TRA yazindua uboreshaji wa TIN

Alphayo Kidata
Alphayo Kidata
Alphayo Kidata

Na Koku  David, Dar es Salaam

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), jana ilizindua uhakiki na uboreshaji wa taarifa za usajili wa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) katika Mkoa wa Dar es Salaam na kazi hiyo inatarajia kufikia ukomo Oktoba 15 mwaka huu.

Akizungumza  Dar es Salaam jana, Kamishna Mkuu wa TRA, Alphayo Kidata, alisema lengo ni kubadili mfumo wa sasa wa kuhifadhi kumbukumbu za walipa kodi na kuuweka katika mfumo mpya unaoendana na ukuaji wa teknolojia ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa wananchi   waweze kutambua umuhimu wa uhakiki wa TIN.

Lengo jingine alisema, ni kupata idadi sahihi ya walipa kodi wanaostahili kuwapo kwenye wigo wa kodi ikiwa ni pamoja na kuwaondoa walipa kodi hewa pamoja na wale ambao hawajihusishi na biashara kutokana na sababu mbalimbali vikiwamo vifo au kampuni zao kufungwa.

Kidata alisema TRA inaamini hiyo itasaidia kuboresha huduma za ulipaji wa kodi na kuongeza ufanisi katika suala zima la usimamizi wa ukusanyaji mapato kwa kiwango cha juu ikiwa   na kufanya unafuu wa gharama za ulipaji wa kodi.

“Kwa kuanza hatua hii tumeanzia mikoa ya  kodi ya Dar es Salaam kwa maana ya Ilala, Temeke na Kinondoni na kutakuwa na vituo vitano.

“Katika Mkoa wa Ilala vituo vitakuwa katika ofisi ya Shauri Moyo na Jengo la 14Rays Gerezani, Mkoa wa Kinondoni vituo vitakuwa Jengo la LAPF Kijitonyama na Kibo Complex Tegeta na kwa Mkoa wa Temeke kituo kitakuwa katika Uwanja wa Taifa.

“Hatua hii itahusisha mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani na  itadumu kwa  miezi miwili na inamtaka kila mwenye TIN kufika yeye mwenyewe na katika ofisi za TRA na siyo kuwakilishwa na mtu mwingine,” alisema Kidata.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Hepautwa Investment and General Brocker Ltd, Nuru Hepautwa alisema serikali inatakiwa kuwachukulia hatua wafanyabiashara wote ambao wanakwepa kodi kwa makusudi kwa kuwa wanakiuka sheria.

Alisema hatua hiyo itasaidia kukuza mapato ya serikali hasa ikizingatiwa kuwa nchi nyingi zilizoendelea zimeendelea kwa sababu ya mapato hivyo kila anayestahili kulipa kodi alipe kwa mujibu wa sheria.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here