28 C
Dar es Salaam
Monday, January 24, 2022

MAHAKAMA YABARIKI KINA SHIKUBA KUPELEKWA MAREKANI

Na Kulwa Mzee-Dar es Salaam


MAHAKAMA imekubali maombi ya aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Harrison Mwakyembe ya kutaka Watanzania watatu washikiliwe wakati wakisubiri kibali cha kusafirishwa kwenda Marekani kujibu mashtaka ya kusafirisha na kusambaza dawa za kulevya nchini humo.

Uamuzi wa kuyakubali maombi hayo ulitolewa jana na   Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Cyprian Mkeha, baada ya kujiridhisha na ushahidi na vielelezo vilivyotolewa mahakamani.

Kabla ya Hakimu Mkeha kutoa uamuzi huo, Shikuba alisema ni bora wakapelekwa Marekani kwa sababu  wanaweza kupata haki yao.

“Ni bora tukapelekwa Marekani tunaweza kupata haki yetu, watu watatu tunatuhumiwa kwa kilo 1.78 za heroine, kweli hiyo?

“Tunaishi kama wahujumu uchumi, hatujabadilisha nguo siku ya tatu, kesi Lindi nimefutiwa na kilo 200 za heroine nakuja kushtakiwa Marekani kwa kilo moja.

“Sina hata viatu, nimetolewa Lindi hivyo hivyo… nitakuwa mtu wa kwanza kuingia Marekani nikiwa nimevaa ndala,”alidai Shikuba wakati akisubiri Hakimu aingie mahakamani.

Kifungu cha 8(3) cha Sheria ya Kusafirisha wahalifu  kinasema hakimu akishajiridhisha na ushahidi uliofikishwa mahakamani anampa taarifa Waziri wa Katiba na Sheria kwa ajili ya kutoa kibali cha kuwasafirisha.

Hakimu Mkeha akisoma uamuzi baada ya kusikiliza hoja za pande mbili, alisema mahakama kabla ya kuamua ilijiuliza maswali kadhaa ikiwamo kama mashtaka wanayohusishwa nayo wajibu maombi yako katika utaratibu wa kubadilisha wahalifu.

Pia mahakama ilijiuliza kama kuna mkataba kati ya nchi husika ambako baada ya kuangalia imebaini kwamba kuna makubaliano ya kubadilishana wahalifu kati ya nchi hizo mbili.

“Mahakama imekubaliana na maombi yaliyowasilishwa na Waziri wa Katiba na Sheria, mahakama inatoa amri ya kuwashikilia wajibu maombi mpaka   waziri atakapotoa kibali cha kuwasafirisha kwenda Marekani,”alisema.

Hakimu Mkeha alisema kama wajibu maombi watakuwa wanapingana na uamuzi huo, mahakama inawapa nafasi ya kukata rufaa ndani ya siku 15.

Mwakyembe aliwasilisha maombi Februari 15 mwaka huu, akiomba mahakama hiyo kuamuru  Kiongozi wa Taasisi ya Kusambaza Dawa za Kulevya nchini, Ally Haji, maarufu Shikuba, Iddy Mfuru na Tiko Adam washikiliwe wakati wakisubiri kibali cha kuwasafirisha kwenda Marekani kujibu tuhuma za kula njama kusafirisha na kusambaza dawa za kulevya nchini humo.

Jamhuri iliwakilishwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Edwin Kakolaki na katika kuiridhisha mahakama iliwasilisha maombi pamoja na ushahidi dhidi ya wajibu maombi, wa kuonyesha kujihusisha kwao katika matukio hayo.

Ushahidi ulionyesha kwamba Marekani iliwachunguza wajibu maombi kwa miaka minne na walitumia Dola za Marekani 10,000 kununua dawa hizo kutoka kwa taasisi yao ili kubaini ukweli..

Wajibu maombi ilibainika walikuwa wakisafirisha heroine kwa kutumia magari, wakifikisha dawa hizo Marekani na kuwatumia watu kusambaza kwa kutumia ndege binafsi na Shikuba ndiye kiongozi wa taasisi hiyo.

Kakolaki alidai maombi yaliambatana na kiapo kilichoapwa na Richard Magnes ambaye katika kiapo chake anadai wajibu maombi wanatuhumiwa kuingiza dawa za kulevya zaidi ya kilo 1.78 Marekani.

Alidai ushahidi katika kiapo hicho unadai aliwahi kukamatwa mbeba dawa(punda) mwaka 2012, alizitoa kwa njia ya haja kubwa na alipohojiwa alimtaja Shikuba kuwa alimpa dawa hizo.

Kakolaki alidai tangu mwaka 2005 wajibu maombi wanatajwa na watuhumiwa mbalimbali   Marekani kwamba ndiyo wanaosambaza dawa hizo kwa kutumia taasisi yao inayoongozwa na Shikuba.

Ushahidi huo wa kiapo unadai Shikuba aliwafundisha miongoni mwa watuhumiwa waliokamatwa, jinsi ya kubeba dawa hizo na kusafirisha na kwamba dawa hizo zilikuwa zikiingia Tanzania kwa meli kupitia mwambao   kwa maelekezo ya Shikuba.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
176,379FollowersFollow
531,000SubscribersSubscribe

Latest Articles