23.3 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

UCHAGUZI MKUU DRC: RAIS KABILA ANG’OA SURA ABAKIZA KIVULI

MARKUS MPANGALA NA MTANDAO                |                


UAMUZI wa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Joseph Kabila kutogombea  nafasi hiyo katika Uchaguzi Mkuu  ujao unaotarajiwa kufanyika Desemba 23, mwaka huu unaonekana kushusha joto la kisiasa nchini humo.

Mazingira ya kushuka kwa joto la kisiasa nchini humo yanatokana na kile kinachoelezwa na wachambuzi wa masuala ya kisiasa kuwa uamuzi aliouchukuwa Rais Kabila umeshusha kwa kiasi kikubwa mihemuko hasi iliyokuwa imetawala vichwa vya wengi kuelekea uchaguzi ujao ambapo hali ya sintofahamu kuhusu kiongozi huyo kama atagombea au la.. ilionekana kuwavuruga wananchi wengi.

Rais Kabila amevunja ukimya baada ya kudhihirisha kuwa hatagombea tena nafasi hiyo. Licha ya kutoa uamuzi huo hata hivyo Rais Kabila ameonyesha sura nyingine ya demokrasia tofauti na ilivyodhaniwa kuwa atang’ang’ania madaraka kama ilivyokuwa awali.

Wakati msemaji wa Rais Kabila, Lambert Mende alipotangaza suala hilo ilikuwa kama ndoto lakini taratibu ukweli unadhihirika kuwa hana mpango wa kugombea tena na amemwachia kijiti Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani, Emmanuel Shadary kupeperusha bendera ya muungano wa chama tawala.

Kwa mujibu wa Katiba ya nchi hiyo Rais Kabila alitakiwa kuachia madaraka mwaka 2016 baada ya kumalizika kipindi chake, lakini amedumu kwa miaka miwili kutokana na mgogoro wa uchaguzi pamoja na majaribio ya kutaka kugombea tena nafasi hiyo.

Sintofahamu iliyokuwapo nchini humo ilisababisha maandamano na machafuko yaliyosababishwa na mapambano kati ya waandamanaji na polisi.

Hata hivyo Kabila amepitia shinikizo kubwa la kumtaka aachie ngazi kutoka nchi jirani ya Angola, mataifa ya Jumuiya ya Ulaya na Marekani pamoja na maandamano ya Maaskofu wa Kanisa Katoliki.

Rais Kabila amejibu mapigo?

Duru za kisiasa zinasema zipo sababu mbalimbali zilizomsukuma Rais Kabila kutogombea tena, mbali ya kumalizika muda wake sababu nyingine ni kuepusha vita vya wenyewe kwa wenyewe, machafuko  na migogoro katika ukanda wa maziwa makuu ambayo yangetokea kama angetangaza nia ya kuendelea na wadhifa huo.

Kubwa zaidi la kumteua Shadary mwenye umri wa miaka 57 ni kujibu mapigo kwani mteule huyo amewekewa vikwazo na Jumuiya ya Ulaya kwa madai ya kuhusika katika uvunjaji wa haki za binadamu baada ya kuamuru jeshi kupambana na waandamanaji.

Duru hizo zinasema Rais Kabila anataka kushiriki siasa za nchi yake kwa ‘kuongoza kutoka nyuma ya pazia’ huku akiwa amemtanguliza Shadary. Kwa maana hiyo kutangaza kutogombea ni kuuhadaa umma, badala yake kivuli chake kitaendelea kuongoza.

Ikumbukwe kuwa Rais Kabila ataendelea na wadhifa wake wa Mwenyekiti wa Chama tawala cha People’s Party for Reconstruction and Democracy (PPRD) ambako amedaiwa kupanga safu ya watu watiifu kwake.

Akizungumza na mtandao wa Televisheni ya CNBCAfrica kuhusu uamuzi wa Rais Kabila kutogombea, Seneta Jacques Ndjoli kutoka chama cha upinzani cha MLC amesema; “Bila kujali kinachoendelea kwa sasa, Katiba ya nchi yetu imeheshimiwa sana, ni jambo la kujivunia. Licha ya majaribio kadhaa ya kuvunja Katiba, Rais Kabila ameelewa na kukiri nafasi ya Katiba katika ujenzi wa nchi, kwamba sheria inamhusu kila mmoja,”

MCL ni chama cha makamu wa zamani wa rais wa nchi hiyo na mgombea wa urais wa chama hicho mwaka huu, ni Jean-Pierre Bemba.

Kwa upande wake Emmanuel Shadary tayari amewasilisha stakabadhi zake za kuwania urais kwa Tume Huru ya Uchaguzi DRC (CENI). Kabla ya uteuzi huo,  Shadary alikuwa Katibu wa Kudumu wa Chama tawala cha PPRD na mtu muhimu wa kampeni za Rais Kabila.

Shirika la haki za binadamu la Human Rights Watch linamuhusisha Shadary na matumizi mabaya ya vyombo vya dola ambapo anadaiwa kuvitumia kuwakamata  viongozi wa upinzani, wafuasi wao pamoja na wanaharakati wa haki za binadamu nchini humo.

Uteuzi wa Shadary umenyamazisha minong’ono ya kuteuliwa wanasiasa wengine akiwamo Augustin Matata Ponyo (Waziri Mkuu wa zamani), Nehemie Mwilanya Wilondja ( Mkuu wa Watumishi wa Rais) na Aubin Minaku (Rais wa Bunge la Taifa).

Jamhuri wa Demokrasia ya Kongo yenye takribani watu milioni 80 haijawahi kuona makabidhiano ya amani ya madaraka tangu ipate uhuru wake mwaka 1960.

Joseph Kabila mwenye umri wa miaka 47 sasa alichukua madaraka kutoka kwa baba yake Laurent-Desire Kabila, ambaye aliuawa na mlinzi wake.

Muda wake wa uongozi unatajwa kukumbwa na matukio mengi ukiwamo ufisadi, kutokuwepo usawa pamoja na ghasia za kisiasa.

Mwaka 2016 Shirika la Transparency International liliiorodhesha DRC namba 156 kati 176 ya nchi zenye ufisadi zaidi duniani.

Mikoa mingi ya taifa hilo imekumbwa na mizozo huku mamilioni ya watu wamekimbia makazi yao na kuwa wakimbizi katika nchi za  Uganda, Tanzania, Angola na Zambia.

Marekani yampongeza Kabila

Uamuzi wa kutogombea urais pia umepongezwa na Serikali ya Marekani ambayo mara kadhaa ilikuwa ikimkosoa na kumtaka Kabila aheshimu Katiba.

“Tumevutiwa na uamuzi wa Rais Kabila, kubainisha kuwa hana mpango wa kugombea na ameheshimu Katiba ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na makubaliano ya kutowania kipindi cha tatu. Wananchi wanatakiwa kuwa huru kutoa maoni yao na kuchagua wagombea wanaowataka bila vitisho vyovyote. Tuinaomba pia tume ya uchaguzi na mamlaka zinazohusika kusimamia kwa uhuru na uwazi,” anasema Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Heather Nauert.

Mfahamu mteule wa Kabila

Emmanuel Shadary ni mzaliwa wa Mji wa Kasongo uliopo Mkoa wa Maniema Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Alizaliwa Novemba 29, mwaka 1960.

Alipata shahada ya Chuo Kikuu cha Lubumbashi katika masomo ya uongozi na sayansi ya siasa.

Alijiunga katika Chuo Kikuu cha Kinshasa kukamilisha masomo yake ya awamu ya tatu ya sayansi ya siasa na uongozi. Amekuwa akisomea shahada ya udaktari tangu 2015.

Shadary ni baba ya watoto wanane. Amewahi kuwa Naibu na Mkurugenzi Mkuu wa Elimu ya Juu, pamoja na kuwa mwanaharakati wa mashirika ya kijamii mkoani Maniema.

Mwaka 1998 hadi 2001 alikuwa Naibu Gavana wa Jimbo la Maniema chini ya usimamizi wa Rais Laurent Desire Kabila.

Mwaka 2002 alishiriki kuanzisha chama cha PPRD. Tangu mwaka 2005 hadi 2015 alikuwa katibu mkuu anayesimamia masuala ya uchaguzi na nidhamu.

Pia amewahi kuwa mkurugenzi wa kampeni za urais za Joseph Kabila katika Mkoa Maniema.

Aliwahi kuwa Makamu wa Rais wa Tume ya PAJ bungeni kati ya mwaka 2006-2011, kabla ya kuchukua uongozi wa chama cha PPRD bungeni mbali na kuwa mshirikishi wa wabunge walio wengi katika Bunge hilo hadi sasa.

Mei 17, 2015, aliteuliwa na Rais Joseph Kabila kuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama cha PPRD.

Shadary ni raia wa Rwanda au DRC?

Mara baada ya Emmanuel Shadary kutangazwa kuwa mrithi wa Rais Kabila, kumezuka minong’ono kuwa si raia halali wa DRC badala yake anaasili ya Kabila la Kitutsi kutoka nchini Rwanda.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kilimo Cha Sokoine (SUA) na mchambuzi wa masuala ya siasa ndani na nje, Richard Ngaya anasema; “Kwanza Shadary ni mwanasiasa halali wa DRC. Wanamuonea pale wanapomtuhumu ni mtu kutoka Rwanda hata kama wazazi wake wote wawili wangetoka huko, yeye atabaki kuwa raia wa DRC wa kuzaliwa na naamini alifuata taratibu zote kuupata uraia huo.

“Ni kweli mama yake anatoka Rwanda, lakini kutoka Rwanda wala haimfanyi kuwa kibaraka wa Kabila kama wanavyotaka tuelewe.

Anaongeza kwa kusema “Anaweza kuwa kibaraka kweli, lakini hakuna sababu yoyote ya kutumia historia ya mama yake kama njia ya kumkataa. Kama atashindwa kuiongoza DRC itatokana na udhaifu wake na atawaangusha wananchi wake si kwa sababu ya asili ya mama yake. DRC wanaweza kuweka historia mpya ya kidemokrasia, sababu hizi si zama za mitutu tena.”

Naibu Katibu Mtendaji wa Chama tawala cha PPRD, Ferdinand Kambere, amesema uteuzi wa Shadary ni alama ya ushujaa wa demokrasia nchini.

Kwa upande wake upinzani umelezea kwamba uteuzi wa mgombea wa chama tawala, ni hatua ya ushindi wa demokrasia, lakini wametarajia mageuzi wakati wa uchaguzi.

Martin Fayulu ambaye ni mgombea wa vuguvugu Dynamique de l’opposition amesema raia ndio wanaotakiwa kuamua kupitia uchaguzi huru.

Hata hivyo amesema hawana maoni yeyote kufuatia uteuzi huo wa mrithi wa Kabila, na kwamba ni mambo yao ya ndani, kwa kuwa Kabila anajua umuhimu wa uamuzi wake.

Amesema ikiwa amepanga njama ya kurejea madarakani baadaye kama alivyofanya Rais wa Urusi Vladimir Putin na Waziri Mkuu Dmitry Medvedev hilo ni haki yake, lakini akionya kwamba wanachotaka uwepo wa uchaguzi huru, wa wazi na wa kidemokrasia ilikuruhusu raia wa Kongo kujichagulia viongozi wao

wenyewe.

Gharama za fomu zatia fora

Licha ya fomu ya kuwania urais

kuuzwa bei ya juu ya Dola za Marekani 100,000 sawa na Sh milioni 224, hata hivyo wagombea 26 wamejitokeza kuwania wadhifa huo.

Gharama gizo zimefahamika siku moja baada ya Rais Kabila kutangaza kuachia ngazi, huku -CENI ikitangaza orodha hiyo

ndefu ya wagombea nchini humo.

Miongoni mwa wagombea hao ni wanawake watatu na mawaziri wakuu wa zamani watatu, wagombea huru wakiwa 16 na wa vyama vya upinzani wanane.

Uchaguzi huo wa duru moja pekee umeorodhesha wagombea mara mbili zaidi kuliko ule wa mwaka 2011. Agosti 8, mwaka huu ambayo ilikuwa siku ya mwisho kwa wagombea kuwasilisha majina yao, walijitokeza 18 pekee akiwamo Shadary.

Katika maelezo yake Waziri huyo wa mambo ya ndani wa zamani amesema akichaguliwa atahakikisha wananchi wanaishi kwa amani na hali yao ya maisha kuboreka.

Washindani wa Shadary:

Wagombea ambao tayari wametangaza kuwania urais ni Jean-Pierre Bemba (55) kwa tiketi ya chama cha MCL. Bemba ni mbabe wa zamani wa vita na hasimu mkubwa wa Rais Kabila ambaye alirejea nchini DRC wiki iliyopita baada ya kufutiwa mashtaka ya uhalifu wa kivita na mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ya huko Hague nchini Uholanzi.

Mgombea mwingine wa upinzani ni Felix Tshisekedi, kiongozi wa Chama cha Union for Democracy and Social Progress (UDPS), naye aliwasilisha fomu yake Agosti 7, mwaka huu.

Mgombea mwingine ni mgombea binafsi Tryphon Kin-Kiey Mulumba ambaye amewahi kuwa msemaji wa Mobutu Sese Seko na waziri wa zamani katika Serikali ya Rais Kabila.

Mfanyabiashara na gavana wa zamani wa Jimbo la Katanga, Moise Katumbi (53), alizuiwa mwishoni mwa wiki iliyopita na mamlaka kuwasilisha fomu yake ya kuwania urais. Katumbi amekuwa akiishi nchini uhamishoni tangu Mei mwaka 2016 baada ya kutofautiana na Kabila.

Wagombea wengine ni Monique Mukuma, Antoine Gizenga (waziri mkuu wa zamani), pamoja na wengine 26 watachuana kumrithi Rais Kabila kwenye uchaguzi mkuu ujao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles