29.2 C
Dar es Salaam
Friday, September 30, 2022

UONGOZI DAR ES SALAAM UJITAFAKARI MAPATO KUPOROMOKA

TANGU Serikali ya awamu ya tano ilipoingia madarakani mwaka 2015, moja ya sera yake ni ukusanyaji wa kodi kwa maendeleo ya nchi.

Imekuwa ikisisitiza kila mtu kulipa kodi kwa sababu kufanya hivyo ni mwanzo wa Serikali kupata fedha ambazo zitaekelezwa katika miradi mbalimbali ya kijamii.

Kutokana na hali hiyo, Rais Dk. John Magufuli amekuwa akiwahimiza wananchi kudai risiti wanaponunua na kuuza bidhaa.

Kumekuwa na mwitikio mkubwa katika hilo tofauti na mwanzoni jambo hilo lilionekana kuwa gumu.

Hali hiyo, ndiyo imesababisha Serikali kuagiza wafanyabiashara wote kutumia mashine za kielektroniki za kutolea risiti – EFDs ambazo zimeidhinishwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Akiapisha viongozi mbalimbali Ikulu Dar es Salaam jana, pamoja na mambo mengine, Rais Magufuli alisema makusanyao ya mapato yameshuka vibaya katika mkoa huo.

Akionekana kutofurahishwa na hali hiyo, alisema anashangaa kuona katika Mkoa wa Dar es Salaam ‘rais wake yupo’, wakuu wa wilaya na mameya wapo, lakini makusanyo yamekuwa yakipomoroka kwa kasi kubwa.

Dar es Salaam ni jiji kongwe lenye kila aina ya shughuli za uzalishaji, kuanzia mama lishe hadi viwanda vikubwa vinavyotegemewa kwa uhai wa taifa hili.

Ni ukweli usiopingika kwamba Dar es Salaam kuna vyanzo vingi vya mapato, lakini inakuwaje mapato yashuke?

Inawezekana uongozi wa mkoa huo umeshindwa kubuni mikakati mipya ya ukusanyaji mapato.

Kwamba hakuna mikakati madhubuti iliyopangwa kuanzia kwenye vikao vya madiwani ambavyo tunaamini ndiyo chimbuko la vyanzo vya mapato.

Mbali ya madiwani na mameya wao kushindwa kutimiza wajibu, inawezekana viongozi wa Serikali nao ambao wamekabidhiwa jukumu hili wamebweteka, kiasi cha kuwafanya waone kila kitu ni cha kawaida.

Haiingii akilini Dar es Salaam izidiwe na Jiji la Dodoma ambalo hata halina uhai wa mwaka mmoja, lakini limeweza kukusanya fedha nyingi kiasi, huku likiwa na vyanzo kidogo vya mapato.

Hata kama wapo wafanyabiashara waliofunga biashara zao kutokana na matatizo mbalimbali ya kodi, bado hakiwezi kuwa chanzo kikuu cha mapato kuporomoka Dar es Salaam.

Tunapatwa na wasiwasi kwamba uongozi wa mkoa huu kwa namna moja au nyingine umeshindwa kubuni mikakati mipya ya kukusanya mapato.

Tunakubaliana na Rais Magufuli kuwa kama mkuu wa mkoa ambaye amepewa mamlaka yote hakusanyi mapato, hapa kuna jambo zito la kujiuliza kama kweli anatimiza wajibu wake sawasawa.

Sisi MTANZANIA, tunasema Jiji la Dar es Salaam, kiongozi wake ambaye ni ‘rais wa mkoa huo’, lazima akae chini kwa kushirikiana na mamlaka nyingine kutafuta njia mbadala ya ukusanyaji mapato.

Kwa Dar es Salaam, yenye utitiri wa viwanda, hoteli, migahawa na vyanzo vingine vingi vya mapato ambavyo tukivitaja hapa vitajaza ukurasa, ni wazi kuna sehemu ambayo wamejikwaa, wanapaswa kujitafakari upya na haraka zaidi.

Tunaamini Dar es Salaam inaweza kuwa mfano wa majiji mengine katika ukusanyaji mapato.

Tunamalizia kwa kusema Mkoa wa Dar es Salaam kushuka mapato ni aibu, viongozi wake wajitafakari haraka, vikao vya mabaraza ya madiwani lazima vionyeshe uwezo wake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,335FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles