22.2 C
Dar es Salaam
Friday, October 11, 2024

Contact us: [email protected]

HOMA YA DENGUE YAREJEA NCHINI

Na VERONICA ROMWALD-DAR ES SALAAM


UGONJWA wa homa ya dengue  umeripotiwa kurejea nchini huku wagonjwa 11 kugundulika kuugua ugonjwa huo  Dar es Salaam.

Taarifa ya Wizara ya Afya, Jinsia, Maendeleo ya Jamii, Wazee na Watoto imeeleza kuwa homa ya ugonjwa huo imendulika baada ya wagonjwa kadhaa waliokuwa na dalili zake kupimwa na kuthibitishwa.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Serikali imeanza kuweka karantini ya kuzuia kuenea kwake kwa kuweka vituo vya uchunguzi wa awali na tiba katika mikoa ya Dar es Salaam na Tanga.

Wagonjwa hao waligundulika katika Hospitali ya Taasisi ya Saratani ya Ocean Road na tahadhari imetolewa kwa wananchi kupima afya haraka wanapohisi wana homa kali, mafua na kuumwa kichwa kwa muda, ambazo ni dalili kubwa za homa ya dengue.

Akizungumza na MTANZANIA   Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Mpoki Ulisubisya amethibitisha kuwapo  ugonjwa huo.

“Ni kweli ugonjwa huo umeripotiwa kuwapo nchini, hivi sasa tunafuatilia kwa karibu tuweze kutoa tamko rasmi kwa jamii,” alisema.

Alisema ili kuudhibiti, serikali imeanza kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuzuia kuenea kwake kwa kuweka vituo vya uchunguzi wa awali na tiba katika mikoa ya Dar es Salaam na Tanga.

“Tunahimiza wananchi kupima afya haraka wanapohisi wana homa kali, mafua na kuumwa kichwa kwa muda, ambazo ni dalili kubwa za homa ya dengue,” alisema

Alisema Wizara kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) inafuatilia kwa  karibu mlipuko wa ugonjwa huo.

Utafiti wa utabibu unaonyesha mbu wanaopatikana maeneo ya pwani ndiyo hubeba zaidi vimelea vya ugonjwa wa homa ya dengue.

Hadi sasa hakuna tiba ya uhakika ya ugonjwa huo, na inaelezwa kuwa wataalamu wa afya wanaendelea kuitafuta.

Inakadiriwa watu wapatao milioni 390 huathiriwa na ugonjwa huo hasa katika maeneo ya Pwani.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linazitaka nchi zote duniani kuchukua tahadhari juu ya ugonjwa huo.

Mara ya kwanza ugonjwa wa homa ya dengue uligundulika Dar es Salaam mwaka 2014  ambako wagonjwa 400 waliupata.  Walitibiwa na kupona  isipokuwa watu watatu ndiyo walifariki dunia.

Vimelea vya ugonjwa wa homa ya dengue husambazwa na mbu kama ilivyo kwa malaria. Hivyo wananchi wanahimizwa kuua mazalia ya wadudu hao haraka.

Juni 12, 2013, Wizara ya Afya ilitoa taarifa kwa umma juu ya kuwepo kwa ugonjwa wa homa ya dengue

Ugonjwa huo ulithibitishwa baada ya sampuli zilizochukuliwa kutoka kwa watu waliohisiwa kuwa na ugonjwa huo  Dar es salaam kupelekwa kwenye maabara ya Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu.

Utafiti huu uliongozwa na jopo la wataalamu kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ikishirikisha programu ya mafunzo ya Epidemiolojia  (Field Epidemiology and Laboratory Training Program) pamoja na Manispaa ya Ilala.

Ilielezwa kuwa wagonjwa waliobainika kwa wakati huo kuwa na dalili za ugonjwa huu ni 20 na hakuna mgonjwa yeyote aliyefariki dunia.

Homa ya dengue   ni ugonjwa unaosababishwa na kirusi ambacho kinaenezwa na mbu wa aina ya Aedes.

Viluwiluwi vya mbu hao huweza kuishi katika mazingara ya ndani ya nyumba mpaka wakawa mbu kamili na kuanza kusambaza ugonjwa huu kwa binadamu.

Mbu hao huwa na tabia ya kuuma wakati wa mchana.

Dalili za ugonjwa huu ni homa, kuumwa kichwa, maumivu ya viungo na uchovu, dalili ambazo huanza kujitokeza kuanzia kati siku ya tatu na 14 tangu mtu alipoambukizwa kirusi cha ugonjwa huo.

Kwa wakati mwingine dalili za ugonjwa huo zinaweza kufanana  na  za malaria, hivyo basi wananchi wanaombwa kuwa wakati wakipata homa kuhakikisha wanapima  kugundua kama wana vimelea vya malaria ua la, ili hatua stahiki zichukuliwe.

Inaelezwa kuwa homa ya dengue inaweza kutibika kama mgonjwa atapelekwa hospitali mapema na kupatiwa matibabu ya haraka.

Jinsi ya kujikinga na dengue

Kuangamiza mazalio ya mbu,  kufukia madimbwi ya maji yaliyotuama au kunyunyuzia dawa ya kuua viluwiluwi vya mbu kwenye madimbwi hayo.

Kwa habari zaidi jipatie nakala ya gazeti la MTANZANIA.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles