MOGADISHU, SOMALIA
RAIS wa Marekani, Donald Trump ameamuru kuondolewa kwa karibu wanajeshi wote wa Marekani kutoka Somalia kufikia Januari 15, idara ya ulinzi nchini humo imesema.
Marekani ina wanajeshi wapatao 700 nchini Somalia wanaosaidia vikosi vya wenyeji kupigana na al-Shabab na wanamgambo wa Islamic State.
Maafisa wa Marekani walisema kuwa askari wengine watahamia nchi jirani, wakiruhusu operesheni za kuvuka mpaka.
Katika miezi ya hivi karibuni Rais Trump alitoa maagizo kama hayo ya kupunguza vikosi vya Marekani huko Iraq na Afghanistan.
Kwa muda mrefu ametaka wanajeshi wa Marekani warudi nyumbani na amekosoa operesheni za majeshi kuwa ya gharama kubwa na zisizo na ufanisi.
Amri ya kujiondoa – ambayo itasababisha wanajeshi kupangwa tena siku chache kabla ya Trump kuondoka mamlakani – inabadilisha sera ya Waziri wa zamani wa ulinzi wa Marekani Mark Esper, ambaye alifutwa kazi mwezi uliopita na kuendelezwa uwepo wa Marekani nchini Somalia.
Taarifa ya Wizara ya ulinzi Pentagon imesema kwamba agizo lakuwaondoa wafanyakazi wake nchini Somalia mapema 2021 haiashirii mabadiliko katika sera ya Marekani
“Tutaendelea kusambaratisha makundi ya wanamgambo wenye msimamo mkali ambayo yanaweza kuwa tishio kwa ardhi yetu.” Ilisema taarifa hiyo.
Wataalamu wengine wameonya kuwa kujitoa kwa Marekani kunaweza kuwapa nguvu wanamgambo katika eneo la pembe ya Afrika.
Wasomali mashuhuri wamekosoa tangazo la Pentagon kwamba karibu wanajeshi wote 700 wa Marekani wataondoka Somalia katikati ya mwezi Januari, kwa amri ya Rais Trump.
Seneta Ayub Ismail Yusuf aliuelezea uamuzi huo kama “wa kusikitisha sana”. Vikosi vya Marekani, alisema, vimetoa “mchango mkubwa” wa mafunzo na ufanisi wa utendaji wa wanajeshi wa Somalia.
Labda Marekani itaendelea kufanya mashambulio ya anga dhidi ya wanamgambo hao kutoka kambi za nchi jirani.
Mwezi uliopita, wakaguzi wa serikali ya Marekani walishauri dhidi ya mpango kujitoa Somalia, wakisema vikosi wenyeji havitaweza kupambana na vitisho kutoka kwa wanamgambo bila msaada wa Marekani.
Vikosi hivyo vya Marekani vitakavyobaki nchini Somalia vitakaa katika mji mkuu wa Mogadishu, Pentagon ilisema.
Somalia imekumbwa na machafuko ya kisiasa kwa miongo kadhaa lakini katika miaka ya hivi karibuni kikosi cha kulinda amani kutoka Umoja wa Afrika pamoja na wanajeshi wa Marekani wamerudisha udhibiti wa Mogadishu na maeneo mengine kutoka kwa al-Shabab – mshirika wa al-Qaeda.
Kundi hilo limepigana kwa zaidi ya miaka 10 kuweka utawala wa sheria za kiislamu, na mara nyingi hushambulia raia na kulilenga jeshi.
Marais wa Marekani wamehofia kuingilia kati nchini Somalia tangu wanajeshi 18 wa vikosi maalum walipokufa wakipambana na wanamgambo huko Mogadishu mwaka 1993, vita vilivyoigizwa katika filamu ya Black Hawk Down.