Tume ya Haki za Binadamu wamejaribu

NEWSPAGES_20160423062933

NA FREDERICK FUSSI,

NITUMIE fursa hii kuipongeza Tume ya Haki za Binadamu kwa kuonesha uongozi katika sakata la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuanzisha operesheni walioipa jina la Umoja wa Kupambana na Udikteta Tanzania (Ukuta) na baadaye kauli za kibabe zikaibuka kutoka Jeshi la Polisi.

Ingawa juhudi hizo hazitoshelezi lakini angalau wameonesha njia kwa kutaka kuanzisha maridhiano baina ya pande mbili yaani Serikali na Chadema.

Itakumbukwa kuwa yapata majuma kadhaa yamepita tangu Chadema watangaze kufanya kampeni hiyo ya Ukuta. Katika tamko hilo la Chadema lililotolewa na Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe, walielezea hoja mbalimbali zilizosababisha kuundwa kwa Ukuta, hoja ambazo hakuna kiongozi yeyote wa Serikali aliyezijibu zaidi ya kutoa kauli za kibabe dhidi ya raia wote watakaojitokeza Septemba mosi kuunga mkono juhudi hizo.

Kutojibiwa kwa hoja hizo ndio sababu yangu ya kufikiria kuwa Tume ya Haki za Binadamu imejaribu kuingilia kati kwa kutaka kuunda meza ya mazungumzo, japokuwa Jeshi la Polisi wala mwakilishi kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) walioalikwa hawakujitokeza katika mazungumzo hayo yaliyoratibiwa na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.

Tamko la Mwenyekiti wa Tume kwa Jeshi la Polisi na Chadema ni ‘premature’ nikimaanisha lilitolewa mapema mno kutokana na upande mmoja wa mazungumzo ambao ni Jeshi la Polisi na mwakilishi wa CCM kutojitokeza kwenye hayo mazungumzo, jambo ambalo linaashiria mazungumzo hayo hayakuwa na mafanikio yaliyokusudiwa.

CCM wao wakiwa wenye Serikali inayotawala hawajaonesha mfano mzuri wa kiungwana kwa kushindwa kupeleka mwakilishi katika mazungumzo hayo.

Jeshi la Polisi nalo halijaonesha mfano mzuri kwa kushindwa kupeleka mwakilishi kwenye mazungumzo hayo ya maridhiano. Kwa kushindwa kushiriki mazungumzo hayo, Jeshi la Polisi linaacha maswali yasiyokuwa na majibu juu ya nafasi ya jeshi hilo katika kuheshimu kazi ya Tume kulinda na kutunza haki za binadamu.

Kitendo hicho ni kutuma ujumbe kwa umma kuwa huenda haki za binadamu si kipaumbele kwao, lakini pia kuitikia wito wa Tume hiyo ni kuitikia wito juu ya kuheshimu utawala bora wa sheria ambazo tume na jeshi kwa pamoja zinazisimamia.

Pamoja na kazi nzuri iliyofanywa na Tume bado iliteleza kwa kutowaalika wahusika wakuu wanaotuhumiwa kwenye tamko la Ukuta ambao ni Serikali kuu ambayo katika mazungumzo hayo ingeweza kuwakilishwa na Waziri Mkuu.

Hata kama Jeshi la Polisi lingejitokeza kwenye mazungumzo hayo bado wasingeweza kujibu hoja zote za Ukuta kwa kuwa wao hupokea na kutekeleza amri kutoka Serikali, katika kuzuia mikutano na mikusanyiko ya vyama vya siasa kama moja ya hoja zinazopingwa na Ukuta, kwa hiyo bado Serikali inabakia kuwa mhusika mkubwa katika mazungumzo yaliyoandaliwa na Tume.

Kazi iliyofanywa na Tume katika hili inapaswa kupongezwa na kutiwa moyo kwa uthubutu waliouonesha. Nchi hii ilipofika inahitaji busara kama zilizooneshwa na Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora. Nitoe rai kuwa zimesalia siku chache kabla ya Septemba mosi, Tume haijachelewa kuandaa mkutano mwingine wa kusaka maridhiano na wakati huu wamwalike Waziri Mkuu, ili mazungumzo yawe na mafanikio.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here