23.2 C
Dar es Salaam
Monday, February 6, 2023

Contact us: [email protected]

MAPAMBANO HAYA SAWA NA KUMPIGISHA SIMBA JIKE MSWAKI

Na Dk. Vera Mugittu,

KWA hili la kupiga vita biashara ya dawa za kulevya, naomba nimtie moyo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, bila chembe ya woga. Angalau yeye amethubutu. Hata akishindwa! Ingawa sikubaliani na mambo yake mengi na mitazamo yake, lakini kwa hili nitampongeza mpaka kesho.

Suala la mihadarati ni jipu kubwa ambalo maumivu na athari zake zinagusa moyo na kiini cha utu wa taifa hili. Vijana wanapoharibika, msingi wa kesho wa taifa unaharibika.

Kwa sasa hali ni mbaya mno kwani wanaouza na kufaidika na biashara hii wenyewe na familia zao hawatumii, bali wanawatumia vijana wa familia nyingine kujineemesha.

Kwa sasa idadi ya watumiaji ni kubwa mno. Imefikia kiwango ambacho hata ukianika nguo usipozilinda zinaibiwa ili mtu akanunue mihadarati!

Watoto wanawaibia mpaka wazazi wao. Wakati mwingine watoto wanatumika kugawa mihadarati bure shuleni ili kutengeneza addicts watakaotafuta fedha za kuwanunua wenyewe baadaye!

Yaani puff ya kwanza wanaitoa bure wakijua utarudi tu. Hebu fikiria hilo mtoto akishaonjeshwa anaanza kutafuta kununua mwenyewe kwa udi na uvumba! Hakika hakuna mahali salama kwa sasa.

Historia inaonyesha kuwa kupambana na biashara ya mihadarati ni sawa na kutaka kumpiga simba mkali mswaki. Hivyo ni lazima uingie na kushughulika kwa haraka! Hakika kwa hapa tulipofikia hatuhitaji siasa. Tunahitaji uthubutu, kasi, nguvu na dhamira ya dhati.

Vijana, hasa wa familia masikini wanadanganywa wanakuwa ‘mules’ wa kubeba unga, wengine wakiwa njiani wanatolewa kafara na waliowatuma ili polisi walio kwenye mtandao wa kuwalinda siku moja moja waonekane wanafanyakazi.

Hivyo wanakamatwa na hata kunyongwa! Wazazi wanalia huku ma-don wakitajirika na kuneemeka. Wanapata fedha kwa kuharibu watoto wa wenzao.

Naomba tukubaliane kuwa kwa hapa tulipofikia njia yoyote ikitumika kutunusuru ni sawa tu. Kwa pamoja tuseme tumechoka kuona kesho na ndoto za vijana wetu zinaharibika. Tuseme imetosha.

Na yeyote anayejaribu kupigana tumsaidie bila kujali itikadi zetu. Ni dhahiri kuwa hawezi kuwa sahihi kwa asilimia 100, lakini tukipambana pamoja tutashinda.

RC Makonda naomba usirudi nyuma, hakikisha wote wanajulikana na majina yalishatolewa. Shughulika na majina yote bila woga.

Tutambue pia kuwa vita hii ni ngumu sana na wengi wamejaribu wakashindwa. Namkumbuka marehemu Amina Chifupa akiwa mbunge. Amina alijaribu kupambana kwa kufuata utaratibu haikuwezekana.

Nasema kwa sasa tukubali mbinu yoyote ile itumike. Na atakayetuhumiwa kwa bahati mbaya basi atusamehe kwani kuwafikia mapapa /ma don wa biashara hii ni lazima kupasua kutokea nje kwenda ndani.

Kumbuka ili kuufikia moyo na kuutibu unapoumwa, ngozi ya nje isiyoumwa hukatwa na kuachwa na jeraha na hatimaye kubaki na kovu. Lakini huwa hailalamiki. bali hujitolea kwani bila kufanya hivyo moyo hautatibiwa na mwili wote utakufa! Hata unapojenga barabara mpya kuna wanaopoteza makazi.

Tusiruhusu mianya ya kuchuja hapa mwanzoni. Mianya yote izibwe mpaka pale tutakapofika kwenye kiini. Tukianza kuruhusu kuchuja.. kwenye kiini hutafika. Honestly (kiungwana) hakuna jinsi nyingine!

Dunia nzima inajua kuwa huwezi kuumaliza mtandao huu kwa kufuata utaratibu pekee. Ni lazima uanze na hear says na kamata kamata isiyokuwa na dhamana tena kwa kutumia utaratibu huo huo wa kukamata na kuhoji.

Kimsingi waliokwisha kukamatwa mpaka sasa hakuna kigeni hapo, wamekamatwa kuisaidia polisi kama ilivyo kwa kesi nyingine. Na kama hawahusiki basi muda ukifika wataachiwa tu.

Uzuri ni kuwa ni adimu sana mtu kusingiziwa jambo zito kama hili kama ahusiki kabisa. Yani asingiziwe tu? Na kisaikolojia, wataalamu wa ‘Crime Investigation’ wanasema ukiwafungia watuhumiwa pamoja japo kwa muda mfupi wana kawaida ya kuanza kujadiliana.

Na katika kuhamanika wanajikuta wameanza kutoa siri za kusaidia uchunguzi zaidi. Hivyo tuvumilie tu (si tumeshaanza kuwasikia?)

Mimi kama mzazi nawasihi Watanzania wenzangu tuache ubinafsi na kutafuta masilahi au umaarufu wa kisiasa. Vita hii ni ya kuungwa mkono kwa kutoa ushauri wenye kusaidia si kukejeli na kukatisha tamaa. Chonde chonde ndugu zangu tuache siasa kwenye hili.

Kama tuna ushauri wa jinsi ya kupambana na kushinda vita hii tuutoe. Haijalishi nani anamuua nyoka aliyeingia ndani hata adui akitupa jiwe ni sawa tu. Hivyo usianze kumkejeli na kumtetea nyoka maana kimsingi hata wewe uko hatarini.

Mihadarati ni mibaya kuliko H.I.V, kwani huififisha nafsi na kuuacha mwili ukijikokota bila dira! Go Makonda Go!!

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,471FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles