28 C
Dar es Salaam
Monday, January 24, 2022

UCHUNGUZI MCHANGA WA DHAHABU, WAIBUA RIPOTI YA JAJI BOMANI

Na Mwandishi Wetu – Dar es Salaam


WAKATI ripoti ya Kamati ya Profesa Abdulkarim Mruma iliyoundwa na Rais Dk. John Magufuli kuchunguza kiasi cha madini yaliyomo katika kontena 277 za mchanga, ikionyesha yana thamani ya Sh trilioni 1.441, tofauti na Sh bilioni 112.1 ambazo mamlaka zilisema, gazeti hili limebaini mapendekezo yaliyowahi kutolewa ili kuepusha hali hiyo, hayakufanyiwa kazi.

Ripoti iliyokabidhiwa juzi kwa Rais Magufuli, ilionyesha kontena hizo zilizokuwa kwenye Bandari ya Dar es Salaam, na maeneo mengine tayari kwa kupelekwa nje ya nchi, zilikuwa na madini ya dhahabu, shaba, fedha, sulfur, chuma, iridium, rhodium, lithium, ytterbium, tantalum na beryllium, ingawa baadhi yake yalikuwa hayajaorodheshwa kwenye nyaraka za mamlaka za Serikali.

 

RIPOTI YA TEITI

Ripoti ya sita ya Kamati ya Uhamasishaji wa Uwazi Katika Mapato ya Madini, Gesi na Mafuta (Teiti), iliyozinduliwa Aprili mwaka jana, ilionyesha kwa mwaka Serikali hupoteza Sh bilioni 6 kwenye mapato ya madini.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Jaji Mark Bomani, alisema kiasi hicho kimepungua kutoka Sh bilioni 66 zilizokaririwa kwenye ripoti ya kwanza ya kamati hiyo ya mwaka 2009.

 “Ripoti ya kwanza ya mwaka 2009 ilionyesha nakisi ya Dola za Marekani milioni 30 (Sh bilioni 66). Hii ilitushtua sana,” alisema Jaji Bomani na kuongeza:

“Angalau ripoti ya mwaka 2014 nakisi imeshuka hadi kufikia Sh bilioni 6. Jumla ya mapato ya Serikali yamepanda kutoka Sh bilioni 28 hadi Sh trilioni 1.2, yaani ongezeko la takribani mara 10.”

 Hata hivyo, alisema licha ya ongezeko hilo, bado mapato yangeongezeka zaidi kama hatua zingechukuliwa.

“Kwa mfano hadi mwaka 2012 mrabaha unaotolewa na kampuni za madini ya dhahabu ulikuwa asilimia tatu. Kamati yangu ilipendekeza… kwanza asilimia ya mrabaha iongezwe kutoka asilimia tatu hadi angalau asilimia tano. Pili, mrabaha usiwe faida zilizopata hizo kampuni, bali jumla ya mauzo. Tofauti yake ni kubwa mno,” alisema Jaji Bomani.

Aliongeza kuwa Serikali ilitekeleza ushauri huo na kupandisha mrabaha huo, kutoka asilimia tatu hadi nne. Hata hivyo alisema pendekezo lao la kutaka asilimia 60 ya mauzo ya kampuni za madini yarejeshwe nchini, halikukubaliwa.

“Kampuni za madini ya dhahabu kwenye mikataba maalumu ziliruhusiwa kuwekeza nje mauzo yao yote, kinyume na utaratibu wa kampuni nyingine ambazo hutakiwa kurejesha nchini mauzo yao,” alisema. Alisema kwa bahati mbaya zaidi ruhusa hiyo imerasimishwa katika sheria ya madini ya mwaka 2010.

 “Utaratibu huu umeinyima Tanzania fursa ya kuongeza fedha za kigeni (foreign reserves) jambo linalochangia kuimarisha thamani ya shilingi. Naishauri Serikali kulitafakari suala hili hasa kwa kujua kwamba ni asilimia 20 tu ya madini yaliyogunduliwa ndiyo inachimbwa hadi leo. Bado asilimia 80 hayajachimbwa,” alisema.

Tanzania ilipitisha sera ya madini mwaka 1997 kwa lengo la kuhakikisha inachangia ipasavyo katika pato la taifa.

 Kufuatia kupitishwa kwa sera hiyo, Serikali iliwasilisha bungeni muswada wa sheria ya madini na kupitishwa mwaka 1998. Sheria hii ilikusudiwa kuweka misingi ya kisheria ya kufanikisha utekelezaji wa sera ya madini.

Takwimu zinaonyesha kuwa shughuli za uchimbaji mkubwa wa madini zimeongezeka kwa kuanzishwa migodi mikubwa sita mipya ya dhahabu kati ya mwaka 1997 na 2007.

 

MIKATABA YA MADINI

Kati ya mwaka 1994 na 2007, mikataba ya migodi mikubwa sita ya dhahabu ilisainiwa

 1.  Bulyanhulu Agosti 5, 1994
 2.  Golden Pride ulioko Nzega – Juni 25, 1997
 3. Geita Gold Mine uliopo Geita – Juni 24, 1999
 4. North Mara uliopo Tarime – Juni 24, 1999
 5. Tulawaka uliopo Biharamulo – Desemba 29, 2003
 6. Buzwagi uliopo Kahama – Februari 17, 2007

 

 

MAPENDEKEZO YA RIPOTI YA BOMANI 2008 KATIKA MIKATABA YA MADINI

 

 • Kuwapo mfumo imara wa sheria utakaofanya uwekezaji katika shughuli za madini ufanyike kufuatana na sheria za nchi zinazosimamia uwekezaji kwa ujumla badala ya mikataba maalumu na mwekezaji mmoja mmoja

 

 •  Mikataba binafsi iruhusiwe pale tu ambapo uwekezaji ni wa kiwango cha dola za Marekani milioni 200 au zaidi

 

 •  Mikataba itakayoingiwa ni lazima ipelekwe bungeni kwa taarifa; Sheria ya madini ifanyiwe marekebisho ili iweke vipengele vyote muhimu vinavyohusu uwekezaji katika sekta ya madini ili kuwa na sheria inayojitosheleza

 

 •  Mikataba iwe wazi kwa wananchi na ipatikane katika ofisi za mikoa, wilaya na halmashauri ambako migodi ipo

 

 • Mikataba yote haifanani. Mikataba yote ifanane na kuwe na model agreement ambayo itakuwa sehemu ya sheria ya madini

 

 •  Msamaha wa ushuru wa mafuta isipokuwa kwa mafuta yatakayotumika kwa uzalishaji wa umeme unaotumika migodini tu; Gavana aachiwe nafasi ya kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria

 

 • Asilimia 60 ya fedha inayotokana na mauzo ya madini irejeshwe nchini kwa ajili ya matumizi ya ndani

 

Utozaji wa mrabaha; Mapendekezo:

Kamati inapendekeza kuwa tozo la mrabaha lizingatie ukokotoaji kwa kigezo cha gross value badala ya net back value.

 

Mgawanyo wa mapato yatokanayo na madini:

Kamati imebaini kuwa hakuna utaratibu wa kufanya mgawanyo maalumu kwa mapato yatokanayo na madini. Jambo hili linaleta wasiwasi na hisia tofauti kuhusu matumizi halisi ya mapato haya na manufaa yake kwa taifa na wananchi kwa ujumla.

 

Mapendekezo:

Katika mgawo wa mrabaha, 60% iende katika mfuko wa maendeleo ya madini kwa ajili ya miradi endelevu; 20% ya mrabaha iende kwenye mamlaka ya madini inayopendekezwa kuundwa katika taarifa hii; 10% iende wilaya yenye mgodi; 7% iende wilaya yenye mgodi; 7% iende kwenye halmashauri nyingine katika mkoa wenye mgodi; 3% iende kwenye vijiji vinavyozunguka mgodi.

 

Biashara ya madini;

Mapendekezo:

Kwa kuwa hakuna utaratibu maalumu wa kuuza na kununua madini, Serikali iweke utaratibu wa biashara ya madini na kusimamia ili kuepusha utoroshwaji wa madini na kupoteza mapato yake;  Kwa kuwa madini yaliyokatwa yana thamani kubwa kuliko yasiyokatwa, kuna umuhimu wa Serikali kuhamasisha na kuwezesha wafanyabiashara wafanye shughuli za ukataji wa madini;  Serikali iwe na utaratibu wa kuandaa maonyesho ya vito na kuanzisha kituo cha minada ya vito;  Kuwe na udhibiti mzuri wa madini ya vito yanayozalishwa nchini ili kuweza kuwavutia wawekezaji katika usanifu wa vito; Kuwe na kitengo maalumu katika mamlaka itakayoundwa kusimamia biashara ya madini ya vito na almasi.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
176,415FollowersFollow
531,000SubscribersSubscribe

Latest Articles