23.3 C
Dar es Salaam
Tuesday, October 3, 2023

Contact us: [email protected]

Maalim Seif, Dk. Shein wachambuliwa na wasomi

Rais wa Zanzibar, Dk. Ally Mohamed Shein
Rais wa Zanzibar, Dk. Ally Mohamed Shein

Na Veronica Romwald, Dar es Salaam

KITENDO cha Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad  kukataa kusalimiana na Rais wa Zanzibar, Dk. Ally Mohamed Shein, kimetafsiriwa kwa hisia tofauti katika jamii.

Viongozi hao walikutana juzi kwenye mazishi ya Rais wa awamu ya pili wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Abood Jumbe Mwinyi, ambako Maalim Seif alikataa kupokea mkono wa Dk. Shein wakati rais huyo alipokuwa akipita kusalimia viongozi mbalimbali waliohudhuria msiba huo.

Akizungumza na MTANZANIA, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine, Profesa Mwesiga Baregu, alisema hali hiyo imeonyesha kuwa Maalim Seif bado anamuona Dk Shein kuwa ni msaliti kwake.

“Si unakumbuka wakati ule wa uchaguzi mkuu, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Salum Jecha Salum, alitangaza kuufuta ule wa awali jambo ambalo Maalim Seif hakukubaliana nalo, wakakaa mezani wakajadiliana kwa vikao kama sita hata hivyo baadaye yalitokea yale yaliyotokea… uchaguzi ulifutwa rasmi na ukarudiwa upya.

“Kwa mantiki hiyo bado Maalim Seif anamuona Dk. Shein kwamba alimsaliti kiasi fulani na kwa utamaduni wetu Watanzania tumezoea ukimpa mtu mkono maana yake unamtambua naona ndiyo maana alikataa kumpa wa kwake,” alisema.

Profesa Baregu ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), alisema kwa kuwa hali imefikia hapo ni vema sasa Rais Dk. John Magufuli akaziita mezani pande zote mbili na kutafuta maridhiano.

“Rais Magufuli anayo nafasi nyingine ya kuanzisha mazungumzo ikiwa bado anahitaji Zanzibar iendelee kuwa shwari maana hali hii ni wazi kuwa hairidhishi,” alisema.

Alisema ana imani kuwa mazungumzo hayo yatasaidia kutafuta mwafaka visiwani humo.

“Atengeneze ajenda, awaite na achague njia ya kutafuta mwafaka huo ikishindakana ndipo  itabidi watafute msuluhishi ambaye atawaita na kuzungumza nao pia,” alisema.

Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya Maadili, Amani na Haki za Binadamu ya Madhehebu ya Dini zote, Askofu Willium Mwamalanga, alisema kitendo kile kimedhihirisha kuwa Zanzibar si salama.

“Picha ile ya jana (juzi) si nzuri, lakini hata marehemu mwenyewe (Aboud Jumbe) alikataa kuzikwa na chama pamoja na serikali na akaandika ujumbe mzito namna ile, ni lazima jambo hili litazamwe kwa kina, si ishara nzuri kwa maisha ya visiwa hivyo,” alisema.

Alisema hata hivyo dawa ya amani ya kuendelea kuwapo ipo mikononi mwa Rais Shein mwenyewe na chama chake.

“Viongozi wa dini tunaona kwamba kuendelea kukaa kimnya kwa serikali pasipo kutoa majibu kwa maswali yaliyoko kwenye mioyo ya watu kutaifikisha pabaya Zanzibar, lazima serikali ichukue hatua,” alisema.

Alisema wapo tayari kukutana na Rais Shein kwa ajili ya kushirikiana naye kutafuta mwafaka wa suala hilo na kwamba hakuna haja ya kutapatapa mahali pengine.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam , Profesa Kitila Mkumbo alisema  ingawa Seif ana hasira, alipaswa kuonyesha uungwana kwa kumsalimia Rais Shein katika msiba huo.

“Seif ameonyesha ana hasira lakini kupeana mikono ni uungwana naona alikosea kukwepa kusalimia na Dk. Shein…yaani anataka kuonyesha kuwa Zanzibar si shwari huku ikiwa si kweli kwani kitendo cha kufutwa uchaguzi ni suala la demokrasia na limegusa vyama vyote na si la Seif peke yake,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles