25.4 C
Dar es Salaam
Monday, January 30, 2023

Contact us: [email protected]

UZALENDO WA KINAFIKI UTAANGUSHA VITA YA DAWA ZA KULEVYA

NA EVANS MAGEGE,

VITA dhidi ya dawa za kulevya iliyoanzishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, inaweza kupata mkwamo wa mafanikio kama jamii itaegemea kutetea hoja za uzalendo wa kinafiki.

Pamoja na watu wengi kujipambanua wazi kuunga mkono vita hiyo, wapo wengi hawaikubali aina ya mbinu anayoitumia Makonda katika mapambano hayo.

Kimantiki, mazingira ya uzalendo wa kupambana na dawa za kulevya yanabaki kama kauli tu kwa wengi na si vitendo kwa sababu wengi wanataka tuhuma zishughulikiwe kwa siri hali ambayo ni tofauti na anavyofanya Makonda.

Hata hivyo, inawezekana aina ya mbinu anayoitumia Makonda katika mapambano yake dhidi ya dawa za kulevya ikiwa haikubaliki moja kwa moja kwa sababu ya upya wake masikioni mwa watu, haijaeleweka kwa sababu ya utofauti wa hisia za watu au inawakera wengi kwa sababu ya uwazi uliopo dhidi ya watuhumiwa.

Ukichambua kwa kina mijadala mbalimbali juu ya mapambano haya, utabaini watu wengi wamesimamia hoja zenye matege ya kiitikadi na propaganda za kusafisha kabla ya kubainika.

Ndani ya mijadala hiyo zipo hoja zinazotoka nje ya muktadha wa mapambano halisi kwa maana ya kuelekezwa kwenye kupambana na mbinu anazozitumia Makonda.

Pia, baadhi ya watu wanaangalia historia ya uhafifu wa mafanikio ya operesheni ambazo Makonda amewahi kuzifanya siku za nyuma kuwa ndicho kinachokwenda kutafsiri taswira ya matokeo ya kampeni yake ya sasa.

Mtazamo kama ule wa kushindwa kwa operesheni za kuwaondoa ombaomba kwenye viunga vya jiji, kushindwa kudhibiti biashara haramu ya ngono (machangudoa) na uhafifu wa matokeo ya kampeni ya usafi (Naona Aibu).

Upo mtanziko wa maswali mengi kutoka kwa watu wanaofuatilia mjadala huo wa mapambano dhidi ya dawa za kulevya. Utawasikia baadhi wanahoji kwanini Makonda na lisiwe Jeshi la Polisi au Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba? Pia utasikia baadhi wanahoji Makonda anatoa wapi jeuri hiyo?

Kimantiki Makonda mwenyewe ameshatoa majibu au mwelekeo wa majibu ya maswali hayo kwa kusema yeye kama Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi ya Mkoa wa Dar es Salaam anao wajibu wa kuhakikisha anadhibiti biashara ya dawa za kulevya ndani ya mkoa wake.

Makonda anastahili kulaumiwa?

Je, Makonda anastahili kulaumiwa? Ndilo swali ambalo linatakiwa kujibiwa na wengi ndani ya mjadala wa mapambano dhidi ya dawa za kulevya anayoyaendesha Makonda kwa sasa.

Katika majibu ya swali hilo wapo wanaounga mkono mbinu ya kuwataja hadharani watumiaji na wauzaji wa dawa za kulevya.

Muktadha wa watoa hoja wa upande huo unajielekeza kuwa mathalani ni tuhuma zenye nia ya kusaidia kundi la watu wengi katika jamii na kwamba si vibaya kuwaweka hadharani watuhumiwa wakati mchakato wa kuwabaini wahusika halisi ukiendelea.

Ndani ya mtazamo huo baadhi wanatanabaisha kwa hoja ya kuwa biashara ya usafirishaji na matumizi ya dawa za kulevya hufanywa kwa siri lakini madhara yake hutokea hadharani kwa kuathiri nguvu kazi ya jamii, hivyo mbinu ya kuwataja hadharani watuhumiwa ni sahihi kwa sababu ya mazingira halisi ya lengo la mapambano.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Benson Bana, anasema hakuna sababu ya kubembelezana katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya.

Anasema si dhambi kwa kutumia falsafa ya Niccolo Machiavelli ambayo inaelekeza kutumia njia yoyote katika kufanikisha jambo.

“Machiavelli alisema: ‘The ends justify the means’, yaani naungana naye Makonda kwamba hii vita si lelemama, wapo watakaomkashifu lakini watambue hii si vita ya mtu mmoja,” anasema Profesa Bana.

Upande wa kundi la pili ambalo linatambua sheria kuruhusu kumtuhumu mtu, lakini wanamtupia lawama Makonda kwa hoja ya kutotanguliza busara ili kuepusha madhara yanayoweza kumtokea mtuhumiwa pale atakapodhihirika hana kosa.

Katika mtazamo wa hoja hiyo, wanatumia hoja ya sheria kwa kusema haielekezi kutumia vyombo vya habari kumtuhumu mtu.

Mchungaji wa Kanisa la Maombezi (GRC) Ubungo, Anthony Lusekelo, anasema operesheni ya kukamata watuhumiwa wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya inatakiwa kufanywa kwa umakini mkubwa ili kulinda heshima ya mtuhumiwa katika jamii ya Watanzania.

Katika mtazamo huo, Lusekelo alitoa mfano halisi unaomhusu yeye kwa tuhuma za kuhusishwa na biashara ya dawa za kulevya zilimuathiri mwaka 1997.

“Ikionekana kama si kweli kuwa hao wanaokamatwa ovyo hawahusiki na biashara hii ya dawa za kulevya itakuwaje? Si jambo dogo kujenga jina kwa sababu yule ni mtuhumiwa bado haijathibitishwa, akifikishwa mahakamani na ikabainika kuwa hahusiki ni kazi sana kurudisha hadhi yake kwa jamii,” anasema Lusekelo.

Vita ya dawa za kulevya na simulizi ya uhujumu uchumi

Mapambano dhidi ya biashara ya dawa za kulevya ambayo ameyaanzisha Makonda yanairejesha nchi katika historia ya vita dhidi ya wahujumu uchumi.

Mtazamo na maudhui hayo naweza kuujenga katika simulizi ya mwaka 1983 ambapo Serikali ilitunga sheria maalumu kwa ajili ya watu ambao walituhumiwa kuwa ni wahujumu uchumi.

Kabla ya hapo, polisi waliwakamata washukiwa na kuwapeleka mahakamani. Kwa vile upelelezi ulikuwa mgumu, kesi nyingi zilifutwa na mahakama, lakini washukiwa wakiwa wamesota rumande kwa siku kadhaa.

Polisi nchi nzima waliwakamata watu wengi tu kwa makosa madogo madogo ya kukutwa na bidhaa majumbani mwao. Madebe manne ya mchele, kreti sita za soda, mabati ishirini au nondo 100, vilitosha kumsukumiza mtu rumande kwa madai ya uhujumu uchumi.

Wengi waliumizwa na hatua hii ya Serikali, kutokana na husuda na wivu. Ukweli ni kuwa nchi ilikuwa inapita katika kipindi kigumu kiuchumi na uchache wa bidhaa uliwalazimu watu kuhodhi bidhaa lakini kwa sababu ya husuda watu hao wakaripotiwa polisi kwa kosa la uhujumu uchumi.

Kwa mtazamo vita hii dhidi ya dawa za kulevya kama ni marudio ya makosa ya vita dhidi ya wahujumu uchumi. Kwamba vyombo vya dola visifanye kazi kwa kusikia maneno ya watu wanaowanyooshea vidole wenzao kwamba ni wachuuzi wa dawa za kulevya.

Ni vema kujiridhisha kwanza kabla ya kuwakamata na kuwaweka korokoroni, ili kulinda dhana nzima ya utawala wa sheria.

Ni kweli dawa za kulevya si tu zimeharibu maisha ya vijana wengi wa Kitanzania ambao ni nguvu kazi ya taifa, lakini pia Tanzania sasa imeingizwa katika nchi zinazotumika kama njia ya kupitishia dawa hizo. Ni lazima tupige vita kama Taifa.

Vijana wengi wanatumika kama ‘punda wa mizigo’ kusafirisha dawa za kulevya. Wengine wamepoteza maisha, wamefungwa katika nchi mbalimbali na wengine wamenyongwa kwa kosa la kukutwa na dawa za kulevya. Kama Taifa hatuwezi kukaa kimya bila kuchukua hatua. Lakini tusikurupuke.

Polisi ina kitengo kinachoshughulika na suala hili la dawa za kulevya. Kikosi hiki kina wataalamu wa mambo hayo. Jeshi la polisi likiimarishe kikosi hiki kwa kukiongezea rasilimali watu na fedha, hasa katika Jiji la Dar es Salaam ambalo linasemwa ndicho kitovu cha kuuza na kusafirisha dawa za kulevya. Lakini wasifanye kazi kama zima moto.

Tatizo la dawa za kulevya ni la Serikali zote duniani zinazopambana nalo. Rais wa Ufilipino, Rodrigo Duterte, amewapa ruhusa polisi kuwaua wafanyabiashara wa dawa za kulevya, lakini bado hajatangaza kama amelimaliza tatizo hilo.

Tanzania tunathamini sana maisha ya binadamu na ikiwa wanaoitwa ‘mapapa’ wa dawa za kulevya watakamatwa na mahakama ikawahukumu, wapewe adhabu kulingana na makosa yao. Hili litatujengea heshima kama Taifa na kuwa ni taifa la haki na linatii na kuheshimu haki za binadamu na sheria na kanuni za utawala bora.

Tunataka Dar es Salaam bila dawa za kulevya na kulifanya kuwa jiji la mfano, kama kila Mtanzania na hasa kila mzalendo atasaidia katika vita hii ngumu.

Tishio la biashara ya dawa za kulevya nchini

Ongezeko la waathirika wa dawa za kulevya (mateja), idadi ya Watanzania wanaokamatwa na dawa za kulevya nje ya nchi ni sehemu ya kiashiria ambacho kinatoa tafsiri ya kiwango cha tishio la biashara hiyo hapa nchini.

Inawezekana mwenendo wa biashara ya dawa za kulevya hapa nchini umefika katika hatua ya juu zaidi kuingiza nchi kwenye ubeberu wa biashara hiyo.

Kwa tathmini ya kawaida, Tanzania imevuka katika kiwango cha kutumiwa na raia wa mataifa mengine kama njia ya kupita kusafirishia dawa za kulevya kwenda nchi nyingine.

Hatua iliyopo kwa sasa ni kwamba Watanzania wenyewe ndio wamegeuzwa wapokeaji wa dawa na kusafirisha kwenda mataifa mengine.

Kama hatua hii itafumbiwa macho, kuna hatari ya Taifa kupata mabeberu wa biashara hiyo kwa maana ya kuingiza dawa hizo katika hali ya ghafi na kuzichakata hapa hapa nchini kisha kuzisambaza kwenye mataifa mengine.

Hatua hiyo ambayo unaweza kuiita kwa jina la ubeberu wa dawa za kulevya, ndiyo inayotajwa kuwa hatari kwa utengamano wa taifa lolote.

Kwamba ukwasi wanaokuwa nao mabeberu wa biashara za dawa za kulevya ndiyo hutoa nguvu ya utawala wa taifa.

Hii inatoa tafsiri ya baadhi ya mataifa ya Amerika Kusini kwamba viongozi wao wengi wanatajwa kuwa wamepata madaraka kwa nguvu ya mabeberu wa dawa za kulevya na lengo kuu ni kulinda biashara hizo.

Dawa za kulevya na utakatishaji fedha

Biashara ya dawa za kulevya na utakatishaji fedha ndizo biashara zinazotegemeana kimazingira na zenye ukwasi wa hali ya juu kuliko biashara yoyote duniani.

Kwa nchi za dunia ya tatu mfano Tanzania, biashara hizo zisipokabiliwa hukimbilia kuendesha uchumi na siasa za nchi.

Uchumi wa dawa za kulevya ambao uzalishwa na utakatishaji wa fedha unapoingia ndani ya siasa za taifa lolote kiwango cha umwagaji damu kwa wananchi huongezeka kwa kiasi kikubwa na sababu kuu ni ushindani wa magenge ya wauza dawa za kulevya.

Mataifa ya Mexico, Colombia, Peru, Panama, Bolivia na Venezuela yanatajwa kuwa na idadi kubwa ya raia waliouawa na magenge ya wahusika wa dawa za kulevya.

Ndani ya biashara hiyo, michezo ya kamari hushamiri katika muktadha wa kuhalalisha fedha zinazotakatishwa.

Kwanini Watanzania wanageuzwa makontena ya dawa za kulevya?

Kuna mitazamo kadha wa kadha ambayo inawahusisha vijana wa Kitanzania kugeuzwa punda au kwa maana nyingine makontena ya kusafirisha dawa za kulevya.

Miongoni mwa mitazamo ni tamaa za maisha bora, ukosefu wa ajira, mkumbo wa vikundi na kukata tama (kujilipua) kunatajwa kuchochea vijana wengi kutumika kusafirisha dawa za kulevya.

Historia inaonyesha kuwa vijana wengi waliokuwa na mtazamo kama huo siku za nyuma kabla ya kushamiri kwa biashara ya dawa za kulevya, wengi walijihusisha na kazi za ubaharia na uzamiaji kwenye mataifa ya kigeni.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles