28.2 C
Dar es Salaam
Monday, February 6, 2023

Contact us: [email protected]

Ulimi wamponza Magufuli

john-magufuliNA EVANS MAGEGE

KITENDO cha Rais John Magufuli kumuahidi Jaji Mkuu wa Tanzania, Chande Othman, Sh bilioni 250 ili ashughulikie kesi za ufisadi ambazo zinatarajiwa kuipatia Serikali Sh trilioni moja, kimeibua hisia tofauti miongoni mwa wanajamii na hasa jamii ya wasomi wa sheria.

Rais Magufuli alitoa ahadi hiyo juzi kwenye kilele cha Wiki ya Sheria, akitanabahisha kwamba mbali na kiasi hicho, pia alimuahidi Jaji Mkuu kuwa ili kuiwezesha Mahakama kufanya kazi zake vizuri ataipatia idara hiyo Sh bilioni 250, fedha ambazo zitapatikana katika kesi hizo na nyingine Sh bilioni 750 zitumike kununulia ndege za Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).

Baadhi ya wasomi wa sheria waliozungumza na gazeti hili wamesema ahadi ya fedha aliyoitoa Rais Magufuli imejenga mazingira ya Serikali kuingilia uhuru wa Mahakama.

Wapo ambao wamekwenda mbali na kusema kauli hiyo ni ya kuushawishi mhimili huo kuhakikisha maslahi ya Serikali yanatimizwa kuliko kutenda haki ili kujipatia kitita hicho.

Mmoja wa watu wenye mtazamo huo ni Wakili wa Kujitegemea ambaye pia ni Mkurugenzi wa Sheria na Haki za Binadamu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Peter Kibatala, ambaye alizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu jana akisema Rais Magufuli aliteleza, tena kuelekea kuanguka kutokana na kauli hiyo.

Alisema anafahamu moyo wa dhati wa Rais Magufuli wa kutaka mambo yaende haraka ili hukumu zipatikane, lakini Mahakama nayo ina mazingira yake ya kujihakikishia ushahidi wa kutosha ili haki ipatikane.

“Hapa Rais aliteleza tu, nadhani hata washauri wake watakuwa wameliona hili, ni kweli hata mimi nafahamu umuhimu wa haki kupatikana mapema, si unajua haki ikichelewa huwa inakufa…

“Rais ana moyo wa dhati wa kuitaka Mahakama iweke uharaka wa kutoa haki kuliko kutumia muda mrefu kutoa hukumu, hata hivyo, kwa picha iliyowazi, kauli aliyoitoa moja kwa moja inaipa mwelekeo Mahakama kuhukumu kwa kuangalia kuna fedha imeahidiwa na Serikali,” alisema Kibatala.

Alisema kitendo cha Rais kuiahidi Mahakama Sh bilioni  250 kwa ajili ya kuendesha shughuli zake kina tafsiri ya rushwa, kwamba hukumu itatolewa kwa kuangalia maslahi ya kupata fedha zilizoahidiwa na si haki.

“Hii ni sawa na mtu amteke nyara mtoto wako na akuahidi kuwa ili umpate lazima utoe milioni tano, kwa muktadha wa kauli ya Rais, Mahakama imetekwa, kama Rais anasema Serikali inatarajia kupata Sh trilioni moja katika kesi hiyo na fedha hizo zitakapopatikana Mahakama ipatiwe Sh bilioni 250, kunamaanisha hapa lazima Serikali ishinde kesi ili mahakama inufaike, hapa kweli kutakuwa na haki?” alihoji Kibatala.

Kwa upande wake Makamu wa  Rais wa Chama Cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Flaviana Charles alisema anaunga mkono jitihada za rais kuhakikisha mambo yanakwenda vizuri na kwa wakati katika idara mbalimbali za serikali.

Hata hivyo alitetea ahadi hiyo ya Rais kwa Mahakama akisema alikuwa anajibu changamoto zinazoukumba mhimili huo ambazo ziliainishwa na Jaji Mkuu na kwamba kauli yake hiyo haimaanishi kwamba kuna jambo litakalofanyika juu ya sheria.

“Mahakama itabaki kama chombo huru cha kusimamia haki na sheria za nchi” alisema Flaviana.

Wakati Makamu huyo wa Rais wa TLS akisema hayo, mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo) Zitto Kabwe aliandika kupitia ukurasa wake wa Facebook akieleza kufurahishwa na kushtushwa na hotuba hiyo ya Rais Magufuli aliyoitoa wakati wa maadhimisho ya siku ya sheria juzi.

Zitto alisema Rais anaonekana kama bado yuko kwenye kampeni  kwamba hotuba yake inaonekana ni kiongozi anayeguswa na mwenendo wa mambo lakini imekosa misingi ya uongozi.

Kwa mujibu wa Zitto Majaji hawatakiwi kufanya kazi kwa uwoga wala upendeleo huku akihoji itakuwaje endapo Jaji Mkuu na majaji wengine wakaendesha kesi zote za trilioni moja ndani ya siku tano pasipokuendana na matakwa ya serikali?

Zitto alisema pamoja na kwamba hotuba hiyo imependwa na baadhi lakini ilikuwa ya vitisho na ya kisiasa zaidi katika mambo ya kitaalamu na haikuwa na hadhi ya kutolewa na mtu anayeitwa Rais.

Mwanasiasa huyo alikwenda mbali zaidi na kusema hotuba hiyo ya Magufuli pia imeua uchunguzi wa sakata la Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) .

Kwa upande wake, Wakili Nakazael Tenga, alipozungumza kwa njia ya simu na gazeti hili alisema Rais Magufuli hakupaswa kutanguliza zawadi ya fedha katika hukumu hiyo ya kesi ya ufisadi.

Alisema kauli hiyo ya Rais inatoa tafsiri ya kuipa ushawishi Mahakama kuangalia fedha iliyoahidiwa kuliko usimamizi wa haki ya mtu.

“Huyu ni mtuhumiwa tu, bado hajakutwa na hatia, halafu inatokea ahadi ya fedha dhidi yake, ina maana lazima haki yake haitapatikana…Mahakama ni chombo huru, lazima kiheshimiwe katika utendaji kazi wake,” alisema Wakili Tenga.

Mwingine aliyezungumza na gazeti hili kwa njia ya simu ni Wakili Mussa Mwapongo, aliyesema Rais Magufuli anasafisha nyumba yake, hivyo anataka mambo yaende haraka ili nyumba yake aiendeshe katika hali ya usafi.

“Tumuache asafishe nyumba yake maana inaonekana watu walijisahau sana katika utawala uliopita,” alisema Mwapongo.

Kwa mujibu wa maelezo ya Rais Magufuli, kuna kesi 442 za kukwepa kodi ambazo zikiamuliwa Serikali itapata Sh trilioni moja, ambayo ingeweza kununua ndege zaidi ya sita.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,471FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles