KIONGOZI wa upinzani wa Muungano wa Cord, Raila Odinga, ameungana na hasimu wake wa kisiasa, Rais Uhuru Kenyatta kutoa mwito wa amani na mshikamano nchini hapa.
Akizungumza katika Kanisa la Familia Takatifu mjini hapa juzi wakati wa ukumbusho wa miaka 38 tangu kufariki dunia kwa mwasisi wa taifa hilo, Mzee Jomo Kenyatta, Raila alisema Uchaguzi Mkuu wa 2017 utakuwa wa amani.
Raila alisema upinzani wa kisiasa haupaswi kusababisha umwagikaji wa damu kama ulioshuhudiwa miaka tisa iliyopita, wakati zaidi ya watu 1,000 walipouawa kutokana na mzozo wa matokeo ya kura za uchaguzi wa rais.
Alisema yeye na Uhuru wana uhusiano tangu utotoni na ili kuthibitisha hilo, walishikana mikono na kuwahimiza Wakenya wote waendelee kudumisha amani wakati nchi ikijiandaa kwa Uchaguzi Mkuu mwakani.
“Kenya ni kubwa kuliko sisi sote. Ushindani wa kisiasa usigeuke uadui. Tunapoelekea uchaguzini, joto la kisiasa litapanda. Lakini Kenya itasalia papa hapa. Tusiruhusu tena umwagikaji wa damu kwa sababu ya uchaguzi,” alisema Raila.
Awali, Raila alisema kuwa aliacha mipango yake yote ya kisiasa jana ili kuungana na Rais Uhuru kwa kuwa Mzee Kenyatta alikuwa mtu muhimu kwake.
Huku akirejea kumbukumbu za utotoni, Raila alicheka alipokumbuka siku moja alipoandamana na baba yake, Jaramogi Oginga Odinga, kwenda kwa Mzee Kenyatta.
“Kwenye mkutano wa watu wengi, ni mimi tu na Mzee Kenyatta tulioweza kuzungumza Kijerumani. Alinisalimia kwa utani nami nikamjibu kwa utani kwa lugha hiyo na tukacheka,” alisema.
Kwa upande wake, Rais Uhuru alisema nchi itaimarika zaidi iwapo wananchi wengine wataiga mfano wake na Raila.
“Urithi wa kweli na sifa bora tutakazoacha ni sisi kuishi kama taifa lenye amani na maendeleo. Kuwakumbuka wote waliotoa maisha yao ili kuwe na uhuru Kenya na kwetu sote. Tunafaa kulenga kukumbukwa kama waliochangia kuifanya Kenya kuwa taifa kuu,” alisema Rais Uhuru.