29.7 C
Dar es Salaam
Monday, October 2, 2023

Contact us: [email protected]

Waasi Burundi waingia nchini

Kassim MajaliwaAgatha Charles na Elias Msuya

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, ametoa hotuba ya kuahirisha Bunge la Jamhuri ya Muungano mjini Dodoma jana, huku akibainisha kuwepo kwa kundi la askari waasi kutoka nchini Burundi ambalo limeingia nchini kupitia kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu, iliyopo mkoani Kigoma.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, kundi hilo liliingia nchini sanjari na wananchi wa kawaida na kwamba linawashawishi vijana kujisajili katika vikundi vya waasi.

Alisema kundi hilo limebainika baada ya kufanyika upekuzi na ukaguzi kwa wakimbizi unaofanywa na vyombo vya dola sanjari na taarifa za kiintelijensia.

Kwa mujibu wa maelezo hayo aliyoyatoa mbele ya Bunge; kutokana na wimbi kubwa la wakimbizi kutoka nchini Burundi, kumejitokeza matukio ya uhalifu wa kutumia silaha za moto ndani na nje ya kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu.

“Aidha, kutokana na upekuzi na ukaguzi  kwa wakimbizi unaofanywa kwa pamoja na vyombo vya dola sanjari na taarifa za ki-intelijensia, imebainika kuwepo kwa askari waasi waliokimbia pamoja na raia wa kawaida ambao wanajaribu kuwashawishi vijana kujisajili ili kujiunga na vikundi vya waasi,” alisema Waziri Majaliwa.

Waziri Majaliwa alisema pamoja na hali hiyo, lakini hali ya usalama nchini ni shwari, ingawa kumekuwa na changamoto ya ongezeko kubwa la wakimbizi, hususani katika Mkoa wa Kigoma.

Alisema kambi za mikoa ya Kigoma, Katavi, Tabora na Tanga zinahifadhi wakimbizi wapatao 218,895 kutoka  mataifa  ya  Burundi (wakimbizi 156,377),  Congo-DRC (wakimbizi 62,176).

Alizitaja nchi nyingine kuwa ni Somalia (wakimbizi 150) na Mataifa Mchanganyiko (wakimbizi 192) kutoka nchi za Rwanda, Uganda, Sudan ya Kusini na Ethiopia.

“Kwa ujumla, katika kipindi hiki wamepokelewa wakimbizi zaidi ya 122,267 kutoka Burundi. Aidha, hadi  kufikia Desemba 31, 2015, kambi mpya ya wakimbizi ya Nduta ilipokea  wakimbizi 38,994, wengi kati yao wamehamishiwa kutoka Kambi ya Nyarugusu na wachache wakiwa wameingia moja kwa moja kutokea Burundi,” alisema Majaliwa.

Waziri Mkuu alitoa wito kwa wananchi na wakimbizi kushirikiana na vyombo vya usalama kutoa taarifa za uhalifu, hususan umiliki haramu wa silaha za moto kwenye makambi na katika maeneo mbalimbali.

Wakati huo huo, Majaliwa alisisitiza zaidi juu ya utoaji wa elimu bure, ikiwa ni miongoni mwa ahadi za Rais John Magufuli wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.

Msisitizo huo wa Waziri Mkuu Majaliwa umekuja huku kukiwa na utata wa utoaji wa elimu hiyo miongoni mwa wabunge na wananchi.

Waziri Mkuu Majaliwa alisema kuna umuhimu wa kutoa elimu na ufafanuzi zaidi juu ya utekelezaji wa agizo la elimu bila malipo kwa Watanzania kuanzia darasa la awali hadi kidato cha nne katika shule za umma.

“Hii ni hatua ya Serikali katika kuhakikisha uwepo wa fursa ya elimu bora kwa wote kwa kuwapunguzia mzigo wazazi na walezi kugharamia au kuchangia upatikanaji wa elimumsingi. Katika mpango huu, Serikali imedhamiria kuhakikisha kuwa mwanafunzi atasoma kuanzia darasa la awali hadi kidato cha nne bila wazazi na walezi kulipa ada ya shule, gharama za mitihani na michango mbalimbali,” alisema Majaliwa.

Hata hivyo, alisema yapo majukumu ambayo yataendelea kutekelezwa na wazazi na walezi ambayo ni pamoja na kununua sare za shule na michezo, madaftari, kalamu na chakula kwa wanafunzi wa shule za kutwa.

“Maeneo mengine ni kulipia nauli ya kwenda na kurudi shule na mahitaji mengine kama kununua godoro, shuka na vifaa vya usafi binafsi. Mzazi au mlezi ana wajibu wa kugharamia matibabu ya mtoto wake,” alisema Majaliwa.

Aliwataka wabunge wote kushirikiana kuunga mkono uamuzi wa Serikali kuhusu elimu bila malipo.

“Nawaomba wote kwa ujumla wetu kushirikiana kuwaelimisha wananchi wetu kuhusu utaratibu huu na wajibu wa kila mmoja wetu kama mzazi/mlezi, Serikali na jamii kuhusu utekelezaji wa zoezi hili. Nia yetu ni kuhakikisha Watanzania wanapata fursa ya kupata elimu bora kwa mtoto mwenye umri wa kwenda shule na wote walioko katika Shule za Msingi na Sekondari,” alisema.

Kuhusu wanafunzi wa bweni, Majaliwa alisema Serikali imetenga Sh bilioni 131.4 kuanzia Desemba 2015 hadi Juni, 2016, kuhudumia wanafunzi wa bweni kwa chakula, kufidia gharama za ada za mitihani, ada ya shule na kutoa fedha za uendeshaji wa shule (Capitation Grants).

“Tunatambua katika utekelezaji wa zoezi hili zipo changamoto zilizojitokeza. Kwa mfano, baadhi ya shule zenye wanafunzi wachache kupata fedha kidogo sana kwa kuwa ugawaji wa fedha unazingatia idadi ya wanafunzi,” alisema.

Aliongeza kuwa, zipo changamoto nyingine katika kutoa chakula cha mchana kwa wanafunzi wa kutwa na uendeshaji wa hosteli ambazo wazazi na walezi au jamii walikuwa wanachangia fedha za chakula.

Kuhusu mikopo ya elimu ya juu, alisema Serikali imeendelea kutoa huduma ya mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2015/2016 kwa kuzingatia Sheria ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu Namba 9 ya mwaka 2004.

“Hadi kufikia mwishoni mwa Januari 2016, Serikali ilikuwa imetoa mikopo yenye thamani ya Sh bilioni 207.9 kwa wanafunzi 122,786 wa elimu ya juu, wakiwemo wanafunzi wa mwaka wa kwanza 53,850, ambao ni asilimia 98.9 ya wanafunzi 55,254 walioomba mikopo hiyo,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles