27.4 C
Dar es Salaam
Monday, October 2, 2023

Contact us: [email protected]

Upendo pekee hautoshi, fanya haya aone unastahili kwake

WENGI wanadhani kwa sababu wanawapenda sana wakina fulani basi nao wana haki ya kupendwa na kusikilizwa na wenzao hao. Kumpenda mwenzako ni suala zuri ila siyo suala lake ni suala lako. Kitu unachotakiwa kufanya ili na yeye akupende na wewe kama unavyompenda ama zaidi.

Siyo kusikilizia tu kiwango cha upendo ulichonacho kwa mwenzako, badala yake ni kufanya mambo na mikakati ya kumfanya mwenzako naye akupenda na akuhitaji kwa kiwango unachotamani.

Kumpenda mwenzako siyo tiketi ya yeye kukupenda ila atakupenda kutokana na unavyotawala akili na hisia zake. Kwa nguvu ya upendo wako anaweza kukuonea huruma na kujali harakati zako kwake ila kujali huko kama hakujashikiliwa na vitendo adimu na vya kumfurahisha katika maisha yake ni sawa na bure.

Mwenzako atakupenda akiona unampa sababu ya kufanya hivyo. Ni jambo la ajabu kutaka mwenzako akupende eti kisa unampenda. Huenda unampenda kwa sababu anakupa raha na msisimko mkubwa katika maisha ila wewe humfanyi hivyo, sasa yeye ana sababu gani makini ya kukupenda.

 Unaweza kupenda na bado usipate heshima na hadhi unayotaka kwa mwenzako kama bado humfanyi akuone mtu bora na makini katika maisha yake.

Heshima ya upendo kiuhalisia haitokani na hisia zako za kumpenda ila ni kutokana na namna unavyomtendea na namna unavyomfanya akutafsiri.

 Jiulize, mwenzako anakutafsiri vipi? Anakuona ni mume/mke tu  au anakuona ni mshirika muhimu na wa kipekee katika maisha yake?

Kama mwenzako anakuona ni mume/mke tu na sio kukuona kama mtu wa kipekee katika maisha yake, hasiti kukufanyia vituko na hata ukienda hatolia sana kwa sababu wanaume/ wanawake wamejaa tele. Ila kama akikutafsiri kama mtu makini, wa kipekee mwenye kustahili kutunzwa kutokana na kauli na matendo yake, atakuheshimu, kukujali na kukusikiliza kwa sababu watu makini na wa kipekee huwa hawapatikani hovyo.

 Acha kuamini kwamba utapendwa kwa sababu hisia zako zinampenda mwenzako. Tengeneza hali ya kustahili kupendwa kutokana na matendo na kauli zako. Ukiweza kuteka fikra za mwenzako, jua utaweza pia kucheza na hisia zake kitu kitakachokupa mamlaka makubwa katika maisha yake.

 Jiulize, unafanya matendo gani ya kumfanya mwenzako akukumbuke na afurahi kuwa karibu na wewe? Jiulize, ukiwa mbali, mambo gani mwenzako atayamisi na kujiona hayuko kamili bila kuyapata? Hata akiamua kuwa na mtu mwingine, ni vitu gani ni maalum kwake hawezi kuvipata mahali pengine?

 Ni jukumu la kila mmoja kutengeneza thamani na ubora wake katika uhusiano. Watu wanatakiwa kuelewa, suala la kuendelea kupendwa na wenzao linahitaji wawe makini, wabunifu na wenye kustahili.

 Hakuna anayeweza kupendwa kwa kiwango stahili kwa kulalamika tu ama kulia kutwa nzima. Jiulize, matendo yako ni kwa namna gani yanagusa hisia za mwenzako? Unachangia kwa kiwango gani furaha ya mwenzako?

Kama upo upo tu, kama humpi furaha wala amani stahili, kama siyo mbunifu wala mjanja kwa mwenzako kiasi cha kushindwa kumfanya asiwe na hamu na wewe hata kupelekea kukuchoka mapema, utalia sana na kuona huna bahati katika maisha.

 Kulia kwamba unampenda ila yeye hakupendi haimfanyi akupende. Watu wanapendwa kutokana na namna wanavyoweza kuwafanya wenzao kuwaona bora, wa kipekee na maalum katika maisha. Hata kama hisia zako zinampenda mwenzako kwa kiwango kikubwa kwa namna gani ila kama husisimui hisia zake na kutawala fikra zake, usitegemee sana kupendwa.

Mapenzi ni mchezo cha kufurahishana na kupeana sababu za kupendana. Kama huwezi kumpa sababu zahihi mwenzako za kukupenda, hata kama unampenda basi fahamu hawezi kukupenda.

Instagram:ramadhan.masenga

Mwandishi wa makala hii ni mtaalamu mbobezi wa masuala ya ushauri wa uhusiano, maisha na utulivu wa hisia( Psychoanalyst)

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles