26.2 C
Dar es Salaam
Thursday, November 14, 2024

Contact us: [email protected]

Uhuru ataka vyombo vya habari kupiga vita ufisadi

ISIJI DOMINIC

RAIS Uhuru Kenyatta amedhamiria kupambana na ufisadi katika awamu yake hii ya mwisho ya uongozi na sasa ameamua kuhusisha vyombo vya habari akiamini ni visikivu na haviyumbishwi.

Akihutubia taifa katika sherehe za miaka 55 za Jamhuri ambazo ni mahsusi kuadhimisha siku Kenya ilipopata uhuru kutoka kwa wakoloni, Rais Uhuru alisisitiza dhamira yake ya kupambana na ufisadi japo alikerwa na namna mahakama yanavyoshughulikia suala nzima la dhamana kwa watuhumiwa.

Katika miaka ya nyuma, Rais aliwahi kukaririwa akisema amechoka kuwaona na kuwasikiza wachambuzi wa siasa kwenye televisheni hata kama wakati mwingine wanachambua masuala nyeti yanayogusa taifa ikiwamo ufisadi.

“Hata nimechoka kuona TV, kila wakati siasa eti analysts (wachambuzi), kila mtu eti ni mchambuzi. Kwani wanachambua nini haswa na siasa imeisha? alihoji Uhuru.

Kama hiyo haitoshi Rais Uhuru aliwahi mara mbili kuonekana kukejeli vyombo vya habari hususani magazeti ambapo mara ya kwanza alifanya hivyo akiwa ziarani Chuka na tena Kaunti ya Bomet baada ya kurejesha bungeni Muswada wa Habari.

“Mimi husoma tu vichwa vya habari… ninazidi kusema mimi hutumia magazeti kufunga nyama. Niliwaambia gazeti ni ya kufunga nyama,” alisema.

Lakini wiki iliyopita akihutubia Taifa katika Uwanja wa Kitaifa wa Nyayo jijini Nairobi kwenye sherehe za Jamhuri, Rais Uhuru aliwataka wale wote wenye taarifa za ufisadi kama hawawezi kufikisha kwa mamlaka husika waende kuripoti kwa vyombo vya habari kwa sababu anaamini wao (vyombo vya habari) wanao ujasiri wa kuchapisha na kutangaza na baadaye sheria kufuata mkondo wake.

Aliwaonya wale wanaojihusisha na ufisadi na matumizi mabaya ya ofisi kwamba wanaweza kukimbia lakini hawawezi kujificha na Serikali itahakikisha kila senti waliyoiba inarudi kwa Wakenya.

Rais Uhuru alisema umefika wakati wa wananchi kuacha kuangalia wakiwa pembeni na kujihusisha kikamilifu katika vita ya ufisadi akisisitiza hakuna mtu aliyepewa jukumu la kuongoza ofisi za umma anayo haki kuomba rushwa au kutumia vibaya mali ya umma.

“Nimeonesha mfano kupambana na hili janga na sasa nataka na nyinyi mnioneshe mapambano yenu. Toa taarifa ya tukio lolote la kiufisadi kwa maofisa wa upelelezi makosa ya jinai walio karibu yako, kama hawatasikia toa ripoti kwa ofisi ya Tume ya Kupambana na Rushwa iliyo karibu nawe. Na kama hawatasikia peleka taarifa hiyo kwa vyombo vya habari na asasi za kiraia ili wawaanike wahusika. Msichoke kufanya kitu kilicho sahihi,” alisema Rais.

Katika hotuba hiyo ambayo huenda si habari njema kwa mafisadi hususani kuelekea sikukuu za Krismasi, Rais Uhuru alimpongeza Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, Noordin Haji, ambaye amekuwa akivutana na mahakama kutokana na dhamana nyepesi wanayotoakwa watuhumiwa wa ufisadi.

Mwezi uliopita, Haji alisema maofisa wakuu wa serikali wanaokabiliwa na kesi za ufisadi bado wapo kazini na wanalipwa hivyo kufanya kazi yake kuwa ngumu. Rais alitaka mahakama kuacha kutoa dhamana za ajabu ambayo inawapa uhuru watuhumiwa kuvuruga mwenendo wa kesi.

Kitendo cha Rais Uhuru kuwataka watu wenye taarifa za ufisadi kutoa ripoti kwa vyombo vya habari ni ishara ya kiongozi huyo kuchukua vita hivyo katika sura nyingine hususani pale mamlaka husika zinashindwa kutekeleza wajibu wao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles