27.1 C
Dar es Salaam
Wednesday, June 12, 2024

Contact us: [email protected]

Mramba, Yona kudeki hospitali

Gray-Mgonja-Daniel-Yona-Basil-Mramba-1024x7681-620x311*Watafanya kazi hiyo kwa saa nne kila siku

*Ni baada ya kuhukumiwa kifungo cha nje

Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam

ALIYEKUWA Waziri wa Fedha, Basil Mramba na Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona, ambao walikuwa wakitumikia kifungo cha miaka miwili jela, sasa wamehukumiwa kifungo cha nje kitakachoambatana na kufanya usafi katika Hospitali ya Palestina, Sinza, Jijini Dar es Salaam.

Mawaziri hao walibadilishiwa adhabu ya jela na kupewa adhabu ya kutumikia kifungo cha nje jana na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya kukamilika kwa mchakato wa kufikia hatua hiyo.

Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Cyprian Mkeha, alisema sheria ya huduma kwa jamii namba 6 kifungu namba 3(1) ya mwaka 2002 inasema mtu yeyote anayetiwa hatiani kwa kosa ambalo adhabu yake ni miaka mitatu kushuka chini mahakama inaweza kumpa adhabu ya kutumikia jamii.

Mramba na Yona baada ya rufaa walibakiwa na adhabu ya miaka miwili, walitiwa hatiani kwa kutumia madaraka vibaya ambapo walitakiwa kumaliza kifungo Novemba 2016.

Hata hivyo, jana Hakimu huyo alisema Magereza walifikisha barua mahakamani hapo Desemba 5, mwaka jana yenye kumbukumbu namba 151/DAR/3/11/223, wakipendekeza kifungo cha nje kwa mawaziri hao.

Hakimu Mkeha alisema baada ya kuipokea barua hiyo mahakama iliamuru watu wa huduma za jamii kuchunguza kama wanastahili kupewa adhabu hiyo na kwamba walifanya hivyo na kurudisha ripoti kwamba wanastahili.

Alivitaja vigezo vya kupewa adhabu hiyo kuwa ni umri ambapo Mramba na Yona wana miaka 75.

Kigezo kingine ni endapo wahusika ni wakosaji wa mara ya kwanza, na kingine ni kama watuhumiwa wanajutia kosa lao na wanakubali kuitumikia jamii bila kulipwa na kuangalia umbali wanakoishi na eneo analokwenda kufanyia shughuli za kijamii pamoja na tabia za washtakiwa.

Alisema sheria haijapendekeza makosa yapi wasipewe kifungo cha nje, isipokuwa inatamka kwa yeyote aliyefungwa kuanzia miaka mitatu kushuka chini.

“Mramba na Yona baada ya kuridhika kwamba wanashtakiwa, wamepangiwa kufanya usafi Hospitali ya Palestina Sinza kila siku kuanzia Jumatatu mpaka Ijumaa na watatumikia mpaka Novemba 5, 2016.

“Watakuwa wanafanya kazi kwa saa nne, wenyewe wameridhia kutumikia adhabu hiyo na endapo watakaidi watarudishwa kifungoni,” alisema Hakimu Mkeha.

Hata hivyo, Mramba na Yona walirudi gerezani kwa ajili ya kukamilisha taratibu, wanatarajia kuanza kutumikia adhabu hiyo Jumatatu.

Kisutu Julai 6, 2015

Julai 6, 2015, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliwahukumu kwenda jela miaka mitatu na kulipa faini ya Sh milioni tano Mramba na Yona, huku ikimuachia huru aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Gray Mgonja, baada ya kumuona hana hatia.

Walikuwa wanakabiliwa na mashtaka mawili ya matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia Serikali hasara ya Sh bilioni 11.7 kwa kutoa msamaha wa kodi kwa Kampuni ya Kukagua Madini ya Dhahabu ya M/S Alex Stewart ya Uingereza.
Hukumu hiyo ilitolewa na jopo la mahakimu watatu, Saul Kinemela, Jaji Sam Rumanyika na Jaji John Utamwa, aliyekuwa mwenyekiti wa jopo hilo.

Kwa mara ya kwanza washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo mwaka 2008, wakikabiliwa na mashtaka ya kuisababishia Serikali hasara ya kiasi hicho cha fedha.

Mahakama Kuu Oktoba 2, 2015

Hata hivyo, Oktoba 2, 2015, viongozi hao wastaafu walipinga adhabu hiyo na kukata rufaa.

Katika rufaa waliyokata Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam mbele ya Jaji Projest Rugazia, wafungwa hao walipunguziwa adhabu kwa kosa la kuisababishia Serikali hasara, hivyo wakabakia na adhabu ya kutumikia kifungo miaka miwili jela kwa kutumia madaraka vibaya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles