23.8 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

DK. BASHIRU: UPEPO WA 2015 ULIKUWA NA MAPEPO YALIYOTIKISA MISINGI YA UTAIFA

Na ELIYA MBONEA-MONDULI


KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally, amesema upepo uliovuma mwaka 2015 ulikuwa na mapepo yaliyotikisa misingi ya utaifa.

Akizungumza na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM ya Wilaya ya Monduli mjini hapa jana, aliwaambia kuwa wameweka ngome wilayani hapa ya kukihuisha chama hicho na hasa kuimarisha zaidi misingi ya Azimio la Arusha.

“Mwaka 2015 ndiyo wakati wanasiasa waliofilisika walianza kutafuta madaraka na tangu hapo taifa halijapona, na upepo uliovuma ulikuwa upepo wa mapepo,” alisema na kuongeza:

“Tulianza kuvurugika na kuvurugana kama taifa na si CCM, ndiyo wakati ambao wanasiasa uchwara waliofilisika kiitikadi na kisiasa walianza kutumia mbinu chafu kutafuta madaraka.

“Na tangu hapo nchi yetu haijapona, tunayo kazi ya kufanya, kurejesha misingi ya kitaifa ili watu wa aina hiyo wasitokane na kizazi cha Watanzania tena.

“Kwa hiyo wanapotokea vijana kama kina Kalanga kurejea katika misingi ya chama chetu, wanakuwa wanatuma ujumbe kwa vijana wenzao kwamba taifa hili linahitaji vijana watakaosimamia misingi imara.

“Kwa Monduli, upepo mwanana umeanza kuvuma, nami nakubaliana na mwenyekiti wa mkoa kwamba kunavuma upepo mwanana na upepo huu utasambaa nchi nzima Tanzania Bara na Zanzibar ili chama hiki kiendelee kupendwa na kuwavutia wanyonge.

“Tulieni msiogope upepo huu, kuna wengine wameanza kulalamika Kalanga (Julius Kalanga, aliyekuwa mbunge wa Chadema aliyehamia CCM) alikimbia usiku, sasa mapambano unayachagulia muda wa kupigana?

“Tutapiga mchana, usiku, wakati wa kiangazi na wakati wa mvua, hapa ni kazi tu. Ni suala la hesabu wakati wao wamelala, wewe shambulia. Hakuna taratibu zilizokiukwa bali ulikuwa ni mkakati wa jemedari.”

Alisema mashambulizi ya kuhama kwa Kalanga yalipangwa usiku na mchana na hivyo yeye aliamua kutangaza ushindi usiku na hao wanaosema ni mwoga hawajui wanachosema.

“Nimpongeze Kalanga, ujasiri wa kurejea CCM tena ukitokea Monduli si kazi rahisi kama mnavyofikiria, upinzani misingi yake imetikisika, wamerudi wengi.

“Lakini Monduli kuna historia yake, kwa hiyo unaporejea CCM ndani ya Monduli unakuwa umerudisha uhai na heshima ya CCM kwa taifa zima kwa sababu tuna historia hapa.

“Umetupa heshima kubwa na sisi tunakuahidi tupo nyuma yako katika mapambano yanayokuja kurejesha jimbo hili kwa chama tawala,” alisema.

 

MWENYEKITI CCM MKOA

Awali kabla ya kumkaribisha Dk. Bashiru kuzungumza, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Loota Sanare, alikiri kutikiswa na kupata misukosuko mwaka 2015.

“Lowassa, tulimpenda sana, tunamtaka bado aje huku nyumbani, tulimwambia asubiri lakini alitokea dirishani, tunawapongeza madiwani wote na mbunge aliyerudi,” alisema.

RC ARUSHA

Akipongeza uamuzi huo wa Kalanga, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, alisema mwanasiasa huyo ni mtu safi.

“Nikuahidi katibu mkuu, tutapigana ili kuhakikisha Jimbo la Monduli linabaki CCM, hivyo Kalanga ninakuomba usijutie uamuzi wako wa kurudi CCM,” alisema Gambo.

KALANGA

Akizungumza katika mkutano huo, Kalanga aliyechukua fomu ya kugombea tena ubunge kupitia CCM, alishukuru kurudi nyumbani kwa sababu alikokuwa hakuwa akiwatumikia wananchi.

“Uamuzi wa kurudi ulikuwa mgumu, lakini nimefanya uamuzi, nimekataa kuwa sehemu ya kuwagawanya wananchi wa Monduli. Niliamua kuwa moto ili niunge mkono juhudi za Rais John Magufuli na si kuwa vuguvugu.

“Nilikuwa mbunge wa mshahara, sikuwa na sauti nikiwapigania wananchi, Serikali hainisikii wala kutelekeza,” alisema.

MGOGORO WA VIONGOZI ARUSHA

Katika hatua nyingine, Dk. Bashiru, alisema viongozi wa Serikali wa Mkoa wa Arusha na CCM Mkoa, wamemuahidi kuanza kujenga ushirikiano miongoni mwao baada ya kutofautiana.

“Nimewataka wawe wanatumiana ujumbe mfupi wa kusalimiana na mimewaambia hakuna kuitana mkuu wala mimi sitaki waniite mkuu, ukuu nautoa wapi mimi?

“Tumianeni ujumbe mfupi ‘RC, mambo vipi, leo tuna Nanenane twende’. Nimeshangaa juzi hapa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha huna habari za kufanyika kwa maonyesho ya Nanenane.

“Wakati waziri yuko hapa ametoka Dar es Salaam, nimekutana naye hapa, namuuliza mwenyekiti wangu unajua habari ya Nanenane, hajui, kiongozi mkubwa wa chama mkoa hana habari?

“Vipimo vya kuwa daraja la chini ndiyo hivyo, maana yake watu wengine wanaweza kusema umetumia vigezo gani, ndiyo hivyo. Hawa viongozi hawaalikani, hawasalimiani, hawashirikiani, wana makundi.

“Kundi la huyu halina ushirikiano na kundi la huyu na ugomvi huo upo pia kwenye Jumuiya ya Wazazi Mkoa (UWT), Mwenyekiti wa UWT upo hapa, komeni kuwagawa wanachama.

“Hiki si chama chenu wala si chama cha viongozi, ni chama cha wanachama, huu ni utaratibu ambao haujazoeleka kuambizana ukweli hadharani, tusifiane hadharani, tukosoane hadharani,” alisema Dk. Bashiru.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles