UCHAKAVU WA MAJENGO WAWEKA MAISHA YA WANAFUNZI REHANI

0
509

Na Amina Omari, KOROGWE


MIUNDOMBINU isiyo rafiki ikiwamo uhaba wa vyumba vya madarasa, imeelezwa kuwa ni sababu moja wapo inayochangia kushuka kwa kiwango cha utoaji wa elimu kwa wanafunzi wengi nchini.

Uhaba wa walimu, uchache wa vitabu vya kiada pamoja na mrundikano wa wanafunzi wengi katika darasa moja nako pia kunaelezwa kuchangia kwa namna moja ama nyingine wanafunzi kushindwa kupata uelewa wa masomo vizuri.

Hizo ni baadhi ya changamoto ambazo zimekuwa ni kikwazo kikubwa katika sekta ya elimu hapa nchini hususani katika maeneo ya pembezoni ndio yameonekana kuwapo kwa matatizo zaidi.

Shule ya Msingi Mgila iliyopo katika Kijiji cha Mgila, Kata ya Kwashemshi, wilayani Korogwe ni moja ya shule kongwe inayokabiliwa na uchakavu wa majengo.

Shule hiyo ambayo ilisajiliwa mwaka 1965 ikiwa na vyumba saba vya madarasa pamoja na ofisi mbili za walimu huku ikiwa na walimu nane pekee ambao wanalazimka kufundisha darasa la kwanza hadi la saba.

Huku shule hiyo ikiwa na jumla ya wanafunzi 681 ambao idadi yao haiendani na uwiano wa walimu waliopo katika kuhakikisha wanapata elimu inayostahiki.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Joel Mshuza anasema kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi, walimu hulazimika kufundisha kwa awamu ili kuhakikisha kila mwanafunzi anaelewa kile kinachofundishwa.

“Unaweza kukuta darasa lina wanafunzi 168 sasa ili kuhakikisha wote wanaelewa ndipo mwalimu hulazimika kugawa, kundi moja kulitoa nje na kubaki na moja ndani, hali ambayo huathiri kiwango cha ufundishaji,”amebainisha mwalimu mkuu huyo.

Hali hiyo ya mrundikano wa wanafunzi katika darasa moja wakati mwingine husababisha dawati moja kukaliwa na wanafunzi kati ya wanne hadi watano, kutegemea na maumbile yao.

“Hali hiyo inachangia kumuathiri mwanafunzi kisaikolojia kwani huanza kujihisi kama amebaguliwa lakini mwalimu naye inambidi atumie muda mwingi kwa ajili ya kufundisha somo moja mpaka liweze

kueleweka,”anabainisha mwalimu huyo.

Hata hivyo, licha ya uchache wa walimu shuleni hapo, pia kuna changamoto ya uchakavu wa majengo hususani vyumba vya madarasa hali inayotishia usalama wa wanafunzi.

Anasema vyumba vilivyopo ni saba pekee hivyo husababisha wanafunzi kurundikana katika darasa moja kwa ajili ya kupata taaluma yao hususani katika msimu wa mvua.

“Kutokana na uchakavu wa madarasa, tunalazimika darasa moja kukaliwa na wanafunzi 168, ambapo uwiano wao ni sawa na wanafunzi wa madarasa mawili,” anasema Mshuza.

Anasema hali ya vyumba ni ya kusikitisha kwani vingi vinanyufa ukutani huku vingine vikiwa vinahitaji kuezekwa mabati mapya kwa kuwa yaliyopo yamejaa matundu.

“Wakati wa msimu wa mvua hali huwa ni mbaya zaidi hivyo tunalazimika kuwafundisha kwa tahadhari, yale madarasa yenye nyufa nyingi “Hatuyatumii tunayafunga kwa muda ili kujiepusha na madhara ya kuangukiwa na kuta,” anasema.

Kuhusu wanafunzi wa darasa la awali, anasema huwa wanalazimika kuwafundisha kwenye banda walilolijenga kwa miti ili kuepuka madhara kwa wanafunzi hao.

Naye Mwalimu wa taaluma, Faraja Jonathan anasema wakati wa mvua huwa wanafundisha kwa wasiwasi kwani madarasa mengi yanavuja.

“Unakuta darasa linavuja upande mmoja hivyo tunalazimika kuwahamishia upande mwingine wa darasa ambako nako unaomba Mungu mvua isiwe ya upepo mkali ikasababisha paa kuezuliwa,” anasema Jonathan.

Anasema mazingira ya kujifunzia shuleni hapo ni hatarishi kwa wanafunzi na hata walimu.

Anasema kuwa kutokana na hali hiyo inayowakabili, wanafunzi wengi wamekuwa watotoro hasa katika kipindi cha mvua.

Wengi wanahofia usalama wao kutokana na hali inavyokuwa.

“Kipindi cha mvua kwa kawaida mahudhurio huwa yanashuka hadi kufikia asilimia 89 hadi 70. Huwa tunatumia vyumba vinne pekee

Kwa ajili ya kufundishia.

“Mwaka 2014 mvua za masika zilisababisha madarasa mawili kudondoka, ambayo yalikuwa yakitumiwa na wanafunzi wa darasa la nne na la tatu, bahati nzuri haikuwa siku ya shule,” anabainisha mwalimu huyo.

Hata hivyo, Waswahili wanasema kila kilio kina mwenyewe kwa kutumia nguvu za wananchi walioko katika kijiji hivyo waliweza kuchangishana na kuyajenga upya madarasa hayo yaliyoanguka.

Mwalimu Mkuu anasema kuwa licha ya vyumba hivyo kujengwa, vimeishia kwenye hatua ya umaliziaji lakini wanalazimika kuvitumia kutokana na uchache wa madarasa.

Joyce Joseph ni mwanafunzi wa darasa la saba katika shule hiyo, anasema uchakavu wa vyumba vya madarasa unawapa wakati mgumu kupata elimu wanayoihitaji.

Anasema changamoto kubwa huipata wakati wa mvua kwani mabati huwa yanagongana hivyo kusababisha kutokuwapo na usikivu darasani.

“Tunaiomba Serikali itusaidia kutujengea vyumba vipya vya madarasa ili tuweze kujifunza vizuri kwa utulivu hatimaye kuongeza kiwango cha ufaulu.

Naye mwanafunzi, Merina Emily anasema ni vema Serikali ikawajengea shule nyingine kwani hii iliyopo ni chakavu mno hivyo inahitajimarekebisho makubwa.

Anasema majengo mengi ni ya zamani hivyo yanahitaji ukarabati kwani bila hivyo wanaweza kupata maafa ya kuangukiwa na kuta kama hakutafanyika ukarabati wa haraka.

Hata hivyo, wazazi wa wanafunzi shuleni hapo wameshaanzisha mchango wa hiari kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo.

Lilian Michael ni mjumbe wa kamati ya ujenzi, anasema kuwa lengo lao ni kujenga vyumba vipya vitano kwa awamu ya kwanza katika eneo hilo la shule.

Anasema vyumba hivyo vitakapokamilika vitaweza kumaliza tatizo la uchakavu wa majengo hivyo watoto wao wataweza kusomakatika mazingira mazuri.

“Tayari tumeshachimba msingi na tumepeana majukumu mbalimbali. Wazazi ambao hawana uwezo kazi yao itakuwa ni kukusanya mawe kwa ajili ya ujenzi huku wengine wakichangia gharama za kununulia vifaa,” anasema mzazi huyo.

Anasema mpaka sasa wazazi wamechangia Sh 800,000 huku wafadhili wanaoishi nje ya kijiji hicho wamechangia Sh milioni 1.6 za kuanzia ujenzi huo.

Anasema wamefanikiwa kupeleka ombi kwa mkuu wa wilaya kuhusu changamoto inayowakabili na hatua walizoweza kuzichukuwaili kukabiliana nayo.

“Tunashukuru Mkuu wa wilaya aliweza kutembelea shule yetu na kujionea hali halisi ya uchakavu wa majengo, ametuahidi kutuongezeanguvu ili ujenzi wake ukamilike kabla ya mwakani,” anasema Michael.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here