24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 10, 2024

Contact us: [email protected]

Kasi ya Dodoma isije ikawa kama mchakato wa Katiba

tumblr_m4r9oa3hM01r67lwjo1_1280

NA EMMANUEL MWANSASU

SUALA la Katiba na la kuhamia Dodoma yote haya yalitamkwa kwa vipindi tofauti na viongozi wawili tofauti lakini yana mfanano mkubwa sana.

Kwanza matamko yote yametolewa na marais; lile la Katiba lilitolewa na Rais mstaafu, Jakaya Kikwete na hili la kuhamia Dodoma limetolewa na Rais John Magufuli, ukiacha kuwa yalitoka kwenye vinywa vya wakubwa hao, mfanano mkubwa ni kuwa masuala haya yote hayakuwemo kwenye Ilani ya chama kilichopo madarakani.

Ukirudi kwenye suala la mchakato wa Katiba mpya, hili halikuwahi kuwa ajenda ya chama tawala bali wapinzani ndio waliokuwa wakilipigania na yawezekana kutokana na msukumo huo rais akaamua kuwapa Watanzania Katiba kabla hajamaliza utawala wake lakini kwa bahati mbaya mchakato ule haukukamilika mpaka JK alipomaliza muda wake.

Hili la kuhamia Dodoma halikuwemo kwenye Ilani ya chama tawala na katika kumbukumbu zangu sikumsikia popote rais akitoa ahadi hiyo na kwa bahati mbaya hata katika bajeti iliyopitishwa ya mwaka huu wa fedha bado suala hilo halikuwemo na halikutengewa fedha lakini ghafla rais akasema kabla ya kumaliza awamu yake ya kwanza Serikali itakuwa tayari imeshahamia Dodoma.

Kama nilivyosema hapo awali kuwa haya yote ni mambo ya heri wala hakuna jambo baya maana lile la Katiba kwa muda ule lilikuwa ni vuguvugu kubwa hasa maeneo ya Zanzibar hivyo yawezekana njia ya kulipooza ilikuwa ni kuuleta mchakato ule vivyo hivyo kwa suala la kuhamia Dodoma.

Hili lilikuwa ni wazo la viongozi tangu kwa waasisi wa Taifa hili na wazo liliasisiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere huku akielezea kuwa sababu za kiusalama ni moja kati ya mambo ya msingi yanayoshawishi Serikali kuhamia katikati ya nchi nako ni Dodoma sababu ambayo pia imerudiwa na rais aliye madarakani, Magufuli.

Sawa tumeshakubali kuhamia Dodoma  lakini je, tumejipanga sawasawa kabla ya kuhakikisha jambo hili linafanyika? Maana tusijerudia makosa tuliyofanya kwenye mchakato wa katiba.

Kwa ufahamu wangu Ilani ya chama ni kama Bajeti ya chama ndani ya miaka mitano, yaani Serikali itafanya mambo haya na haya ndani ya miaka mitano hivyo kwa asilimia kubwa bajeti itakuwa ndani ya ilani ile japo hiyo haina maana kuwa mambo mengine ambayo yako nje ya ilani ile kuwa hayatafanyika la, hasha.

Huwa yanafanyika lakini ni baada ya kufanya tathmini ya kutosha juu ya jambo hilo ili kuzuia mgogoro wa kiuchumi. Leo hii ukimuuliza mtaalamu yeyote wa uchumi atakwambia ni kwa jinsi gani mchakato ule wa katiba ulivyoathiri hali ya uchumi wa nchi yetu maana ili mchakato ule kufanyika ilibidi miradi mingine isitishwe ili fedha ielekezwe kule na kwa bahati mbaya mchakato ule mpaka leo haujakamilika japo Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi amesema mchakato haujakwama ila kinachosubiriwa ni kura ya maoni.

Nafikiri mchakato wa Katiba ulikuwa ni somo kubwa sana ambalo lingetupa tahadhari juu ya suala hili la kuhamishia Serikali Dodoma pamoja na kwamba rais hakutaja ni lini siku rasmi ya kuhamia huko naona mawaziri wamelipokea kwa kasi maana wengine wamesema haitafika Septemba watakuwa wameshawasili Dodoma yawezekana wanaenda na kasi ya Magufuli.

Ningependa kutoa rai yangu kuwa kuhamia Dodoma wala si jambo baya ila tungelitizama kwa upana ili lisije kuathiri mipango mingine ya maendeleo ambayo tuliahidi kuwatimizia Watanzania.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles