27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Ukawa watoka bungeni

bwege akizomeaNa Khamis Mkotya, Dodoma

WABUNGE wa kambi ya upinzani jana walitoka bungeni, huku ulinzi mkali ukiwa umeimarishwa katika viunga vya Bunge, MTANZANIA linaripoti.

Hatua hiyo ilitokea baada ya kipindi cha maswali na majibu pamoja na maswali kwa Waziri Mkuu alichokiongoza Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson.

Wabunge hao wa kambi ya upinzani inayoundwa na wabunge wengi kutoka vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), walitoka nje ya ukumbi wa Bunge baada ya kutaka mwongozo wa mambo mbalimbali jambo lililokataliwa na Naibu Spika Dk. Tulia.

Hatua hiyo ilikuja mara baada ya Dk. Tulia kutoa taarifa kuhusu ajali ya kivuko cha Mto Kilombero kilichozama juzi, ambapo Serikali ilitoa kauli juu ya tukio hilo.

Wakati Naibu Spika akitoa maelezo hayo, baadhi ya wabunge wa upinzani walisimama na kuomba mwongozo.

Hata hivyo Dk. Tulia alimpa nafasi Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko kuomba mwongozo wake.

Matiko alitumia kanuni ya 68(7) na 63(1) akidai Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema uongo bungeni alipokuwa akifafanua kuhusu utoaji wa elimu bure.

“Kwanini Waziri Mkuu anatoa maelezo ambayo hana uhakika nayo? Kwa mfano kule jimboni kwangu kule Tarime, wanafunzi wa bweni wanatakiwa wapeleke chakula magunia ya mahindi na mwisho wa siku michango inafikia Sh 500,000, iko wapi dhana ya elimu bure?” alihoji Matiko.

Akijibu mwongozo huo, Dk. Tulia alisema tayari ufafanuzi ulishatolewa ya kuwapo kwa changamoto ya utoaji wa elimu bure.

Hata hivyo, kauli hiyo iliibua mzozo zaidi baada ya wabunge wa upinzani kuinuka na kudai miongozo zaidi.

Mbali na Matiko wengine walioomba mwongozo huo ni Mbunge wa Kilombero, Peter Lijualikali

Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea, Mbunge wa Bunda Mjini, Esther Bulaya na Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara wote wa Chadema.

 

Wabunge hao waliendelea kusimama na kupiga kelele wakiomba mwongozo na baadae kiti kilipoelekeza shughuli nyingine, wabunge wote wa upinzani walisimama na kuondoka wakiongozwa na Kiongozi wa upinzani bungeni, Freeman Mbowe na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo).

 

ULINZI MKALI BUNGENI

MTANZANIA lilishuhudia askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) zaidi ya 15 wakirandaranda katika viwanja vya Bunge, na wengine wakiwa wamesimama na kutanda katika milango yote ya kuingia bungeni.

Kuimarishwa kwa ulinzi huo kumetokana na hali ya juzi, ambapo Bunge lilichafuka wakati wa jioni pale polisi walipoamriwa kuingia ukumbini kuwatoa wabunge wa upinzani waliokuwa wakipinga kauli ya Serikali ya kuzuia matangazo ya moja kwa moja ya vikao vya Bunge kupitia Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC).

 

BULAYA

Mbunge wa Bunda Mjini, Esther Bulaya, alishangazwa na uwepo wa wingi wa polisi bungeni na kusema ni aibu katika karne ya sasa Bunge kuendeshwa kwa mtutu wa bunduki.

“Tumetoka kuonyesha hatukubaliani na uamuzi wa Serikali wa kuzuia matangazao ya Bunge yasiende ‘live’ (moja kwa moja). Wamejipanga kwa wingi wao kukandamiza haki ya wananchi ya kupata habari.

“Sisi tunajua, huu ni mkakati mpana utakaovikumba hadi vyombo vingine, TBC ni mwanzo tu, lakini hili ni tatizo, hapa si tu wananyima haki za wananchi, lakini wanakandamiza uhuru wa vyombo vya habari,” alisema.

 

LIJUALIKALI

Kwa upande wake, Mbunge wa Kilombero, Peter Lijualikali, alisikitishwa na hatua ya Naibu Spika kumnyima nafasi wakati akiomba mwongozo wa kiti.

“Mara baada ya Waziri Mhagama kutoa taarifa ya ajali ya kuzama kwa Kivuko cha Kilombero, nilisimama kuomba mwongozo ili nitoe taarifa nilizokuwa nazo kuhusiana na tatizo hilo.

“Nilipokuwa nikiomba nafasi nilidhani hawanijui, nikasema mimi ndiye Mbunge wa Kilombero kwa ‘attention’ zaidi, lakini bado sikusikilizwa.

“Nilitaka kutoa taarifa kwamba waziri amedanganya, yeye anasema watu 30 wameokolewa, lakini taarifa nilizonazo mimi nimepigiwa simu na wananchi jimboni kwamba kuna watu wamefariki dunia,” alisema.

 

KUBENEA

Naye Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea, alisema: “Kutoka kwetu ni mwendelezo wa hoja ya jana ya kupinga kauli ya Serikali juu ya matangazo ya TBC.

“Lakini hoja yangu ilikuwa kutaka kujua kama ni sahihi katika nchi kama Tanzania inayoheshimu haki za raia kuwanyima wananchi haki ya kupata habari.

“Lakini pia katika vurugu za jana, wapo wabunge wanawake waliporwa hereni na mikufu yao, lakini pia kuna waandishi wa habari walizuiliwa kutimiza majukumu yao, sasa yote haya ni sahihi?” alihoji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles