WASHNGTON, MAREKANI
Rais wa Marekani, Donald Trump, amefanya mkutano wa kwanza wa kampeni tangu ashindwe katika uchaguzi wa Novemba 3.
Mkutano huu alioufanya kwenye jimbo la Georgia, umekuja siku chache tu kabla ya jimbo hilo kurudia uchaguzi wa Useneta, ambao utaamua nani atakuwa na viti vingi kwenye bunge hilo.
Rais mteule, Joe Biden, alikuwa mgombea wa kwanza wa Democrats, kushinda jimbo la Georgia, tangu mwaka 1992.
Rais Trump, kwa mara nyingine ameendelea kutoa madai ya kuibiwa uchaguzi bila ya kuweka wazi ushahidi alionao.
Kabla ya mkutano wake rais Trump, kupitia ukurasa wake wa kijamii wa Twitter, aliendelea kumkashifu gavana wa jimbo la Georgia kutoka chama chake, akimtaka amsaidie kubadili matokeo ya jimbo hilo.
Hata hivyo katika hotuba yake, rais Trump alionesha kukubali kushindwa, akidai kuwa sera yake ya mambo ya nje huenda ikabadilishwa hivi karibuni ikiwa Biden ataanza kazi Januari 20.
Rais Trump, alikuwa akiwapigia kampeni wagombea wawili wa Republican wanaotaka kuchaguliwa tena katika uchaguzi wa marudio baada ya raundi ya kwanza kuwa hakuna aliyefikisha zaidi ya asilimia 50.