu waliopoteza maisha katika ajali hiyo.

Tukio hilo la kuzama kwa kivuko hicho ni la pili katika   mto huo ambapo mwaka 2002 kilizama na kusababisha  watu zaidi ya 30 kupoteza maisha.

Aidha licha ya taarifa hiyo ya mkuu wa wilaya, kuna taarifa ambazo hazikuthibitishwa zinazodai kuwa waliofariki kutokana na ajali hiyo ya kivuko inaweza kufikia 40. kwani kwa kawaida kivuko hicho huvusha wastani wa watu 50
hadi 60 kwa safari moja.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles