23.2 C
Dar es Salaam
Thursday, June 1, 2023

Contact us: [email protected]

Ukawa kuzunguka nchi nzima

mbowe_bungeNa Khamis Mkotya, Dodoma

VYAMA vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), vinakusudia kufanya ziara ya kuzunguka nchi nzima kuwaeleza wananchi kilichotokea bungeni hadi wabunge wa upinzani wakafukuzwa.

Mpango huo ulitangazwa jana na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe katika viwanja vya Bunge alipozungumza na waandishi wa habari.

Alifanya hivyo ikiwa ni siku moja tangu wabunge saba wa upinzani wasimamishwe kuhudhuria vikao vya Bunge, baada ya kukutwa na makosa ya kudharau kiti na kufanya fujo bungeni.

Uamuzi huo wa Bunge ulitolewa kwa kuridhia mapendekezo ya adhabu yaliyotolewa na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, baada ya kuwahoji wabunge hao kutokana na kufanya vurugu katika mkutano wa pili wa Bunge wa Januari 27, 2016 kuhusu matangazo ya Bunge ‘Live’.

Wabunge waliowekwa kifungoni kwa vipindi tofauti  ni Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, Mbunge wa Bunda Mjini, Esther Bulaya, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema na Mbunge wa Babati Mjini, Pauline Gekul.

Wengine ni Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee wote kutoka Chadema   na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe wa Chama cha ACT- Wazalendo.

Mbowe alisema baada ya kutoka bungeni, wabunge wa kambi hiyo watakutana   kujadili na kupanga mikakati ya pamoja kufanya siasa nje ya Bunge, kutokana na mwenendo wa kiongozi huyo wa Bunge na hatua ya wabunge wa upinzani kufukuzwa.

“Siasa haifanywi ndani ya Bunge pekee, siasa inafanywa pia nje ya Bunge na tutafanya siasa nje ya Bunge, tutakwenda kuwashitaki kwa wananchi juu hiki kilichotokea bungeni  wananchi waelewe,” alisema.

Alipoulizwa anazungumziaje habari ya kufanya siasa bungeni wakati kinachopaswa kufanywa ndani ya Bunge ni hoja, Mbowe alisema: “Mimi sijui hoja ni nini na siasa ni nini? Lakini kwangu mimi kinachofanyika bungeni ni siasa kwa asilimia 100, tunakwenda kukutana na wenzetu kupanga,” alisema.

Hiyo itakuwa mara pili kwa vyama vya upinzani kwenda kwa wananchi.  Mwaka 2007 aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe wakati huo akiwa Chadema, aliwahi kusimamishwa kwa miezi mitatu kuhudhuria vikao vya Bunge  kutokana na hoja ya Buzwagi.

Kutokana na adhabu hiyo,  Chadema kwa kushirikiana na vyama vingine vya upinzani kiliratibu na kufanya ziara nchi nzima kuwaeleza wananchi kuhusu adhabu ya Zitto.

Zitto aliibua hoja binafsi akituhumu liyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi kwamba alisaini mkataba wa Buzwagi hotelini  Uingereza kinyume na utaratibu.

Waanza kumsusia Dk. Tulia

Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni jana ilianza kutekeleza azimio lake la kutokuwa na imani na Naibu Spika, Dk. Ackson Tulia.

Hatua hiyo ilijitokeza jana asubuhi wakati wabunge wa kambi hiyo walipotoka nje  baada ya Naibu Spika kumaliza kusoma dua ikiwa ni ishara ya kuanza kwa shughuli za Bunge.

Juzi kambi hiyo ilitangaza kutokuwa na imani na Naibu Spika  kwa kile kilichoelezwa kuwa kiongozi huyo analiyumbisha Bunge katika kutekeleza majukumu yake.

- Advertisement -
Previous article
Next article

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,226FollowersFollow
567,000SubscribersSubscribe

Latest Articles