29.7 C
Dar es Salaam
Wednesday, August 17, 2022

Ugwachanya: Shule inayoweka rehani maisha ya wanafunzi

jk5Na RAYMOND MINJA – IRINGA
JUNI 30 mwaka huu, ndio ilikuwa siku ya mwisho ya utekelezaji wa agizo la Rais Dk. John Magufuli la kuhakikisha kila wilaya inakamilisha utengenezaji wa madawati katika shule za msingi na sekondari.

Hata hivyo bado kuna wilaya ambazo hazijakamilisha zoezi hilo kwa wakati huku wengine wakitengeneza madawati yaliyo chini ya kiwango.

Katika mikoa mingine kuna wilaya zimefanikiwa kufanya vema katika kutekeleza agizo hilo na hata kuvuka malengo jambo lililosababisha madawati mengine kukosa sehemu ya kuwekwa kutokana na kuwa na vyumba vichache vya madarasa.

Mkoa wa Iringa ni moja kati ya mikoa iliyofanikiwa kwa kiasi kikubwa kukamilisha zoezi hilo la madawati licha ya changamoto chache zilizojitokeza katika wilaya Kilolo baada ya mbunge wa jimbo hilo kukataa madawati  zaidi ya 600 yaliyotengenezwa chini ya kiwango lakini baadaye yalirekebishwa na kuwa katika kiwango kinachokubalika.

Kwa sasa uhaba wa madawati katika mkoa huo umepungua katika shule nyingi na changamoto kubwa iliyoko sasa ni uhaba wa vyumba vya madarasa.

Katika shule nyingi mkoani humo vyumba vilivyopo havilingani na idadi ya wanafunzi waliopo.

Moja kati ya shule hizo ni Shule ya Msingi Ugwachanya iliyopo Kata ya Mseke katika Halmashauri ya Iringa Vijijini.

Shule hiyo inakabiliwa na upungufu mkubwa wa vyumba vya madarasa, huku mengine yakiwa katika hali mbaya kiasi cha kuhatarisha usalama wa wanafunzi shuleni hapo.

Shule hiyo yenye wanafunzi 578 ambayo inahudumia wanachi katika kata hiyo ni miongoni mwa shule kadhaa katika Halmashauri ya Iringa Vijijini zinazokabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo uchakavu wa miundombinu ya elimu kama vyumba vya madarasa.

Shule hiyo iliyojengwa mwaka 1975 ina vyumba vya madarasa vinane pekee huku mahitaji yakiwa ni vyumba 17.

Hata madarasa machache yaliyopo hali yake si ya kuridhisha na hivyo kuhatarisha maisha ya wanafunzi wanaoyatumia.
MWALIMU MKUU

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Mbuta Zakaria, anasema changamoto kubwa inayoikabili shule hiyo ni ubovu wa madarasa kwani ilijengwa miaka mingi iliyopita hali iliyosababisha madarasa yaliyokuwepo kuchakaa na mengine kuanguka kabisa kutokana na kuzeeka.

Mwalimu Zakaria anasema kuwa kufuatia changamoto hiyo halmashauri ya kijiji kwa kushirikiana na shule waliamua kufanya harambee na kufanikiwa kujenga madarasa mawili kwa tabu ambayo yanakamilisha idadi hiyo ya
madarasa nane.

“Hali ya madarasa kwa hapa shuleni ni mbaya ndio maana unaona yale majengo mengine (anamuonyesha mwandishi) yameanguka na mengine yaliezuliwa na upepo tukaamua kunza kuyajenga upya, lakini changamoto ni katika uchangiaji kwani tangu serikali itangaze elimu bure wazazi wengi wamekuwa ni wagumu kuchangia.

“Wanasema serikali ilitangaza elimu bure hivyo hawana haja ya kuchangia, tuliamua kuwatafuta wadau mbalimbali nao watusaidie ili tuweze kujenga vyumba vya madarasa ili watoto wetu waweze kukaa katika eneo salama,” anasema Mwalimu Zakaria.

Anasema kuwa changamoto nyingine wanayokabiliana nayo ni ukosefu wa nyumba za walimu pamoja na uhaba wa madawati kwani waliyonayo hayatoshi licha ya kupata msaada wa madawati kutoka kwa wadau mbalimbali wa maendeleo.

“Hivi karibuni tulipokea msaada wa madawati 70 kutoka kwa wadau wetu kwa kweli msaada huu utatusaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza tatizo la madawati katika shule yetu licha ya kuonekana bado kutakuwa na upungufu wa madawati mengine zaidi kwanihapo awali tulikuwa tunahitaji 170,” anasema.

 

Naye Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Ugwachanya, Charles Matunduru, anasema licha ya shule hiyo kukabiliwa na uhaba wa madawati lakini miundombinu yake ni mibovu yakiwemo majengo ambayo yamechakaa kutokana na kujengwa muda mrefu.

WADAU WAJITOLEA KUISAIDIA

Jesca Msambatavangu ambaye ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM ) Mkoa wa Iringa, anapiga hodi shuleni hapo na kutoa rai kwa wazazi na hasa viongozi waliowahi kusoma katika shule hiyo kujitokeza kuinusuru kwa kujenga madarasa mapoja na kusaidia mahitaji mbalimbali.
Msambatavangu anabainisha kuwa ni wajibu wa vingozi wa kiserikali na watu wengine waliopita katika shule mbalimbali hapa nchini kugeuka nyuma na kuangalia shule  walizosoma ili kuweza kusaidia katika mambo mbalimbali ikiwa ni kama kurudisha fadhila kwa kile walichokipata katika shule hizo.

“Kumekuwa na kasumba ya viongozi wakubwa wa kiserikali hasa wanasiasa kusahau walikotoka na kushindwa kusaidia kuimarisha miondombinu ya shule walizosoma ili kuwasaidia watoto wa watu wengine waweze kusoma sehemu nzuri nao waje kuwa na maisha mazuri kama wao.

“Nawaomba wakubwa wote hasa wana CCM wenzangu tujitokeze kusaidia shule zetu, tuwekeze katika elimu. Mimi
nimewasaidia madawati si kwamba nina fedha nyingi, hapana ni wajibu wetu kurudisha hata kile kidogo tulichopata na Mungu atakubariki.

“Using’ang’anie kukusanya tu mwisho wa siku utakusanya na visivyo vyako halafu Mungu anavichukua utafanyaje,” anasema Msambatavangu.

Anasema urithi mkubwa katika maisha ya mtoto hapa duniani ni kumpatia elimu bora na hiyo huchangiwa kwa kiasi
kikubwa na mazingira ya kusomea hivyo ni jambo la busara kila mmoja kushiriki kusaidia suala la elimu katika nafasi aliyonayo.

Mdau mwingine wa maendeleo mkoani humo, Kampuni ya Dash Industries ltd baada ya kusikia kilio cha shule hiyo iliamua kutoa madawati 20 yenye thamani ya Sh 500,000 kuunga mkono mkono agizo la Rais Magufuli la kutaka kila mwanafunzi akae kwenye dawati.

Mwakilishi wa kampuni hiyo, Samiri Mether, anasema ni jukumu la jamii kujitolea kuchangia shughuli za
maendeleo katika maeneo yao ili kusukuma mbele gurudumu na kuachana na dhana potofu kuwa kila jambo linapaswa kufanywa na serikali.

“Tumeanza na madawati ili watoto wetu waweze kusoma wakiwa wamekaa, tumekuwa tukichangia sehemu mbalimbali ikiwemo kuwaletea maji na leo tumekuja katika elimu. Naamini pia tutashiriki hata katika ujenzi wa madarasa yanayo poromoka,” anasema Mether.

Mdau huyo anawataka wazazi, walezi na wadau mbalimbali kuendelea kuchangia shughuli za kimaendeleo katika shule na kuachana na dhana ya kusema kuwa elimu ni bure.

“Kila kukicha huwa kunaibuka mambo mapya yanayohitaji michango au nguvu kazi za wazazi ili kuweza kutatua changamoto husika hivyo kama kwa dhana kuwa elimu ni bure ni dhahiri kuwa tutachukua muda mrefu kupata maendeleo,” anasema.

Mmoja wa wananchi wa Kijiji hicho, Tilifina Mtavilalo, anapaza sauti kwa wadau mbalimali kuweza kujitokeza ili kuinusuru shule hiyo iliyo hatarini kuporomoka ili wanafunzi waweze kupata sehemu nzuri za kujisomea.

 

“Watoto hawa ndio viongozi wa kesho hivyo kama hatutajitoa kutengeneza miundombinu ya shule tutafifisha ndoto zao.
“Kuna watu wachache wenye moyo wa kujitoa kusaidia watu wengine ilhali wao hawakusoma katika shule hizo na wala si wakazi wa eneo hilo lakini

wamekua wakitoa fedha zao kusaidia mambo mbalimbali hapa nchini, hivyo hakuna budi na wengine kujitokeza kuwekeza katika elimu badala ya kuangalia nini atakachokipata baada ya kutoa msaada wake,” anasema Mtavilalo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,905FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles