Na Celina Mwakabwale, Dodoma
Afisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote(UCSAF), Justina Mashiba amesema kupitia miradi ya Mfuko huo wamekuwa wakitoa mafunzo yenye lengo la kumuhamasisha mtoto wa kike kupenda masomo ya sayansi, kuwa mbunifu na kupenda kujifunza masuala ya teknolojia na TEHAMA tangu anapokuwa shuleni.
Amesema, mpaka sasa UCSAF imetoa mafunzo ya TEHAMA kwa wanafunzi wa kike 744 wa shule za umma Tanzania nzima, imetoa vifaa vya TEHAMA kwa shule takribani 700 pamoja na kuunganisha shule 400 za umma na mtandao wa intaneti.

Mashiba ameeleza hayo alipokuwa akijibu swali lililoelekezwa kwake kuhusu mchango wa UCSAF katika kuwajengea uwezo wasichana wa kushiriki kwenye masuala ya ubunifu na kuhimiza matumizi ya TEHAMA tangu wanapokuwa shuleni ikiwa ni pamoja na kusaidia watoto wa hao kupenda masomo ya sayansi ili kuongeza idadi ya wanawake wataalam wa masuala ya TEHAMA hapa nchini.
Akiendelea kutoa ufafanuzi amesema, kupitia siku ya kimataifa ya mtoto wa kike na TEHAMA (girls in ICT), Mfuko umekuwa ukiendesha mafunzo kwa watoto wa kike waliofanya vizurI kwenye masomo ya sayansi kutoka shule zote za umma za Tanzania bara na Zanzibar.
Pia ameongeza kuwa Mfuko unatekeleza mradi wa kutoa vifaa vya TEHAMA kwa shule za umma na kusaidia katika kuziunganisha shule hizo na mtandao wa intaneti ili kurahisisha mchakato wa kujifunza masomo ya TEHAMA.
Aidha, Mashiba ametoa wito kwa wazazi kuunga mkono juhudi hizo za Serikali huku akisisitiza mabadiliko ya kimtazamo kuhusu mtoto wa kike.
“Baadhi ya wazazi wanaamini kuwa TEHAMA na ubunifu ni kwa ajili ya mtoto wa kiume, ili watoto wa kike wawe na ujasiri inabidi wazazi na walimu watoe elimu na kuamini kuwa TEHAMA sio ngumu kama ambavyo tumeaminishwa,” aliongeza Mashiba.

Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk. Zainab Chaula amepongeza juhudi za UCSAF huku akitoa wito kwa taasisi hiyo ya Serikali kuendelea kushirikiana na wadau wengine katika kuufanya ubunifu kuwa rafiki kwa wanawake na wasichana nchini. Dk. Chaula ameongeza kuwa ubunifu ni Sera ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo imedhamiria kujenga uchumi wa kati wa juu unaotegemea viwanda ifikapo mwaka 2025.
Nae mbunge wa viti maalum CCM, kundi la Asasi za kiraia Tanzania Bara, Neema Lugangira ametoa wito wa kupitia sera ili kuhakikisha zinamjumuisha msichana na mwanamke hasa aliyeko pembezoni huku akisisitiza kuwa wanawake wanaoishi maeneo ya vijijini wanapaswa pia kuwa na uelewa wa matumizi ya teknolojia zilipo.
Majadiliano hayo yameandaliwa na kituo cha ujasiriamali na ubunifu cha Capital space kwa kushirikiana na jukwaa la kuwezesha wanawake wajasiliamali (NDOTO HUB) pamoja na mtandao wa kujifunza kidigitali (Shule Direct) ikiwa ni katika kuadhimisha wiki ya ubunifu kwa mwaka 2021.

Washiriki wengine katika majadiliano hayo walikuwa ni Tupokigwe Isagah Mhadhiri kitengo cha Sayansi ya Teknolojia Chuo kikuu cha Mzumbe, Jumanne Mtambalike Mtendaji Mkuu wa Sahara Ventures na Irene Paul msanii na mbunifu wa asili( naturaliStar).