23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

TUMEISIGINA MISINGI YA NYERERE, TUNAMTAFUTA MCHAWI

Na Balinagwe Mwambungu,

‘WHERE did the rain start beating us?’ Haya ni maneno ya mwandishi nguli Mnigeria, Chinua Achebe (marehemu), alipokuwa anazungumza na kaka yangu Osija Mwambungu; a.k.a Prince Kagwema (marehemu).

Chinua alikuwa amealikwa nyumbani Oysterbay, niliwatengea viti kwenye bustani.  Kaka akanieleza kwamba Chinua Achebe alikuwa mwandishi maarufu wa vitabu kutoka Nigeria. Nilikaa karibu ili nisikie mazungumzo yao. Sikujua kwamba siku moja nitakuja kumsoma Chinua Achebe hadi nilipoingia sekondari na kusoma kitabu chake, Things Fall Apart. Chinua alimhamasisha Osija

Nikagundua kuwa wote wawili walikuwa na hamasa ya kuona Bara la Afrika baada ya vua kongwa la ukoloni, linaungana na kuifanya ndoto ya ‘Afrika ni Moja’ na kuleta maendeleo kwa watu wake.

Aidha, niliwasikia wakisema kuwa viongozi wa Kiafrika baada ya kujitawala, budi wasilewe madaraka na wakasahau kuwatumikia watu wao, badala yake wanajikuta wanazama katika kuusaka utajiri na kutumia vibaya rasilimali za nchi.

Viongozi husahau kwamba kabla ya uhuru, waliahidi kupambana na ujinga, maradhi na umasikini. Hapa ndipo Chinua alipouliza: Where did the rain start beating us? Yaani mvua ilianzia kutupiga wapi?

Swali hili nimejiuliza hivi majuzi niliposikia maoni ya wadau mbalimbali wa elimu, waliokuwa wakichangia mada ya kushuka kwa elimu nchini, where did the rain start beating us? Nilijiuliza swali hili nililolisikia mwaka 1964 nikiwa darasa la nane nikiwa likizo kwa kaka yangu.

Nimekuwa najiuliza swali hili mara nyingi ninapoona mambo mengi ya nchi yetu yanakwenda visivyo. Mwalimu Julius Nyerere, Baba wa Taifa, alijenga misingi mizuri ya wapi alitaka nchi hii iende. Alikuwa na ndoto ya Tanzania yenye viwanda. Ndoto hii haitaweza kutekelezwa tusipo uangalia mfumo wetu wa elimu. Elimu, si bora elimu, bali elimu bora ndiyo msingi wa maendeleo na Mwalimu alilijua hilo.

Kabla ya kujenga viwanda, aliwasomesha vijana kwanza. Alijenga viwanda vingi vya kuchakata pamba, kutengeneza nyuzi hatimaye kutengeneza nguo. Kulikuwa na viwanda vya kutengeneza mafuta ya kula, chai, kubangua korosho, mbao na hata kiwanda cha kutengeneza viberiti.

Kulikuwa na viwanda vya ngozi na viatu, alijenga viwanda vya kutengeneza karatasi, viwanda vya kahawa na vya kusindika vyakula. Alijenga kiwanda kikubwa cha kutengeneza vipuri, Kilimanjaro Machine Tools, ambacho kilikuwa kimeandaliwa kuhudumia viwanda vikubwa, lakini ndoto hiyo ilizimika hata kabla ya Mwalimu kufariki dunia.

Tanzania ilisifika sana kutokana na uthabiti wa msimamo wake. Kwenye mikutano ya kimataifa, nchi za Kiafrika zilikuwa zinasubiri Tanzania iseme kwanza, halafu wao waunge mkono.

Tanzania ilikuwa miongoni mwa nchi chache za Kiafrika ambazo zilivunja uhusiano na Uingereza kwa sababu haikuchukua hatua za kijeshi dhidi ya uasi wa masetla wa iliyokuwa Rhodesia (koloni la Uingereza), walipojitangazia uhuru mwaka 1965, Tanzania iliongoza katika kupambana na Makaburu wa Afrika Kusini.

Ilivunja uhusiano na Israeli baada ya vita na nchi za Kiarabu zilizokuwa zinawaunga mkono wananchi wa Palestina. Hivi sasa tunakaa meza moja na Waisreli na kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia.

Tanzania inatambua uwepo wa Jamhuri ya Watu wa Saharawi ambayo sehemu kubwa inakaliwa na Morocco, lakini pia tumeanzisha uhusiano na nchi hiyo ya kifalme.

Where did the rain start beating us? Tunakumbuka shuka asubuhi. Tunaanza upya, tunataka Tanzania ya viwanda baada ya kuviporomosha vile vilivyokuwapo, hivi sasa nchi yetu ingekuwa inaingia katika ujenzi wa viwanda mama, maana viwanda vyepesi (light industries) tulikuwa navyo tayari. Sasa hivi tunaagiza sindano na vijiti vya kuchokonyoa meno! Tujenge mfumo bora wa elimu ili yeyote atakayekuja, asiutikise, lakini kila waziri wa elimu anayekuja, anakuja na kutekeleza anayoyafikia yeye, tutaendelea kuboronga na vijana wetu hawataweza kufanya vizuri katika soko shindani la ajira.

Alipokuwa ametufikisha Mwalimu Nyerere, viwanda vilivyokuwapo, vilitosha kuirudisha Tanzania kwenye karne ya teknolojia na viwanda mama, kwa kuwa alisomesha vijana wa kuviendesha.

Aliwapeleka vijana kwenye nchi mbalimbali; Cuba, China, India, Japan, Urusi, Bulgaria, Yugoslavia, Ujerumani, Uingereza, Marekani, Sweden, Denmark, Uholanzi na kwingineko kusaka elimu.

Viongozi wetu wakadanganywa kwamba haikuwa kazi ya Serikali kujenga na kuendesha viwanda na wakakubaliana na ushauri huo mbovu. Miongo mitatu (na labda tutafikisha 40 kama Wana wa Israel), miaka ya kutangatanga Jangwani, ndipo tunakumbuka wapi mvua ilianza kutupiga.

Katika masuala ya maadili na mapokezi ya utamaduni wetu, tumekuwa tunashabikia mambo ya Wamarekani na Wazungu wa Ulaya. Hata katika michezo, hasa mpira wa miguu, vijana kwa wazee ni mashabiki wakubwa wa timu za Ulaya.

Kushindwa kwa nchi yetu kuruka kiuchumi na kijamii, ni matokeo ya viongozi kukosa mwelekeo. Ndiyo maana sasa tunashindwa kuendesha elimu yetu kwa manufaa ya nchi yetu.

Kuna baadhi ya watu wanasema waasisi walikosea, kwa sababu walijielekeza kwenye mfumo ambao ulishindwa kabla ya kutekelezwa, mfumo wa Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea na wanataka tuendelee kuwa tegemezi wa bidhaa zinazozalishwa na nchi nyingine. Sisi eti hatuna fedha za kutosha kuagiza mitambo mikubwa ya kisasa na kujenga viwanda vyetu.

Mtu asiyejua alikotoka, alipo sasa na anakusudia kwenda wapi, huyu ni sawa na kipofu, anaishi ‘kufikirika’; nchi ambayo mtunzi wa kitabu hicho, Shaaban Robert, anasema ni nchi ambayo haipo duniani.

Tusitafute mchawi, tuangalie tulipojikwaa, tusimame na kuendelea na safari ya huko tuendako, tuwe waangalifu ili tusijikwae tena. Nchi haiwezi kusimama, ni lazima isonge mbele baada ya kujua, where the rain started beating us.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles