31.9 C
Dar es Salaam
Monday, December 5, 2022

Contact us: [email protected]

‘Tunahitaji sheria atakayowawajibisha wanaotelekeza wazazi’

Mratibu wa Shirika la Sakila Hope for Elderly ,Hamphurey Mafie wakati wa mahojiano na mwandishi wa makala hii.
Mratibu wa Shirika la Sakila Hope for Elderly ,Hamphurey Mafie wakati wa mahojiano na mwandishi wa makala hii.

Na Mary Mwita, Arumeru

WAZEE ni hazina katika Taifa lolote duniani na kwa kutambua umuhimu wao tayari Serikali na wadau wanafanya jitihada kuhakikisha kuwa wanapata mahitaji ya msingi pamoja na kushirikishwa katika maendeleo ya nchi.

Tangu nchi yetu ilipopata Uhuru wake mwaka 1961 haja ya kuwa na mwongozo wa kitaifa kama dira ya kuelekeza huduma kwa wazee ilibainika.

Ilidhihirika waziwazi kuwa huduma zilizokuwa zikitolewa kwa wazee zilihitaji kuwekewa malengo na utaratibu mzuri ili walengwa waweze kunufaika kwa kuzingatia matarajio yao.

Mwaka 1982 Umoja wa Mataifa ulitoa mpango wa kimataifa wa utekelezaji ikiwa ni dira ya kimataifa ya utoaji huduma na ushirikishwaji wa wazee katika maendeleo yao na ya jamii kwa ujumla.

Mpango huu wa Kimataifa ulifanyiwa mapitio mwaka 2002 kwa lengo la kuainisha matatizo na mahitaji ya wazee katika karne ya 21.

Katika kuadhimisha Mwaka wa Kimataifa wa Wazee (1999), Serikali iliamua kuwa na Sera ya Taifa ya Wazee.

Maamuzi ya kuwa na Sera ni kielelezo cha dhamira ya Serikali ya kuweka masuala ya wazee katika agenda ya maendeleo ya nchi.

Pamoja na sera hiyo kuwepo wazee bado wanakabiliwa na matatizo mbalimbali ikiwa ni pamoja na umaskini, huduma finyu za afya na pensheni.

Aidha Wazee wanalalamika kuwa hawashirikishwi katika maamuzi muhimu yanayohusu maendeleo ya nchi hali inayofanya matatizo yao kushindwa kupewa kipawa mbele.

Mmomonyoko wa maadili katika jamii pia umewaathiri wazee wengi kwa kuwa vijana wamepoteza ari ya kuwatunza wazee kutokana na kuiga ustaarabu wa Kigeni.

Ingawa wazee hao wanapitia changamoto lukuki ukweli unabaki kuwa wazee ni rasilimali muhimu katika maendeleo ya nchi, kutokana na ukweli huo wazee hawana budi kutambuliwa na kupatiwa fursa ya kushiriki katika shughuli za maendeleo ya nchi kama ilivyo kwa makundi mengine.

Wadau wa kutetea haki za wazee wapo mstari wa mbele kuhakikisha kuwa wazee wanapatiwa mahitaji ya msingi na kuendelea kuishi na kuhudumia jamii zao.

Miongoni mwa wadau hao ni Shirika lisilo la Kiserikali la Sakila Hope For Eldery, liliopo katika Kitongoji cha Surumala kijiji cha Kikatiki,Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha.

Mratibu wa Shirika hilo, Humphery Mafie, anasema lilianza kuhudumia wazee mwaka 2004 kwa kushirikiana na Kanisa la International Evangalism Church, lililopo Kilombero ambapo walianza kuhudumia wazee 20.

Mafie anasema wamefanikiwa kuhudumia wazee 368 na kwa sasa wanahudumia wazee 280 baada ya wengine kufariki kutokana na umri na maradhi mbalimbali.

“Tulivyoanza huduma hii hatukujua kama katika Wilaya ya Arumeru kuna kundi kubwa la wazee ambao wana mahitaji ya msingi kama vile chakula, malazi na mavazi. Tumeshangaa baada ya kuanza kuwahudumia tumepata kundi kubwa kama unavyoona mwenyewe.

“Wazee hawa tunawapatia huduma ya chakula kila mwezi na kwa kweli tumeona afya zao zikiimarika baada ya kuanza kupata chakula ingawa hakitoshelezi,” anasema Mafie.

Pamoja na mambo mengine anasema kuwa wamefanikiwa kujenga makazi ya wazee na kuwa tayari wazee 13 wanahudumiwa katika kambi ya wazee.

Anataja mafanikio mengine kuwa wamefanikiwa kuwawezesha kupata huduma za afya, kuwachangia katika miradi ya kujikimu na kukarabati nyumba za wazee 42.

Aidha, wazee wameweza kupatiwa mbuzi na kondoo wapatao 50 na kufanya safari za kitalii mara moja kila mwaka.

Mafie anasema pamoja na mafanikio hayo wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo ni uhaba wa fedha za ujenzi kwa ajili ya kujenga jiko na ukumbi mdogo ambapo zinahitajika Sh milioni 25.

Anataja changamoto nyingine kuwa ni gari la usafiri kwa ajili ya kuwachukua wazee kutoka katika makazi yao, uhaba wa maji ambapo anaomba wasamaria kuwasaidia ili waweze kuvuna maji.

“Wazee hawa wanatumia zaidi ya Sh milioni nane kwa mwezi, na sisi hatuna kipato cha kuwasaidia zaidi ya wasamaria kujitokeza kuwasaidia. Kati ya wazee hawa wanaokaa katika makazi haya, zaidi ya 10 wanahitaji huduma za msingi kila siku na wengine zaidi ya 200 wanaokaa majumbani.

“Tunawatembelea na kuwapatia huduma za msingi lakini uwezo ni mdogo hivyo tunaomba wadau wajitokeze kutusaidia,” anasema Mafie.

Mafie anasema wanakabiliwa na uhaba wa fedha za kuwanunulia wazee hao chakula kutokana na kuwa na idadi yao kuwa kubwa na kutaka wadau wa maendeleo kujitokeza kuwasaidia.

Kwa upande wake Mchungaji Amos Baruti, ambaye ni mwanzilishi wa huduma hiyo, anasema imekuwa ni msaada mkubwa kwa wazee hao kwa kuwa wanapata chakula na hivyo kuwa na afya bora.

Anasema mahitaji wanayopata wazee hayatoshelezi na kuomba Serikali kuwasaidia wazee hao kama sera ya wazee inavyoelekeza ikiwa ni pamoja na kuwapatia matibabu.

Mchungaji huyo anawakumbusha vijana kurudia desturi za kiafrika za kuwatunza wazee na kuacha mila mbaya za kigeni na kusisitiza kuwa maandiko matakatifu yanahimiza kuwaheshimu wazazi.

Bakari Juma (45) mkazi wa Usa River, Wilaya ya Arumeru, anasema hali ya kuwapa wazee kisogo katika jamii haina budi kukemewa na ikiwezekana Serikali iwawajibishe watoto wanaotelekeza wazazi wao.

“Kuwe na sheria itakayomwajibisha yule ambaye ana uwezo lakini anashindwa kumtunza mzazi wake, wanaiga ustaarabu wa kigeni huo ni upuuzi, kila mtu mwenye uwezo awajibike kwa wazazi wake. Mimi naona aibu baba yangu kutunzwa na wasamaria wakati nina uwezo wa kumtunza,” anasema Juma.

Geofrey Petro mkazi wa Sakila, anasifu jitihada za wadau wanaotetea haki za wazee na kusisitiza kuwa uzee unaweza kumpata kila mtu hivyo ni vyema jamii na vijana wakatambua hilo na kuwatunza wazee.

“Unajua baadhi ya wazee wastaafu ambao hawana kipato chochote wanafariki kabla ya muda wao kwa kukosa matunzo bora, hii ni laana na tusipokemea itaathiri hata watoto wetu.

“Jambo la ajabu kuna vijana wanawaachia wazee jukumu la kulea wajukuu huku wakijua hawana kipato cha kuwatunza, kwa kweli jamii isiendelee kukumbatia hali hii, wahusika wachukuliwe hatua pindi wanapobainika kuwa wanawanyanyasa wazee,” anasema Petro.

Petro anasema kutokana na hali ngumu ya maisha vijana wamewapa kisogo wazazi wao kwa kuwa baadhi wanapangisha katika miji mbalimbali na wanashindwa kukaa nao na kudai kuwa jukumu la kuwatunza wazee linatakiwa kuwa la jamii nzima.

Ndetaula Palllanyo (89) ni miongoni mwa wazee wanaopatiwa mahitaji ya msingi na shirika hilo, anasema tangu aanze kuhudumiwa na shirika hilo afya yake imeimarika na anatarajia kuishi miaka 100.

“Nina matumaini mapya hasa ninapokutana na wazee wenzangu kituoni hapa, ninaona kuna maisha mapya kwa kuwa tunafurahi na kucheza na hata kutembezwa katika mbuga za wanyama ,”anasema Mzee Pallangyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,586FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles