28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, October 12, 2024

Contact us: [email protected]

Ukatili wa kingono wazidi kuongezeka

GABRIEL MUSHI, DAR ES SALAAM

LICHA ya jitihada za Serikali kwa kushirikiana na watetezi wa haki za binadamu kutokomeza ukatili wa kijinsia, hali ya matukio hayo yaliyoripotiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala imeongezeka mara tatu katika kipindi cha miaka mitatu huku ukatili wa kingono ukiongoza kwa asilimia 76.

Hayo yalibainishwa Dar es Salaam jana na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mwananyamala, Dk. Daniel Nkungu, katika makabidhiano ya kituo cha kutoa huduma kwa wanawake na watoto waliofanyiwa ukatili wa kijinsia.

Akizungumza kwa niaba ya Dk. Nkungu, Ofisa Utumishi wa hospitali hiyo, Mansour Karama, alisema matukio ya ukatili wa kijinsia yaliyoripotiwa hospitalini hapo kuanzia mwaka 2016 hadi 2018, yamedhihirisha kuwa tatizo hilo bado linakua kwa kasi.

Alisema mwaka 2016, kesi 108 ziliripotiwa huku wanawake wakiwa 79 na wanaume 29, mwaka 2017, kesi 219 ziliripotiwa na wanawake walikuwa 164 na wanaume 55 wakati mwaka 2018, kesi 350 ziliripotiwa kati yake wanawake walikuwa 262 na wanaume 88.

Alisema kati ya matukio hayo, ukatili wa kingono ulikuwa asilimia 76 huku matukio mengine ikiwamo kudhuriwa kimwili yakiwa asilimia 26.

“Kwa kuwa sisi kazi yetu ni kutibu, tulikuwa tunawatibu ila namna ya kushughulikia matukio hayo ilikuwa mtihani, hivyo ujio wa kituo hiki hapa Mwananyamala utasaidia kushughulikia matukio haya kwa ukamilifu,” alisema.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF), Koshuma Mtengeti, aliiomba Serikali kutenga wataalamu wa kutosha kuhudumia kituo hicho kitakachotoa huduma kwa wahanga wa ukatili wa kijinsia ikiwamo kutoa fomu namba 3 na ushauri nasaha.

Alisema kituo hicho kilichofadhiliwa na Shirika la Maendeleo ya Idadi ya Watu Duniani (UNFPA), kimekabidhiwa na CDF kwa hospitali hiyo kwa lengo la kuwapatia msaada wahanga wa matukio ya ukatili wa kijinsia.

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. John Jingu, alisema Serikali itajitahidi kuhakikisha kituo hicho kinafanya kazi.

“Tuna vituo 11 nchi nzima, lakini kasi ya matukio haya ni kubwa na Serikali peke yake haiwezi kutokomeza hali hii, tunaomba ushirikiano zaidi ili kufikia malengo ya Serikali,” alisema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkazi wa UNFPA–Tanzania, Dk. Hashima Begum, alisema uzinduzi wa kituo hicho utakuwa chachu kwa wanawake kuripoti matukio hayo kwa sababu takwimu za Wizara ya Afya zinaonesha wanawake peke yao wanaripoti matukio ya ukatili wa kijinsia.

Naye Mwakilishi wa Kituo cha Huduma ya Simu kwa watoto kutoka Shirika la C-Sema, Thelma Dhaje, aliwataka waathirika wa matukio hayo kutoa taarifa kwa kupiga simu bure namba 116 ili kupata msaada zaidi kulingana na aina ya tukio husika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles