30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Ummy Mwalimu :Vituo vya afya vimeongezeka nchini

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema miaka mitatu ya Rais Samia Suluhu Hassan sekta ya afya imeendelea kuimarika katika maeneo mbalimbali kama miundombinu na kuongezeka kwa vituo vya afya kutoka 8,549 mwaka 2021 hadi kufikia 9,610 Machi 2024.

Akizungumza leo Machi 18 jijini Dar es Salaam kuhudu kuhusu miaka mitatu ya Rais Dk. Samia katika mageuzi ya sekta ya afya, serikali imeweza kufanya maboresho ya miundombinu ya kutolea huduma za afya ikiwa ni pamoja na ujenzi wa majengo mapya, ukarabati na kukamilisha ujenzi wa hospitali mpya katika mikoa mipya mitano.

Amesema maboresho hayo yamegharimu kiasi cha jumla ya Sh trilioni 1.02 na yalifanyika katika maeneo mbalimbali nchini ikiendeleza ujenzi katika hospitali za Rufaa za Mikoa mipya mitano ambazo ni Katavi, Njombe, Songwe, Simiyu na Geita.

“Ongezeko la vituo vya kutoa huduma za afya nchini na maboresho ya miundombinu yaliyofanyika yametuwezesha kusogeza huduma za afya karibu zaidi na wananchi kama tunavyoelekezwa na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 – 2025.

”Hivi sasa asilimia 80 ya wananchi wanapata huduma za afya ndani ya kilometa tano ya maeneo yao wanayoishi lengo ni kufikia asilimia 95 ifikapo mwaka 2030,”amesema Ummy .

Amesema licha ya hospitali hizo kuendelea na ujenzi pia tayari zimeanza kutoa huduma kwa wananchi kwa maeneo husika kwa kupata matibabu.

Amesema katika kuimarisha huduma za uchunguzi wa wagonjwa, Serikali imenunua vifaa tiba vya uchunguzi na matibabu ya wagonjwa vyenye thamani ya sh. bilioni 290.9 ambavyo vinapatikana kuanzia ngazi ya Hospitali ya Taifa hadi hospitali za Rufaa za Mikoa (RRHs) na Halmashauri.

Amesema katika huduma za kipimo cha CT Scan,kwa sasa zinapatikana katika hospitali takribani 27 kati ya 28 za rufaa.

Ummy amesema kwa mwaka 2023, jumla ya wagonjwa 15,386 walipatiwa huduma za kipimo cha CT Scan katika Hospitali za Rufaa za Mikoa ambapo huduma hizo zilikuwa hazitolewi katika hospitali za Rufaa za mikoa hapo awali.

Ameeleza kuwa katika kipindi cha miaka mitatu ya Rais Samia wameweza kupunguza vifo vya wanawake wajawazito kwa asilimia 80 na kuimarisha kwa huduma za uzazi, mama na mtoto.

Amesema maboresho hayo yamefanya kupunguza vifo vya wajawazito vitokanavyo na uzazi kutoka vifo 556 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2016 hadi kufikia vifo 104 kwa kila vizazi hai 100,000 kwa sasa .

”Vifo vya watoto umri chini ya miaka mitano vimepungua kutoka vifo 67 kwa kila vizazi hai 1,000 mwaka 2016 hadi kufikia vifo 43 kwa kila vizazi hai 1,000 mwaka 2022.

”Vifo vya watoto umri chini ya mwaka mmoja vimepungua kutoka vifo 43 kwa kila vizazi hai 1,000 mwaka 2016 hadi kufikia vifo 33 kwa kila vizazi hai 1,000 hadi sasa, huku vifo vya watoto wachanga (wenye umri wa chini ya siku 28) vimepungua kutoka 25 kwa kila vizazi hai 1,000 mwaka 2016 hadi vifo 24 kwa vizazi hai 1,000 hadi sasa,”amesisitiza.

Aidha amesema uwekezaji mkubwa uliofanywa na Rais Dk. Samia katika kuimarisha huduma bingwa na ubingwa bobezi, umewezesha wananchi wengi kupata huduma hizi ndani ya nchi kwa gharama nafuu badala ya kuzitafuta nje ya nchi.

Ummy amesema uwekezaji huo umeweza kuvutia wagonjwa mbalimbali kutoka nje ya nchi na hivyo kuifanya Tanzania kuwa Kituo cha Tiba Utalii kwa ukanda wa nchi za Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika.

Amesema kumekuwa na ongezeko la raia wa kigeni kuja Tanzania kwa ajili ya matibabu ambapo kwa mwaka 2023, idadi ya wagonjwa kutoka nje ya nchi wa Tiba Utalii waliokuja kutibiwa nchini ilikuwa 6,931 ikilinganishwa na wagonjwa 3,957 mwaka 2022 na wagonjwa 75 mwaka 2021.

Ametaja nchi walipotoka wagonjwa hao ni pamoja na nchi za Comoro, Malawi, Burundi, Zambia, Congo DRC, Uganda, Zimbabwe na Kenya.

”Wagonjwa hawa walihudumiwa katika hospitali sita ambazo ni Hospitali ya Taifa Muhimbili, Taasisi ya Saratani ya Ocean road, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Taasisi ya Mifupa (MOI) na hospitali binafsi za Agakhan na Saifee,”amesema.

Amesisitiza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya imejipanga kuendelea kutoa huduma za ubingwa na ubingwa bobezi karibu zaidi na wananchi.

”Kupitia mafunzo elekezi kutoka kwa wataalam bingwa (Mentorship Program) kutasaidia kuleta chachu ya mabadiliko ya utoaji huduma za afya ili kuweza hudumia vyema wananchi katika kupata huduma bora za kibingwa,”amesema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles