23.8 C
Dar es Salaam
Sunday, October 13, 2024

Contact us: [email protected]

UCHIMBAJI TANZANITE NJIAPANDA

Na Masyaga Matinyi, Mirerani


SHUGHULI za uchimbaji madini ya vito ya tanzanite katika eneo la Mirerani mkoani Manyara zimepungua kwa kiasi kikubwa baada ya agizo la kuwataka wamiliki wa migodi kulipa mishahara wafanyakazi wao.

Agizo hilo lilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti, Februari 25, mwaka huu alipokuwa akizungumza na wamiliki wa migodi na wachimbaji katika Mji Mdogo wa Mirerani.

Mnyeti aliwataka wamiliki wa migodi kuanza kulipa mishahara kuanzia mwezi huu (Machi), na watakaoshindwa waondoke eneo hilo.

Kutokana na agizo hilo, migodi kadhaa imesimamisha uzalishaji, jambo lililosababisha shughuli nyingi za kiuchumi katika eneo hilo kusimama au kudorora.

MTANZANIA ambalo lilikuwa Mirerani kwa takribani siku tano, limeshuhudia migodi kadhaa ikiwa imesimamisha shughuli zake, na kuwaacha mamia ya vijana wanaofanya kazi migodini wakirandaranda mitaani.

Wamiliki wa migodi kupitia chama chao cha Manyara Region Miners Association (MAREMA), walifanya kikao Jumatatu iliyopita, na kwa pamoja walisema suala la ulipaji mishahara haliwezekani kutokana na mazingira ya uchimbaji na biashara ya madini ya tanzanite.

Walisema kwa muda mrefu wamekuwa na utaratibu au mikataba na wafanyakazi wao, ambao wanawaita wabia na kwamba mgodi unapozalisha madini huchukua asilimia 10, na mmiliki 90.

“Sisi wamiliki wa migodi wenye leseni ndogo zijulikanazo kama Primary Mining Licence (PML) au wachimbaji wadogo, kiuhalisia wa mambo hatuwezi kabisa kulipa mishahara, kuambiwa tulipe mishahara, ni sawa na kutufukuza hapa Mirerani.

“Kwanza hatuna mitaji, na hata Serikali yetu kwa maana ya Wizara ya Madini ni shuhuda katika hili, kwa miaka mingi tumekuwa tukiomba iangalie utaratibu wa kutupatia mitaji na utaalamu (teknolojia), haya yote yanadhihirisha uduni wetu.

“Mifano ni mingi, unaweza kukuta mchimbaji mdogo anajinyima kiasi hata cha kuuza mali zake kama mashamba ili aweze kuhudumia mgodi, na wakati mwingine mtu anapambana kwa zaidi ya miaka 10 bila kupata hata jiwe moja. Sasa mmiliki kama huyu anatoa wapi fedha za kulipa mishahara wafanyakazi?

“Ndiyo maana wale tunaofanya nao kazi kwenye migodi yetu huwa hatupendi kuwaita wafanyakazi, badala yake tunawaita wabia, kwa sababu kinachofanyika pale ni mjumuisho wa nguvu za kila mmoja.

“Mimi mwenye mgodi natafuta fedha kuhudumia mgodi kuhakikisha chakula, maji, dizeli na mashine vinapatikana, na wabia wangine wanachangia nguvu kazi, siku tukizalisha basi tunagawana kwa mujibu wa makubaliano, na makubaliano haya yanafahamika hadi Ofisi ya Madini ya Kanda.

“Hata ilani ya chama tawala, Chama Cha Mapinduzi (CCM) inatutambua vizuri pamoja na changamoto zote tunazokabiliana nazo siku hadi siku, sasa haya yanayotokea leo, kwa kweli yanatushangaza sana, kwa sababu mwisho wa siku tutaondolewa kwenye uchimbaji.

“Pia kuambiwa tuondoke kama hatuwezi kulipa mishahara, kwa kweli ni jambo zito mno, baadhi yetu tumewekeza muda wetu mwingi kwenye migodi, na mali zetu nyingi kama si zote zimeishia kwenye yale mashimo, na hadi sasa hatujazalisha, ingawaje kwa baadhi yetu tayari dalili zimeanza kuonekana, sasa kutuambia tuondoke, ni sawa na kutuua kiuchumi na kimaisha kabisa,” alisema Abubakar Madiwa, ambaye ni Katibu wa MAREMA.

Akizungumza na MTANZANIA, mmiliki wa mgodi na mchimbaji wa siku nyingi katika eneo hilo, Money Yusuf, alisema kama hali ingekuwa inaruhusu kulipa mishahara, ingelipwa bila tatizo lolote.

Alisema mgodi wake haujawahi kuzalisha tanzanite kwa kipindi cha miaka takribani 17 sasa, ingawaje dalili za uzalishaji zimeanza kuonekana, hivyo si rahisi kulipa mishahara katika mazingira magumu kama hayo.

Akiwa mgodini kwake eneo la kitalu D, Yusuf alionyesha nakala za mikataba na utaratibu wa malipo (nakala tunazo) pindi ulipotokea uzalishaji miaka ya nyuma, ambao wahusika wote walipata mgawo wao.

Pia mchimbaji huyo aliandika historia katika eneo hilo mwaka 2002 kwa kupeleka umeme wa Tanesco kwa gharama zake kutoka eneo la kitalu B kwenda kitalu D, hatua ambayo imerahisisha na kuboresha utendaji kwa wachimbaji wengi katika eneo hilo.

“Baada ya kuona changamoto nyingi pamoja na gharama kubwa za kuendesha mitambo kwa kutumia mafuta, mwaka 2002 niliamua kuvuta umeme kwa gharama ya Sh milioni 30, na aliyekuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini wakati huo, Dk. Ibrahim Msabaha, alifika na alipongeza jitihada hizo,” alisema.

 Kwa habari zaidi jipatie nakala ya gazeti la MTANZANIA.

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles