24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

TUCTA SASA KUDAI NYONGEZA YA MSHAHARA KORTINI

Na LEONARD MANG'OHA-DAR ES SALAAM


SHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), linajipanga kuiburuza Serikali mahakamani kudai haki za wafanyakazi, ikiwamo kushindwa kuzingatia nyongeza ya mshahara kwa wafanyakazi wa umma.

Pamoja na hayo, Shirikisho hilo limesema kuwa wamechoshwa na Serikali kushindwa kutekeleza hoja zao haraka.

Kauli hiyo ilitolewa Dar es Salaam jana na Rais wa Tucta, Tumaini Nyamhokya, alipokuwa akisoma maazimio manane ya kikao cha Baraza Kuu la shirikisho hilo.

Nyamhokya alisema tangu Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani, haijafanya nyongeza yoyote ya mshahara kwa watumishi wake.

Kutokana na hali hiyo, alisema ni lazima Serikali izingatie nyongeza ya mshahara katika mwaka ujao wa fedha (2017/2018), kwani hivi sasa wanaishi maisha magumu na yenye kudhalilisha.

Kutokana na hali hiyo, Tucta imesema kuwa Serikali inapaswa kuzingatia nyongeza hiyo ikizingatiwa kwa sasa kuna uwepo wa mfumuko wa bei unaofikia asilimia 5.5, kupanda kwa gharama za maisha na kushuka kwa thamani ya shilingi dhidi ya dola ya Marekani.

“Tunajipanga kwenda mahakamani kwani Serikali imekiuka mambo mengi, ikiwamo kima cha chini cha mshahara ni shilingi 300,000 lakini Serikali bado inalipa Sh 170,000. Huku ni kuvunja sheria.

“Nyongeza ya mshahara ya kila mwaka imesitishwa, hivyo inawafanya wafanyakazi nchini kudhalilika kimaisha. Serikali imekuwa ikionyesha ubaguzi kwa kuongeza kiwango cha mshahara kwa walimu pekee japo kwa kiwango kidogo, huku wafanyakazi wengine wakishindwa kuongezewa kabisa.

“Pamoja na ukweli kwamba Serikali imeonyesha dhamira ya kulipa madeni ya baadhi ya watumishi, hasa walimu, Tucta inaitaka Serikali kwa kuzingatia dhamira hiyo hiyo, kuongeza kasi wa ulipaji wa madeni kwa watumishi wote wa umma,” alisema Nyamhokya.

Akizungumzia makato ya kodi katika mshahara, alisema kuwa ni vema Serikali iweke uwiano wa kodi kwenye kodi (PAYE) kwa kuzingatia vima vya mshahara.

Alisema Tucta imebaini kuwa kodi ni kubwa sana ikilinganishwa na mapato ya mtu mmoja mmoja.

“Tunaitaka Serikali kuanzisha majadiliano, kwani hadi sasa inatumia kima cha chini cha Sh 170,000 kama kigezo cha kuanzia wakati kima cha chini kimebadilika,” alisema.

Pia alisema wameitaka Serikali kusitisha mara moja ukataji wa asilimia 15 ya marejesho ya mkopo wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB), kwa kutaka kuheshimiwa kwa mikataba ya awali ambayo  inatambua makato ya asilimia nane.

“Hii inatokana na ukweli kwamba waathirika wote hawajashirikishwa katika mabadiliko haya ya kisheria, pia Tucta inasikitishwa na hali mbaya ya ajira nchini inayotokana na kusitiswa kwa ajira serikalini,” alisema Nyamhokya.

Kutokana na hali hiyo, alisema Serikali imeshindwa kushirikiana na sekta binafsi jambo linalodhohofisha sekta hiyo na kusababisha wafanyakazi kupoteza ajira.

Nyamhokya alisema ni vema Serikali iwezeshe sekta binafsi, hususan wawekezaji wazalendo ili waweze kutoa ajira zaidi.

Alisema sasa ni wakati mwafaka kwa Serikali kuzindua Bodi ya Mishahara ya Kima cha Chini cha Watumishi wa Umma sambamba na kuziwezesha bodi zote mbili kufanya kazi ili kuboresha hali ya wafanyakazi nchini.

“Ifahamike kuwa vima vya chini vya mishahara kwa mujibu wa sheria vinatakiwa kufanyiwa utafiti kila baada ya miaka mitatu na bodi za mishahara na kwamba utafiti wa mwisho ulifanyika mwaka 2013,” alisema

Akizungumzia mabadiliko ya Sheria ya Utumishi wa Umma namba 8 ya mwaka 2002, Nyamhokya alisema imeathiri haki za msingi za watumishi wa umma, ikiwamo kuwaondolea madaraka viongozi wa taasisi kujadili na kufunga mikataba ya hali bora ya vyama vya wafanyakazi.

“Hii ina maana kuwa wafanyakazi wamenyang'anywa haki ya kutumia vyombo vya utoaji haki kisheria, kama vile CMA na Mahakama Kuu Kitengo cha Kazi. Kwa kuwa Tucta haikushirikishwa kwa namna yoyote katika mchakato mzima wa mabadiliko hayo ya sheria, tunaitaka Serikali kuacha mara moja matumizi ya mabadiliko yaliyofanyika katika sheria hiyo,” alisema.

Kutokana na hali hiyo, alisema Serikali inapaswa kuacha kuzuia utekelezaji wa mikataba ya hali bora kazini kwa kuondoa baadhi ya mambo ambayo yanaonekana kuwa na masilahi kwa watumishi, kwani kufanya hivyo inakinzana na mkataba wa Shirika la Kazi la Kimataifa (ILO) namba 98 ambao Serikali imeuridhia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles