29.2 C
Dar es Salaam
Friday, May 3, 2024

Contact us: [email protected]

TRA yasisitiza Wafanyabiashara Chato kuzingatia sheria

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Geita imewataka wafanyabishara kufanya biashara zao bila woga wa sheria ya kodi badala yake wazingatie sheria kwa kulipa kodi kuchangia mapato serikalini.

Ofisa Elimu kwa Mlipa Kodi na Mawasiliano TRA mkoa wa Geita, Justine Katiti amebainisha hayo alipokutana na wafanyabiashara kata ya Muganza wilayani Chato kuhamasisha kampeni ya Tuwajibike.

Amesema serikali ya awamu ya sita chini ya Dk. Samia Suluhu Hassan inatamani kuona kila sekta ikiwemo sekta ya biashara inakua na hivo wafanyabiashara wawe huru na wazingatie sheria za nchi.

Katiti amesisitiza wafanyabiashara hao kuliwekea mkazo suala la kutunza kumbukumbu za biashara zao na kudai risiti za manunuzi, kutoa risiti za Mashine za Kielektroniki (EFD) kwa kila mauzo.

Amesema utunzaji wa gharama wanazotumia kwenye biashara zao inaweka msingi bora wakati wa kufanyiwa makadirio ya kodi, kulipa kodi stahiki na kupunguza migogoro ya kodi na kukuza biashara zao.

Amewakumbusha kuwa madhara ya kutotoa au kudai risiti yanasababisha Serikali kupoteza mapato yake na hivyo kurudisha nyuma mipango ya serikali ya kuleta maendeleo kwa wananchi wake.

Katiti amewashauri pia wafanyabiashara kurasimisha biashara zao kwa kufika TRA na kujisajili kwa kupatiwa namba ya utambulisho wa mlipakodi (TIN) ikiwa ni utambulisho wa biashara zao kisheria.

Ameongeza TIN namba pia inamwezesha mtu kupata leseni ya biashara, kupata mikopo kutoka taasisi za fedha na hata kuwa na fursa ya kushiriki masoko ya kimataifa na hivyo kujiongezea kipato.

Mwenyekiti wa Kata ya Muganza wilayani Chato, James Mpanduji alikiri ekampeni ya Tuwajibike inayoratibiwa na TRA imewaleta pamoja wafanyabisahara, wananchi na serikali kwa ujumla.

Amesema kupitia kampeni hiyo wamekumbushwa wajibu wao kama walipakodi na madhara ya kutofuata sheria za kodi ikiwemo kutotoa risiti za EFD na kuahidi kuendelea kuiunga mkono TRA.

Ameomba elimu iendelee kutolewa zaidi hasa kuhusu mabadiliko mbalimbali ya sheria yanayotokea ili kuwafanya wasibakie wahanga wa sheria hizo kiasi cha kupelekea kutozwa adhabu na hata kufilisika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles