26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Wananchi wachangia maji na fisi, ng’ombe

cropped-fisi

NA BENJAMIN MASESE, MWANZA

BAADHI ya wananchi wa mitaa ya kata za Lwanima  na Kishili  wilayani Nyamagana wanachangia  maji ya visima vya asili  na fisi, ng’ombe na  mbweha kutokana na kukosa huduma kutoka  Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA).

Kitendo hicho kimeonekana kuleta hofu  kwa  wakazi hao wakidai kupatwa na magonjwa kwa sababu wamekuwa wakikuta vinyesi katika  visima vya maji.

Mbali ya  magonjwa, wanawake wengi wa mitaa hiyo wamekuwa wakiamka  kati ya saa 11.00 na 12.00 ri na kuacha watoto ndani kwa ajili  kuwahi kuchota maji  na   wengine wamekuwa wakikutana na fisi wakiwa visimani, jambo ambalo ni hatari kwa usalama wao.

Mpaka sasa tayari familia  moja ya Mwarabu Benard imepatwa na athari ya mtoto wao, Profipeli Mwarabu (miezi minane), kufariki dunia  hivi karibuni baada ya kuungua moto saa 12.00 asubuhi akiwa ndani ya nyumba wakati mama yake, Honatha Timatheo, akiwa amekwenda kuchota maji katika   visima hivyo.

Tukio hilo lilisababisha Mbunge wa   Nyamagana, Stanslaus Mabula (CCM)   na Mkurugenzi wa Mwauwasa,  Antony Sanga  kwenda katika   familia hiyo na kutoa mkono wa pole  pamoja na kutembelea mitaa yenye ukosefu wa maji na wakaahidi  kupeleka huduma hiyo haraka.

MTANZANIA ilitembelea baadhi ya visima vya asili katika mitaa  mbalimbali ya kata hizo pamoja na bonde la linalotenganisha Kata ya Lwanima na Kishili  kwa nyakati tofauti na kushuhudia jinsi wanawake  wanavyohangaika kugombania  maji.

Kisima kimoja cha asili maarufu kinachojulikana kwa jina la Kibundululu ambacho kinatumiwa na wakazi wa Bushitu, Kakebe, Majengomapya na Kilimo, kimekuwa msaada mkubwa kwa wananchi hao lakini ng’ombe wa maeneo hayo wamekuwa  wakinywa maji   mchana na kujisaidia humo.

Faustina Christopher ambaye ni miongoni mwa wanawake ambao huwahi   kuchota maji hayo, alisema  analazimika kuwahi alfajiri ili kupata maji masafi.

Alisema wakati mwingine amekuwa akikutana na fisi maeneo hayo.

Edna Samweli, alisema kutokana na kuwa na biashara yake ya mhagawa amekuwa akiwahi kwenda kisimani alfajiri kabla ya ng’ombe  kuyachafua kwa vile maji hayo wakati wa  mchana yamekuwa yakinuka kinyesi cha mifugo.

Hata hivyo visima vingine vilivyopo bonde linalotenganisha kata za Lwanima na Kishili vimekuwa na idadi kubwa ya wananchi wanaochota maji, huku  wafugaji nao wakitegemea kunywesha hapo.

Wakazi hao wameiomba Serikali hususan Mwauwasa, kuwapatia huduma ya maji ikizingatiwa wamekuwa wakiteseka kwa kiasi kikubwa wakati wa kiangazi, kama ilivyo sasa.

Akizungumza na MTANZANIA, Mkurugenzi wa Mwauwasa,  Sanga alisema   mamlaka imetenga  fedha kwa ajili ya kununua mabomba ya kusambaza maji.

“Tunaomba wananchi watuvumilie kwa kuwa tayari watalaamu wametembelea maeneo hayo na kuchukua takwimu za bomba zinazotakiwa kusambazwa.

“Tutaunganisha maji kutoka Mahina, kupitia Kakebe na kuelekea Majengomapya , Kilimo hadi Kanindo, kazi hii itaanza kufanyika ndani ya mwezi huu,”alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles