30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Mazoezi salama kwa wajawazito

pilates2-1

WATU wengi wanaamini kwamba ujauzito ni sababu ya mapumziko, kula kupita kiasi na kutokufanya kazi kabisa. Ukizungumzia mazoezi, ndiyo kabisa–wengi wetu bado tunaamini kwamba mjamzito hatakiwi kabisa kufanya mazoezi.

Tofauti na imani hii, tafiti zinaonyesha kwamba ukosefu wa mazoezi wakati wa ujauzito ni sababu mojawapo inayochangia matatizo mbalimbali ya kiafya. Matatizo hayo ni pamoja na magonjwa kama vile kisukari cha mimba, kifafa cha mimba, kuchukua muda mrefu katika kujifungua na hata kuharibika kwa mimba.

Utafiti uliofanyika hivi karibuni hapa nchini, umebaini kwamba liko ongezeko kubwa la tatizo la kisukari cha mimba (gastational diabetes mellitus) katika maeneo ya mijini–sababu mojawapo ya ongezeko hilo ikiwa ni ukosefu wa mazoezi ya kutosha kabla na wakati wa ujauzito. Hii inamaanisha kwamba mazoezi au kujishughulisha ni kitu muhimu hata wakati wa ujauzito.

Pamoja na ufahamu huo, swali linabakia pale pale–ni mazoezi gani yaliyosalama na yenye faida wakati wa ujauzito?

MAANA YA MAZOEZI

Ikumbukwe kwamba, mazoezi si kwenda gym na kushiriki michezo peke yake. Mazoezi yanahusisha shughuli zozote za mwili, zinazotumia misuli na kuufanya mwili kutumia nguvu. Kwa maana hiyo, mazoezi yanahusisha shughuli za nyumbani na kazini kama vile kupanda ngazi, mazoezi wakati wa usafiri kama vile kutembea na kuendesha baiskeli na mazoezi yanayofanyika katika muda maalumu kama vile michezo na kwenda katika sehemu maalumu za kufanyia mazoezi (gym).

MAZOEZI/SHUGHULI ZILIZO SALAMA WAKATI WA UJAUZITO

Unapokuwa mjamzito, endelea kufanya shughuli zako za kila siku kama kawaida. Shughuli kama kucheza mziki, kutembea kwenda dukani na hata kukimbia mchaka mchaka ni salama kabisa. Mazoezi si hatari kwa ujauzito.

Mazoezi ya taratibu kama yoga ni mazuri mno wakati wa ujauzito na hayana hatari yoyote. Kuogelea au kucheza katika maji ni mojawapo ya mazoezi yanayoshauriwa wakati wa ujauzito. Mazoezi mengine ni pamoja na kutumia mashine mbalimbali za mazoezi kama zile za mikono, miguu na mabega. Kupanda ngazi za gorofa pia ni mazoezi mazuri kwa mjamzito.

Unapofanya mazoezi wakati wa ujauzito zingatia yafuatayo:

  1. Usijichoshe

Kama ulikuwa mtu wa mazoezi kabla ya ujauzito, punguza kidogo kiwango cha mazoezi–ila usiache. Huna haja ya kufanya mazoezi mpaka kuchoka. Katika miezi ya mwanzo ya ujauzito, unaweza kufanya mazoezi ya nguvu kidogo, lakini ni vema kupunguza kiwango kadri umri wa mimba unavyoongezeka.

Kwa urahisi wa kuelewa, hakikisha unaouwezo wa kuzungumza na mtu wakati unafanya mazoezi. Kama mazoezi unayofanya yanakufanya kukosa pumzi unapokuwa unazungumza–inawezekana kabisa unazidisha kiwango cha mazoezi hayo.

Kama hukuwa mtu wa mazoezi kabla ya ujauzito, usianze ghafla. Na kama utajiunga na darasa la mazoezi–iwe kuogelea, kukimbia au kucheza dansi, mfahamishe mwalimu wa mazoezi kwamba una ujauzito. Katika siku za mwanzo usizidishe zaidi ya dakika 15 za mazoezi mfululizo. Ila unaweza kuongeza hadi dakika 30 kama utazoea.

  1. Siku zote anza kwa kupasha (warm-up)

Unapofanya mazoezi kumbuka ni muhimu kupasha viungo ili kuuandaa mwili. Hii inasaidia kuzuia kuumia na kuwa na mzunguko wa damu wa kutosha wakati unafanya mazoezi.

  1. Jaribu kujishughulisha kila siku

Angalau nusu saa ya kutembea kila siku ni muhimu. Lakini kama huwezi kufikisha nusu saa–usijali, kiasi chochote cha mazoezi kina faida wakati wa ujauzito.

  1. Mazoezi ya nguvu

Kwepa kabisa kufanya mazoezi ya nguvu hususani kwenye hali ya joto.

  1. Kunywa maji mengi

Hakikisha unakunywa maji mengi pamoja na vinywaji vingine visivyokuwa na madhara kiafya.

  1. Pata mwalimu mwelewa

Unapohudhuria madarasa ya mazoezi, hakikisha unafundishwa na mwalimu mwenye weledi, uelewa mzuri wa mazoezi, ujauzito na afya kwa ujumla.

  1. Fikiria kuogelea

Kuogelea ni zoezi zuri wakati wa ujauzito kutokana na uwezo wa maji kuubeba uzito wa mimba.

MAZOEZI/SHUGHULI ZISIZO SALAMA WAKATI WA UJAUZITO

  1. Kwepa aina yeyote ya mazoezi inayokufanya kulala chali (tumbo juu mgongo chini)

Uzito wa mimba yako unaweza kukandamiza mishipa mikubwa ya damu na kuilazimisha damu kurudi kwenye moyo baadala ya kwenda katika sehemu zingine za mwili. Hii inaweza kukusababishia kizungu zungu.

  1. Epuka kugongana na watu

Usishiriki katika michezo au mazoezi yanayoweza kusababisha kugongana na watu kama vile ngumi, mpira wa kikapu na mazoezi mengine kama hayo.

3. Usiingie kwenye kina kirefu cha maji

Mjamzito anapaswa kuepuka kufanya diving (kuingia ndani kabisa ya kina kirefu cha maji).

Hii inaweza kumuathiri mtoto aliye tumboni mwako.

  1. Usifanye mazoezi juu sana

Zaidi ya mita 2500 juu ya usawa wa bahari. Hii inaweza kukusababishia wewe na mtoto madhara yatokanayo na kuwa juu zaidi

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles