29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Mradi wa umeme wa Rufiji (RHPP) Ndoto ya Mwalimu Nyerere inayotekelezwa na JPM

MWANDISHI WETU – DAR ES SALAAM

MACHO ya Watanzania yameshuhudia historia kubwa ikiandikwa chini ya Rais Dk. John Magufuli baada ya kufanyika kwa tukio la utiaji saini mkataba wa ujenzi wa mradi wa umeme wa Bonde la Mto Rufiji kati ya Tanzania na Misri ambao umesubiriwa kwa zaidi ya miaka 40 sasa.

Kabla ya kuendelea na makala haya nimpongeze Rais Dk. Magufuli kwa kuonesha uzalendo kwa nchi yake. Rais Dk. Magufuli amejiwekea historia kwa kuhakikisha mradi huo unafanikiwa. Hongera Rais.

Baada ya kumpongeza Rais Magufuli nikiri kutambua kazi iliyopo mbele yetu katika kuhakikisha tunashirikiana kwa umoja wetu kufanikisha dhamira ya Rais wetu kuhakikisha Tanzania inakuwa na nishati ya umeme ambao utatosheleza mahitaji ya nchi yetu na hata kuuza kwa nchi nyingine.

Kwa kukumbusha tu mradi huo uliosainiwa Ikulu jijini Dar es Salaam Desemba 13, mwaka huu ulishuhudiwa pia na Waziri Mkuu wa Misri, Dk. Mostafa Madbouly ambaye aliongozana na Waziri wa Nishati wa nchi hiyo, Dk. Mohamed Shaqqah pamoja na viongozi wengine 150.

Nakumbuka maneno ya msingi ambayo Rais Magufuli alisema wakati wa utiaji saini kwa kuweka wazi mradi huo utakapo kamilika utazalisha megawati 2,100 na kugharimu Sh. trilioni 6.558, fedha zitakazotumika ni za walipa kodi wa Tanzania.

“Pamoja na mambo mengine mradi huu utakapokamilika, utasaidia pia kutunza mazingira tofauti na baadhi ya watu wanaoupinga wanaodai kuwa utaharibu mazingira. Kabla ya kufikiwa kwa uamuzi wa utekelezaji wa mradihuo, baadhi ya watu walipinga mradi huo kwa kigezo kuwa utaleta tishio la uharibifu wa mazingira katika hifadhi ya Selous jambo alilosema si la kweli,” alisema Rais Magufuli

Alieleza matarajio ya mradi huo ulikuwa uanze kujengwa tangu mwaka 1970 lakini leo ni zaidi ya miaka 40 ndiyo unaanza kutekelezwa.

Rais Magufuli alisema kuwa “Mradi huu umepigwa vita sana kwa hiyo sishangai kama mawazo haya ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere tangu mwaka 1970 leo ndiyo tunakuja kuweka saini zaidi ya miaka 40, nilijua matatizo waliyokuwa wanapambana nayo.

“Nafahamu wapo wanaosema mradi huu utaharibu mazingira, hiyo si kweli hata kidogo ninavyojua mradi huu utasaidia kutunza mazingira. Kwanza ni kwa sababu umeme wa maji ni rafiki wa mazingira, pili eneo la kutekeleza mradi huu ni dogo ambalo ni asilimia 1.8 hadi 2 ya eneo zima la Selous.”

Alifafanua kuwa mradi utakapo kamilika utazalisha umeme kwa miaka 60 na gharama za kuzalisha umeme wa maji ni ndogo kuliko zingine, gharama za kuuza pia itakuwa nafuu kwa hiyo ukikamilika umeme utashuka.

Alisema kuwa bei ya umeme kwa nchi yetu ni kubwa kuliko nchi zingine na kutoa mfano umeme hapa kwetu kwa unit unauzwa dola za kimarekani senti 10.7 wakati Misri ni senti 4.6, Korea ya Kaskazini ni chini yasenti 8, China nayo ni hivyo hivyo chini ya senti 8.

“Afrika Kusini ni senti 7.4, India ni senti 6.8, Ethiopia senti 2.4. Hii ndiyo inatufanya gharama za uzalishaji kuwa juu kwa sababu gharama za umeme ziko juu.

“Kwa hiyo mradi huu utakapokamilika tutauza umeme kwa bei ya chini, viwanda vyetu product (uzalishaji) yake itakuwa kwa bei ya chini na tutaweza kushindana kwenye soko la kimataifa,” alisema Rais Magufuli.

Ni wazi kabla ya kuamua kuanza kwa mradi huo, walikaa chini na kutafakari kwamba ni chanzo kipi kitafaa katika mazingira ya sasa ya kupata umeme ndipo wakabaini mradi huo ndiyo unafaa.

Hifadhi ya mazingira

Kutokana na umuhimu wa mradi huo wa Taifa, Rais Magufuli alisema ukikamilika utapunguza ukataji wa miti kwa sababu utafiti uliofanyika mwaka 2015, mgawanyo wa matumizi ya aina ya nishati ya kuni na mkaa ni asilimia 92, petrol asilimia 7 na umeme asilimia 1.

“Kwa mujibu wa utafiti huo, matumizi ya mkaa yanakadiriwa kuwa ni tani milioni 2.3 kwa mwaka na inatarajiwa kuongezeka ifikapo mwaka 2030.

“Ili kuzalisha tani moja ya mkaa kwa kutumia matanuru yakienyeji zinahitaji tani 10 mpaka 12 za miti ili upate tani moja ya mkaa, hii maana yake ni kwamba  milioni 2.3 za mkaa tunazotumia kwa mwaka zinahitaji milioni 23 hadi tani milioni 27 za miti.

“Utafiti unaonesha kwa kila miti 18 inatoa magunia 26 yamkaa yenye kilo 53 zitatumia miti milioni 30. Hivyo basi kukamilika kwa mradi huu utasaidia kuokoa idadi kubwa ya miti na hivyo kutunza mazingira yetu ndiyo maana nasema huu mradi ni rafiki wa mazingira kwa sababu utaokoa miti inayokatwa kwa ajili ya mkaa na kuni,” alisema mkuu huyo wa nchi

Hatua hiyo inamfanya kiongozi huyo wa nchi kuwataka wapenda mazingira wote kuunga mkono mradi huo mkubwa wa kihistoria nchini kwa sababu utatunza mazingira na kuinua uchumi.

Kutokana na hali hiyo aliipongeza kampuni hiyo ya Arab Contractors ya nchini Misri kwa kushinda zabuni ya mradi huo  na kwamba wanao utaalamu wa ujenzi kulikotaifa lolote.

Alisema mkandarasi wa mradi huo, atapewa miezi sita kwa ajili ya kukusanya vifaa na miezi 36 kwa ajili kukamilisha mradi huo.

“Naamini mkandarasi atakamilisha mapema kwa sababu Wamisrini wachapa kazi sana, kwa hiyo wakiukamilisha mapema itadhihirisha hiyo historia ya Wamisri.

“Nilipokuwa nazungumza na Rais wa Misri amenihakikishia kwamba wameamua kujenga mradi huu na kwamba yeye anauchukua kama project yake na alitamani sana awepo kusaini nikamwambia siku ya jiwe la msingi aje.

“Kwa hiyo nitashangaa Arab Contractors  wakiuchelewesha nitasikitita sana hela yakulipa kwa asilimia 15 tunazo leo kwa sababu mradi huu umepigwa sana vita. Mradi huu una baraka za pekee kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa sababu utiaji saini umeshuhudiwa na viongozi wa dini haijawahi kutokea viongozi wa dini wakawawengi kiasi hiki, nimefurahi na viongozi wa dini ninawashukuru sana.

“Haiwezekani viongozi wote hawa wa dini wote waje halafu mradi usifanyike na kule Misri ndiko Yesu alikokimbilia,” alisema.

Aliwataka wananchi wa maeneo ambayo mradi unatekelezwa waunge mkono na wasifuge mifugo karibu na mradi huu.

Waziri Mkuu wa Misri

Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Misri, Dk. Mostafa Madbouly, alisema Serikali yake itaendelea kuimarisha ushirikiano wa kiufundi, kitaalamu na kidiplomasia na Tanzania ili kuhakikisha kuwa ndoto za waasisi waurafiki wa mataifa hayo zinaweza kutimizwa ikiwamo utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Madbouly alisema katika kipindi cha miaka michache ijayo, Serikali ya Misri kupitia kwa taasisi zake za kiuchumi zitaendelea kuwekeza kwakasi zaidi nchini Tanzania ili kuhakikisha kuwa miradi yote ya maendeleo inayotekelezwa na Tanzania inaweza kuleta tija kwa wananchi wake.

Ukubwa wake

Naye Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani alisema mradi huo ukikamilika utakuwa mkubwa kuliko yote Afrika Mashariki kwa kuzalisha megawati 2,115.

Alisema bwawa linalofuata kwa kuzalisha umeme mwingi ni la Bujagari nchini Uganda, likitarajiwa kuzalisha megawati 300 tu.

“Tanzania sasa kwa Afrika Mashariki ni ya kwanza tukiwa na megawati 2,115. Bwawa lililokuwa likiongoza kabla yetu ni lile la Bujagari la Uganda bado linajengwa na lina megawati 300.

“Tanzania itakuwa ya nne na kwamba nchi inayoongoza kwa kuwa na mabwawa makubwa ni Ethiopia, ambapo bwawa lake la  Renaissance linaloendelea kujengwa litazalisha megawati 6,450 na ujenzi wake utakamilika mwaka 2022. La pili lipo Mambira Nigeria linazalisha megawati 3,050, la tatu liko Ethiopia ambalo ni Shaika likizalisha megawati 2,160.

“Bwawa la tano liko Misri (Aswan Dam) la megawati 2,100 nala sita liko Angola la Rauka linalozalisha megawati 2,066. Hongera sana Rais Magufuli,” alisema Dk. Kalemani.

Ukubwa  wa bwawa

Alisema mbali na Afrika, Tanzania ni kati ya nchi 60 zenye mabwawa makubwa ya kuzalisha umeme, huku akisema jumla yapo 70.

Waziri huyo alisema bwawa kubwa kuliko yote liko China likizalisha megawati 22,500, la pili nchini Brazil (megawati 14,000) na jingine China (megawati 13,860),” alisema

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles