24.8 C
Dar es Salaam
Friday, October 4, 2024

Contact us: [email protected]

Tume Uchaguzi Nigeria yakana kuahirisha uchaguzi kisiasa

LAGOS, NIGERIA

WAKATI wagombea urais nchini Nigeria wakishutumiana kwa tangazo la ghafla la kuahirishwa uchaguzi, Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) imesema uamuzi huo haukushinikizwa kisiasa wala kiusalama.

Wagombea wakuu wa urais; Rais mtetezi Muhammadu Buhari na mpinzani wake Atiku Abubakari wametupiana lawama kutokana na uamuzi wa ghafla uliochukuliwa na tume wa kuahirisha uchaguzi huo kwa wiki moja hadi Februari 23.

Uamuzi huo uliotangazwa saa tano tu kabla ya vituo vya kura kufunguliwa siku ya Jumamosi unatajwa kuigharimu nchi hiyo dola bilioni mbili za Kimarekani, sambamba na kuathiri hadhi ya taifa hilo kubwa kabisa kufuata mfumo wa kidemokrasia barani Afrika.

Mwenyekiti wa INEC, Mahmood Yakub, aliwaambia waangalizi, wanadiplomasia na wanahabari kuwa kusogezwa kwa uchaguzi hakuhusiani na hali ya ukosefu wa usalama wala kuingiliwa kisiasa.

Badala yake, alisema ni mazingira yasiyo rafiki ikiwemo hali mbaya ya hewa iliyosababisha ndege zilizobeba vifaa kuchelewa kuwasili pamoja na kuteketea moto wa ofisi tatu za tume hiyo.

Iwapo uchaguzi ungefanyika kama ulivyopangwa, vituo vya kura visingeweza kufunguliwa kwa wakati mmoja nchi nzima, alisema.

“Lengo letu ni kuhakikisha wananchi wanashiriki uchaguzi ulio huru, wa haki na wenye kuaminika, alisema Yakub.

Alisema awali hadi saa nane usiku ya kuamkia siku ya uchaguzi walikuwa na uhakika uchaguzi huo ungefanyika kabla ya kuahirisha baada ya kubaini changamoto za vifaa.

Alisema tarehe mpya, Februari 23 haina mjadala tena.

Lakini wapigakura wenye hasira katika mji mkuu, Abuja, na kwingineko ambao walitoka majumbani kwao kwenda kupiga kura zao, wakiwemo raia wengi wa nchi hiyo wanaoishi mataifa ya nje walishutumu kitendo hicho.

Auwolu Usman kutoka mji wa Maiduguri amelalamika, “’Usiku kuchwa hatukupata usingizi, tukiwa na matumaini ya kupiga kura asubuhi, lakini tumeishia kuambiwa uchaguzi umeahirishwa.”

Kulingana na sheria ya uchaguzi ya Nigeria, raia wanatakiwa wapige kura katika jimbo analotoka.

Pamoja na kuomba utulivu, wagombea hao wanaoongoza katika kinyang’anyiro cha urais wamesema wamesikitika, na kutupiana lawama.

Festus Keyamo ambaye ni msemaji wa kambi ya Rais Buhari, amekishutumu chama kikuu cha upinzani cha People’s Democratic Party (PDP) kula na njama na Tume ya Uchaguzi kuahirisha uchaguzi huo.

”Ni matumaini yetu kwamba INEC itaendelea kutoegemea upande wowote, kwa sababu tetesi zimeenea kuwa imekula njama na PDP kuahirisha upigaji wa kura kwa sababu hakikuwa tayari.” alisema Keyamo.

Kwa upande mwingine lakini, chama cha PDP nacho kimerudisha lawama upande wa chama cha All People’s Congress (APC) cha Buhari, kikidai kucheleweshwa kwa uchaguzi ni mbinu ya kiongozi huyo kuendelea kung’ang’ania madarakani.

“’Hii ni hatua ya hatari kwa demokrasia yetu, na haikubaliki.” alisema msemaji PDP, Uchoe Secondu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles