23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Acha kulalamikia changamoto za maisha, pambana

ATHUMANI MOHAMED

KATIKA maisha hutakiwi kabisa kuchukia changamoto, matatizo au kero zozote unazokutana nazo. Kumbuka maisha ni safari. Kila kinachopita katika maisha yako ufahamu kwamba kinapita kwa sababu na hakitajirudia tena.

Mfano elimu ya msingi ni mara moja tu. Ukishahitimu  usitegemee tena kurudi shule ya msingi na kuanza kujifunza tebo. Kichekesho ni pale, mtu mzima ambaye tayari ana familia yake, anataka kufanya mambo ya watoto wa shule ya msingi.

Ndugu zangu, tusisahau kuwa hatua ni mara moja tu. Hakuna kujirudia. Kadhalika katika matatizo au kero, ujue kuwa zinakuja kwa ajili ya kukuweka sawa kukabiliana nazo. Usiwe mtu wa kulalamika tu, labda mwenye nyumba anakusumbua, wapangaji wenzako siyo wastaarabu nk.

Itasaidia nini kulalama kuwa maisha ya nyumba za kupanga ni kero wakati hayajakupa changamoto? Hapo ndipo watu wengi wanapokosea.

Wengine ni mabingwa wa kulalamika kuwa wanafanya kazi ngumu sana, wanaishi mitaa wasiyoipenda nk. Jambo la msingi unalopaswa kujiuliza ni je, umechukua hatua gani kukabiliana na hayo unayolalamikia?

TUNAJIFUNZA NINI?

Wafanyabiashara wakubwa wote waliofanikiwa, walitumia mbinu ya kutafuta suluhu la matatizo ya watu ili kujitajirisha. Maana yake ni nini? Ukienda mahali ukakuta wana shida ya maji, unapaswa kuchimba visima vingi na uuze maji.

Watu watakushukuru kwa uamuzi wako huo, lakini wakati huohuo utakuwa unatajirika. Ilivyo ni kwamba, ikiwa unaona unakereka na nyumba za kupanga, unatakiwa kuweka mpango wa kujenga nyumba yako.

Siyo lazima uwe na fedha cash. Weka mipango kwanza. Unaambiwa usiogope ukubwa wa samaki, uliza bei yake. Kama hujawahi kuuliza hata bei ya kiwanja, kamwe hutajua. Achana na watu wanaowakatisha wenzao tamaa, kwamba kujenga ni gharama kubwa nk…

Jiulize, kama ni gharama kubwa, walioweza waliwezaje wewe ushindwe? Wao ni kina nani na wewe ni nani hadi ushindwe? Utakuja kukuta siku unauliza bei, unagundua kuwa unaweza kujipanga taratibu hata kwa miaka mitatu kisha ukanunua kiwanja chako.

Kumbuka kununua kiwanja ni mwanzo wa kuelekea kujenga. Ukishakuwa na kiwanja, hutakuwa na haja tena ya kuulizia kiwanja bali sasa utaanza kuuliza bei ya mchanga kwa ajili ya kufyatua matofali. Ni hatua kwa hatua.

Ni sawa na mtu anayelalamika kuwa hapendi kuishi uswahilini, sawa… unafanya nini ili uweze kuondoka kwenye maisha ya uswahilini na kuhamia kwenye maeneo ya wenye nazo?

Unakereka na daladala sawa lakini je, umewahi kufikiria kuanza kuhifadhi fedha kwa ajili ya kununua gari lako mwenyewe? Ni suala la wewe mwenyewe kuamua na kuchukua hatua.

HESHIMU HATUA ZAKO  

Usijidharau, kila hatua ina maana yake. Kama unaishi chumba kimoja na umepanga, unalipa labda 30,000 au 50,000, siyo tatizo kabisa kufikiria kujenga chumba kimoja kama unachoishi sasa ukiwa umepanga.

Kadhalika ni afadhali ufikirie kununua hata baiskeli ambayo itakurahisishia usafiri kuliko kuendelea kutumia daladala ambayo kila kituo unalipia 400 (hii inategemea na eneo unaloishi).

Jambo kubwa la msingi ambalo nataka kuhitimisha nalo mada hii ni kwamba, usiishie kunung’unika, badala yake pambana, tafuta majibu ya matatizo yanayokusumbua.

Wako katika mafanikio, naitwa Athumani Mohamed, wasalaam. Hadi wiki ijayo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles